Majokofu ya nyumbani yabainika kuhifadhia damu Korogwe

Majokofu ya nyumbani yabainika kuhifadhia damu Korogwe.

Aprili 10, 2024 ilibainika ukiukwaji wa manunuzi ya vifaatiba ikiwemo majokofu mawili ya kuhifadhia damu katika kituo cha afya Mwalugulu katika Halmashauri ya Msalala.

Mwezi mmoja baada ya kubainika jokofu la matumizi ya nyumbani kuhifadhia damu katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, hilo limebainika tena mkoani Tanga.

 Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali (Tamisemi), Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Rashid Mfaume akiwa katika ziara ya usimamizi shirikishi katika Mkoa wa Tanga amebaini jokofu la matumizi ya nyumbani likitumika kuhifadhia damu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Korogwe (Magunga).

Kutokana na hilo, Dk Mfaume ameelekeza kufanyika utaratibu wa haraka wa upatikanaji wa jokofu maalumu kwa ajili ya kuhifadhia damu.

“Hili jokofu ambalo mnatunzia damu ni kama tulilolikuta kule na hii tumeletewa na mdau, tumetoka kule Shinyanga, Mwalugulu tumewasema tukajua huku mmejifunza mtahangaika. Hatutaki kuona haya yanayofanyika huku tuyaone sehemu nyingine,” amesema.

“Mnaonekana Korogwe TC (Halmashauri ya Mji) mna wataalamu wa kununua majokofu ya nyumbani, maabara tumeenda tumekuta majokofu sita,” amesema Dk Mfaume.

Aprili 10, 2024 Dk Mfaume alibaini ukiukwaji wa ununuzi ya vifaatiba yakiwamo majokofu mawili ya kuhifadhia damu Kituo cha Afya Mwalugulu katika halmashauri hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk Rashid Mfaume akitizama jokofu linalotumika kuhifadhia damu.

Akiwa kwenye ziara kukagua na kuangalia usimamizi shirikishi wa shughuli za huduma za afya ndani ya kituo hicho cha afya, Dk Mfaume amebaini majokofu hayo yaliyonunuliwa kila moja kwa Sh3.8 milioni ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Pia, amebaini mashine ya dawa za usingizi (Anaesthetic Machine) iliyonunuliwa kwa Sh140 milioni imepokewa katika kituo hicho bila kukaguliwa.

“Tunaponunua vifaa vya hospitali ni tofauti na  vingine, tunakuwa na viwango vyetu ambavyo tunaainisha wakati wa kuagiza, hata yale majokofu ambayo tunahifadhia damu si kama haya ambayo tunahifadhia matunda, tunahifadhia ubwabwa nyumbani, yale yanakuwa mazuri kufanya ile damu iendelee kuwa na ubora ule wa viwango vya joto na vingine,” amesema Dk Mfaume alipozungumza na gazeti hili.

Dk Mfaume amesema majokofu hayo yalitarajiwa kutumiwa mwezi ujao baada ya huduma za damu salama kuanza katika kituo hicho cha afya.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Hamisi Katimba bila kutaja hatua gani za awali zilizochukuliwa, amesema tayari uchunguzi umeanza na watakaobainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!