Mizozo na majanga yahusianayo na tabianchi yamefanya elimu kusalia ndoto

Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati kuivusha Afrika – Guterres

Profesa Amivi Kafui Tete-Benissan (kushoto) ambaye anafundisha biolojia na kemia kwenye chuo kikuu cha Lomé, Togo, pia ni mwanaharakati ambaye anachagiza wasichana kushirika kazi za sayansi.

“Afrika Tuitakayo” haina budi kuungwa mkono na mifumo ya elimu ambayo Afrika inahitaji, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wakati wa moja ya kikao cha ngazi ya juu cha Mlolongo wa Mijadala ya Afrika iliyokunja jamvi hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Mlolongo huo wa mijadala uliofanyika kwa mwezi mzima ukiwa umeandaliwa na Ofisi ya Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Afrika, UNOSAA, ulijikita katika marekebisho ya mfumo wa elimu ambapo Guterres amesema maudhui hayo yanakumbusha kuwa kuwezesha bara la Afrika kustawi, kiambato muhimu ni elimu.

Katika kikao hicho cha leo kilichomulika Elimu kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kuelekea Afrika Tuitakayo, Guterres amesema elimu ni kichocheo cha ustawi na maendeleo ya Afrika na ndio injini ya fursa kwa vijana wa kiafrika na zaidi ya yote elimu inaunganisha waafrika na urithi wa utamaduni wa zamani huku ikiwaandaa kwa siku zijazo.

Hata hivyo amesema mizozo na majanga yahusianayo na tabianchi yamefanya elimu kusalia ndoto kwa mamilioni ya watoto na vijana barani Afrika, huku kukiwa hakuna walimu wenye sifa zinazotakiwa na mbinu za kufundishia zinashindwa kuwaandaa wanafunzi kwa ajira kwenye zama za dunia ya sasa hasa kwa kuzingatia umuhimu wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati au STEM.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia Kikao cha ngazi ya juu cha kisera cha mlolongo wa mijadala ya Afrika kwa mwaka huu wa 2024 kikimulika Kufikia Afrika tuitakayo kupitia Sayansi, Teknolojoia, na Ugunduzi.

Guterres anapigia chepuo ufadhili zaidi kwenye mifumo ya elimu na zaidi ya yote msingi wa mifumo ya elimu barani Afrika ijikite kwenye STEM.

“Kuongeza idadi ya watoto shuleni pekee haitoshelezi, kinachohitajika ni stadi na ufahamu zaidi wa kuweza kushindana kwenye uchumi wa kisasa wa dunia,” amesema Guterres.

Rais wa Baraza Kuu naye apazia sauti Sayansi, Teknolojia na Ugunduzi

Balozi Dennis Francis ambaye ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa pamoja na kuunga mkono hoja ya kusongesha STEM na ubia katika kuimarisha mfumo wa elimu Afrika, yeye ametanabaisha kuwa sayansi, teknolojia na ugunduzi (STI)  vitaziba pengo la kidijitali  na hivyo kuchochea suala la kupata elimu bora Afrika, na kuimarisha tafiti na kupunguza kasi ya wasomi wa Afrika kukimbia bara lao.

“Tukiwa na mwelekeo tulioazimia, STI inaweza kuchochcea maendeleo ya viwanda Afrika na kuleta mabadiliko mapana ya kiuchumi ambayo yanaweka fursa zaidi na bora za ajira kwa watu wote,” amesema Balozi Francis.

Amenukuu maneno ya Hayati Nelson Mandela ya kwamba Elimu ndio silaha yenye nguvu zaidi tunayoweza kuitumia kubadilisha dunia.

Via-UN

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!