Ticker

6/recent/ticker-posts

WHO yaendesha kampeni ya "Afya yangu, haki yangu



#PICHA:Juliana Germano, mtaalamu wa afya kutoka Chama cha maendeleo ya familia Msumbiji, (AMODEFA) ndani ya kliniki tembezi.

Katika maadhimisho ya kuanzishwa kwake hii leo, Shirika la Afya Duniani WHO linazitaka nchi kuwekeza, kukabiliana na ubaguzi na kutovumiliana, na kupanua wigo wa upatikanaji sawa wa huduma bora za afya.

Katika maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka  7 Aprili mwaka huu , WHO inaendesha kampeni ya “Afya yangu, haki yangu” ili kutetea haki ya afya ya kila mtu, kila mahali.

Kwa mujibu wa WHO kampeni hiyo inatetea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, na taarifa kwa wote, pamoja na maji safi ya kunywa, hewa safi, lishe bora, makazi bora, mazingira bora ya kazi na uhuru dhidi ya ubaguzi.

Kote duniani, changamoto kuu zinazoathiri haki ya afya mara kwa mara ni kutochukua hatua za kisiasa pamoja na ukosefu wa uwajibikaji na ufadhili, unaochangiwa na kutovumiliana, ubaguzi na unyanyapaa.

Shirika hilo linasema watu wengi wanaokabiliwa na kutengwa au mazingira magumu wanateseka zaidi, kama vile watu wanaoishi katika umaskini, waliokimbia makazi yao, wazee au watu wanaoishi na ulemavu.

 Vita inachochea kukosa haki ya afya

Kwa mujibu wa shirika hilo la afya duniani wakati kutochukua hatua na dhuluma ni vichochezi vikubwa vya kushindwa kwa kimataifa kutoa haki ya afya, migogoro ya sasa inaongoza kwa ukiukwaji mkubwa wa haki hii. Migogoro inaacha njia za uharibifu, changamoto ya kiakili na ya mwili, na vifo.

Limeongeza kuwa matumizi ya wa nishati ya mafuta kisukuku wakati huo huo yanachochea janga la mabadiliko ya tabianchi na kukiuka haki yetu ya kupumua hewa safi.

Pia limeongeza kuwa janga la mabadiliko ya tabianchi linasababisha hali mbaya ya hewa ambayo inatishia afya na ustawi katika sayari nzima na kuzorotesha upatikanaji wa huduma ili kukidhi mahitaji ya msingi.

Kila mtu anastahili kupata huduma bora za afya, kwa wakati unaofaa na zinazofaa, bila kubaguliwa au matatizo ya kifedha. Limesisitiza shirika hilo.

Hata hivyo limesema mwaka 2021, watu bilioni 4.5, zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote ulimwenguni, hawakupata huduma muhimu za afya, na kuwaacha katika hatari ya magonjwa na majanga.

Hata wale wanaopata huduma mara nyingi hupata changamoto za kiuchumi, huku takriban watu bilioni 2 wakikabiliwa na ugumu wa kifedha kutokana na gharama za afya, hali ambayo imekuwa mbaya zaidi kwa miongo miwili.

Dola bilioni 328 zinahitajika kwa ajili ya afya

Ili kupanua wigo wa huduma, WHO inasema dola bilioni 200-328 za ziada kwa mwaka zinahitajika duniani kote kuweza kuongeza huduma za afya ya msingi katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati yaani asilimia 3.3 ya matarajio ya pato la taifa.

Maendeleo yameonyesha kuwa inawezekana pale ambapo kuna utashi wa kisiasa. Tangu 2000, nchi 42, zinazowakilisha kanda zote na viwango vya mapato, zilifanikiwa kuboresha huduma za afya na ulinzi dhidi ya matumizi mabaya ya afya.

“Kutambua haki ya afya kunahitaji serikali kupitisha na kutekeleza sheria, kuwekeza, kushughulikia ubaguzi na kuwajibishwa na watu wao,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Ameongeza kuwa “WHO inafanya kazi na serikali, washirika na jamii ili kuhakikisha kiwango cha juu zaidi cha afya kinachofikiwa, kama haki ya msingi kwa watu wote, kila mahali.”

Haki ya afya imewekwa ndani ya Katiba ya WHO, na angalau nchi 140 zinatambua haki ya afya katika katiba zao za kitaifa.

Lakini utambuzi pekee hautoshi, amesema ndiyo maana WHO inaunga mkono nchi kutunga sheria za haki ya afya katika sekta zote na kuunganisha haki za binadamu katika sera na programu za afya. 

Amesema lengo la msaada huu ni kufanya huduma za afya zipatikane, ziweze kufikiwa na kukidhi mahitaji ya watu wanaowahudumia na kuongeza ushiriki wa jamii katika kufanya maamuzi ya afya.

Wakati wa siku ya afya duniani 7 Aprili 2023, walinda amani wa UN kutoka kikosi cha Tanzania cha kutoa msaada wa haraka, TANZQRF katika kwneye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO nchini DRC wametoa huduma za kupima magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa wakazi wa kijiji cha Nzuma mjini Beni, huko Kivu Kaskazini.

Serikali ziwekeze katika afya

Katika Siku hii ya Afya Duniani na ziku zijazo, WHO inatoa wito kwa serikali kufanya uwekezaji wa maana ili kuongeza huduma za afya ya msingi, kuhakikisha uwazi na uwajibikaji na kuhusisha watu binafsi na jamii kwa kina katika kufanya maamuzi kuhusu afya. 

Shirika hilo linasema kwa kutambua uhusiano uliopo kati ya haki ya afya na haki nyingine za msingi, kampeni hiyo inajumuisha wito wa kuchukua hatua kuhusu fedha, kilimo, mazingira, haki, usafiri, kazi na masuala ya kijamii.

Watu binafsi, jumuiya na mashirika ya kiraia kwa muda mrefu wametetea haki yao ya afya, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa kuondoa vikwazo na kutetea usawa.

WHO inahimiza umma kujua, kulinda na kuendeleza haki zao za afya, ikiwa ni pamoja na zile zinazohusiana na huduma salama na bora, kutobagua, faragha na usiri, taarifa, uhuru wa mwili, na kufanya maamuzi.



Post a Comment

0 Comments