WHO yaitangaza Cape Verde kutokomeza Malaria
Shirika la afya ulimwenguni WHO, limeitangaza Cape Verde kuwa nchi ya tatu barani Afrika kutokomeza ugonjwa wa Malaria, wakati ambapo ugonjwa huo bado unaendelea kuwaua maelfu ya watu barani humo.
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amekipongeza kisiwa hicho kwa dhamira isiyoyumba na ustahimilivu katika safari yake ya kutokomeza maradhi hayo.
Kisiwa hicho chenye wakaazi wapatao laki tano kinafuatia nchi za Mauritius na Algeria ambazo zimetangazwa kudhibiti Malaria. Duniani kote, nchi takribani 43 zimeorodheshwa na WHO kudhibiti ugonjwa huo.
Shirika hilo linakadiria kwamba watu laki sita ulimwenguni kote walifariki kwa Malaria mwaka 2022 na milioni 250 waliambukizwa.
Ugonjwa huo umeathiri pakubwa bara la afrika ambako mwaka 2021 zaidi ya asilimia 90 ya vifo na maambukizi yaliripotiwa. Watoto chini ya umri wa miaka mitano ndio hufariki zaidi.
Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Matshidiso Moeti, amesema “mafanikio ya Cape Verde ni mwanga wa matumaini kwa kanda ya Afrika na kwingineko. Inadhihirisha kuwa kwa utashi thabiti wa kisiasa, sera madhubuti, ushirikishwaji wa jamii na ushirikiano wa sekta mbalimbali, kutokomeza malaria ni lengo linaloweza kufikiwa.”
Kampeni za kupambana na Malaria
Malaria huambukizwa kwa njia ya mbu jike na hupatikana zaidi katika nchi za kitropiki. Dalili za ugonjwa huo ni kichwa kuuma na homa na unaweza kusababisha kifo ndani ya saa 24.
Kampeni za kupambana na malaria kwa kiasi kikubwa zimejikita katika kujikinga kupitia vyandarua na dawa za kinga, pamoja na kampeni za kutokomeza ugonjwa huo kwa kutumia dawa za kuulia wadudu. Tangu mwaka 2021WHO imependekeza chanjo mbili tofauti.
Utokomezaji wa Malaria katika kisiwa hicho kumetajwa na WHO kuwa kutavutia wageni zaidi na kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi katika nchi ambayo utalii unachangia asilimia 25 ya pato la taifa.
Kulingana na WHO, kabla ya miaka ya 1950, visiwa vyote 10 nchini humo viliathiriwa na malaria na milipuko mikali ya mara kwa mara ilizuka katika maeneo yenye watu wengi zaidi.
Chanjo ya Malaria Afrika: Chanjo ya Malaria kuanza kutumika Ghana na kutoa matumaini ya kudhibiti ugonjwa huo hatari barani Afrika
Kupitia mpango wa unyunyiziaji dawa, nchi hiyo ilifanikiwa kutokomeza malaria mara mbili mwaka 1967 na 1983, lakini kukosekana kampeni ya madhubuti ya kutokomeza maradhi hayo kulisababisha kuzuka kwa ugonjwa huo kila mara.
Kutokomeza malaria kumekuwa ni lengo la kitaifa la visiwa hivyo tangu 2007, na kusababisha mpango mkakati wa malaria kutoka 2009 hadi 2013.
Mpango huo ulijikita katika utambuzi, matibabu ya mapema na madhubuti, kuripoti na uchunguzi wa visa vyote, huku mamlaka za Cape Verde ziliendelea kuwa makini wakati wa janga la Covid-19.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!