Fahamu kuhusu meli ya MV Clarias iliyopinduka Ziwa Victoria
“Kilisikika kishindo cha kamba zinazoishikilia meli zikikatika.” Ni kauli ya Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Abdulrahman Salim akisimulia tukio la meli ya Mn Clarias iliyopinduka ikiwa kwenye gati la bandari ya Mwanza Kaskazini jijini humo.
Meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 290 na tani 10 za mizigo, ilijengwa mwaka 1961 na wataalamu kutoka Uingereza na imekuwa ikifanya safari zake kati ya mwalo wa Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza na Kisiwa cha Goziba wilayani Muleba mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa Salim, wakati meli hiyo inapinduka hakukuwa na mtumishi wala mizigo iliyokuwemo.
Salum amesema kufuatia tukio hilo huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya maeneo inapotoa huduma meli hiyo, zimesitishwa ili kupisha uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo.
“Hadi saa 9 usiku meli hiyo bado ilikuwa inaelea kwenye maji lakini ilipofika kati ya saa 10 kuelekea 11 alfajiri ya leo, kilisikika kishindo cha kamba zinazoshikilia meli kama zinakaza na kukatika, ndipo watu waliposhtuka kwenda kuangalia wakakuta inalalia upande wa ziwani,” amesema Salim.
Amesema tangu Januari 2024, Mv Clarias inayofanya safari zake ndani ya Ziwa Victoria ilikuwa inatoa huduma ya usafirishaji kati ya Mwanza na Goziba mara mbili kwa wiki (Jumatatu na Ijumaa).
“Baada ya kufika Mwanza katika mwalo wa Kirumba inashusha abiria na mizigo na kuja hapa Bandari ya Mwanza Kaskazini kwa ajili ya kulala, hapa ndiyo sehemu tunayoamini ni salama zaidi, kwa hiyo jana meli ilitoka mwalo wa Kirumba na kuegeshwa hapa lakini kufikia huo muda ikapinduka,” amesema Salim.
Akizungumzia athari za tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uhusiano kwa Umma wa MSCL, Anselm Namala amesema mbali na kusitisha huduma ya usafiri, tukio hilo limekwamisha safari za meli ya Mv Butiama inayotokea Bandari ya Mwanza Kaskazini kwenda Ukerewe mkoani humo.
“Kutokana na kupinduka kwa MV Clarias katika bandari yetu, tumesitisha safari za meli nyingine ya Mv Butiama inayotoa huduma kati ya Mwanza na Ukerewe kwa sababu eneo ambalo meli hii imepindukia ndipo ambapo Mv Butiama inageuzia. Baada ya kuinasua safari zitaendelea kesho,” amesema Namala.
Amesema tayari timu ya wataalam kutoka MSCL, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Shirika la Uwakala wa Meli (Tasac) wamewasili katika bandari hiyo kwa ajili ya kuinasua na kuipandisha katika cherezo lililoko Bandari ya Mwanza Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo.
“Taarifa za awali bado hazijabaini chanzo cha tukio hili, lakini tunapambana kuinasua kutoka majini na kuipandisha kwenye cherezo ili kuikagua kubaini chanzo chake, tutatoa taarifa kwa umma baada ya uchunguzi kukamilika,” amesema Namala.
Tukio la kwanza
Akisimulia kisa hicho, Salim anasema hilo ni tukio la kwanza kwa meli hiyo kupinduka tangu ujenzi wake ukamilike na kuanza kutoa huduma mwaka 1961 huku akisisitiza kwamba jambo hilo limewashtua kwani siyo rahisi kwa meli ya aina ya Clarias aliyoiita ya ‘kipekee’ kukumbwa na kisa cha aina hiyo.
“Katika meli ambazo wataalamu wa MSCL hawana mashaka nayo ni MV Clarias kutokana na umbile lake lilivyo, ambalo ni la Kalai, tofauti ya Mv Butiama ambayo ina umbile la V ambalo ni rahisi kupinduka. Kwa kisa hiki cha Mv Clarias watalaamu bado hawajapata majibu,” amesema.
Abiria wafunguka
Mkazi wa Ukerewe mkoani Mwanza, Florah Tale amesema tukio hilo mbali na kumshtua, limemkwamisha kusafiri kwenda Ukerewe na hivyo ameomba mamlaka husika kuinasua meli hiyo ili kutoa mwanya kwa Mv Butiama kuendelea kutoa huduma.
“Hofu yetu ni kwamba endapo kungekuwa na abiria, maana yake ingeleta madhara makubwa lakini imeleta madhara kwetu, tumekosa usafiri kwenda kwenye makazi yetu. Wajitahidi kufanya ukarabati na ukaguzi wa mara kwa mara ili kuimarisha usalama wa abiria ambao tunategemea vyombo hivi,” amesema Florah.
Abiria mwingine, Mussa Katwale ameeleza kuingiwa na hofu kutokana na tukio hilo huku akiomba vyombo vinavyotoa huduma ndani ya Ziwa Victoria kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa abiria.
“Tukio la chombo kupata hitilafu hivi ni mara ya kwanza kulishuhudia, sina maelezo ya kina kuhusu chanzo ni nini lakini imenishtua. Tumekuwa tukishuhudia vivuko ndiyo vinapata changamoto kama hizi, hofu ipo kwa kiasi fulani kwetu wakazi wa visiwani tunaotegemea meli kufika katika makazi yetu lakini hatuna namna,” amesema Katwale.
Mwananchi imefika bandari ya Mwanza Kaskazini na kushuhudia meli hiyo ikiwa imepindukia upande wa kushoto wa gati la bandari hiyo huku watumishi wa MSCL na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) wakiendelea na jitihada za kuinasua kutoka majini.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!