Ticker

6/recent/ticker-posts

Saratani ya uume inaonekana kuongezeka kwa kiwango cha kutisha katika miaka ya hivi karibuni



Saratani ya uume inaonekana kuongezeka kwa kiwango cha kutisha katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka 2018, João, mwenye umri wa miaka 63, alianza kugundua maumivu kwenye uume wake.

“Nilianza kutembelea kliniki ili kujua ni nini, lakini madaktari wote waliniambia ni kutokana na ngozi ya ziada na kunipatia dawa ,” anakumbuka mzee huyo mwenye umri wa miaka 63.

Licha ya dawa hiyo ngozi iliendelea kuvimba.

Hii ilianza kumuathiri João na ndoa yake na mkewe hususan katika Swala la kufanya tendo. “Tulikuwa kama ndugu,” anakiri.

Kwa miaka mitano, João (sio jina lake halisi) alitembelea wataalamu wengi ambao walimuandikia dawa zaidi na kuagiza afanyiwe uchunguzi wa kina kubaini ni nini kinachoendelea katika uume wake. “Hakuna kitu kilichoweza kutatuliwa,” alisema.

Kisha, mnamo 2023, waliweza kupata utambuzi: João alikuwa na saratani ya uume .

“Kwa familia yangu ilikuwa kitu kibaya sana, hasa kwasababu walilazimika kukata sehemu ya uume wangu. ” Nahisi kama nimekatwa kichwa,” anasema.

“Ni aina ya saratani ambayo huwezi kuzungumza na watu kuihusu kwa sababu inaweza kuwa Aibu.”

Ukweli ni kwamba saratani ya uume ni nadra, lakini matukio na viwango vya vifo vinaongezeka duniani kote.

“Hofu kuhusu upasuaji”

Kulingana na tafiti za hivi karibuni, Brazil, ambapo João anatoka, ina moja ya viwango vya juu vya saratani ya uume ulimwenguni: kuna idadi ya 2.1 kwa wanaume 100,000.

Kati ya mwaka 2012 na 2022, visa 21,000 viliripotiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Brazil.

Hii imesababisha vifo vya watu 4,000 na 6,500 kukatwa uume wao katika kipindi cha miaka kumi iliyopita: mmoja kila baada ya siku mbili.

Dalili za saratani ya uume mara nyingi huanza na vidonda ambavyo haviponi na mara nyingi huwa na harufu mbaya.

Wakati utambuzi wa mapema wa ugonjwa huo unafanikiwa, kuna uwezekano mkubwa wa kupona kupitia taratibu kama vile upasuaji, na tiba za mionzi za radiotherapy au chemotherapy.

Lakini ikiwa haitatibiwa, inaweza kusababisha kukatwa kwa sehemu au uume wote kwa ujumla na labda hata viungo vingine vya siri kama vile korodani.

João alilazimika kufanyiwa upasuaji wa sehemu ya uume wake mwezi Januari mwaka jana. Kwake ulikuwa ni wakati mgumu.

“Sikuwahi kufikiria kwamba nitasumbuliwa na ugonjwa. Na ni kitu ambacho huwezi kumwambia kila mtu, “anafafanua.

“Niliogopa sana kuhusu upasuaji, lakini hakukuwa na njia nyingine. Hisia katika wiki za kwanza zilikuwa huzuni. Siwezi kukataa. Kuachwa bila sehemu ya uume wako ni jambo la kutisha.”

Kwa wagonjwa wengine suluhisho pekee ni kukatwa kwa uume. Ni kitu ambacho kinabadilisha maisha milele.

Thiago Camelo Mourão, kutoka idara ya tiba ya uzazi ya wanaume-(urolojia) ya Kituo cha Saratani cha Sao Paulo, anasema kuwa “ikiwa kuna kukatwa kwa sehemu, mkojo unaendelea kutoka kwa uume.”

“Katika kisa cha kukatwa kabisa, njia ya mkojo inaweza kuhamishwa kwa sehemu ya mwili, kati ya scrotum(mfuko wa korodani unaobeba mbegu za kiume) na njia ya haja kubwa, na kusababisha mgonjwa kukojoa akiwa ameketi chooni.”

Inasababishwa na nini?

Kulingana na wataalamu, kuna sababu kadhaa za hatari ambazo zinaweza kusababisha saratani ya uume, kama vile phimosis – ugonjwa ambao huzuia ngozi ya uume kuondolewa – au uvutaji wa sigara.

Mauricio Dener Cordeiro, mtaalamu aliyebobea katika mada hii ya tiba ya uzazi kwa wanaume, anasema kuwa usafi binafsi ni muhimu sana katika ugonjwa huu.

“Kutokufunua ngozi ya uume na kutosafisha ngozi inayozunguka vizuri, hii husababisha kutokwa na maji maji ambayo hukusanyika na kusababisha maambukizi ya bakteria,”

“Ikiwa hii itatokea mara kwa mara, inakuwa sababu ya hatari ya kutokea kwa uvimbe ,”

Lakini pamoja na usafi, Cordeiro anasema kuwa maambukizi ya mara kwa mara na virusi vinavyosababisha magonjwa ya zinaa au Human papilloma yanaweza kuwa moja ya “sababu kuu za hatari.”

Katika baadhi ya matukio, virusi vya Human papilloma vinaweza kusababisha saratani ya mdomo na uume.

“Chanjo dhidi ya virusi vya Human papilloma ni muhimu kutokana na ufanisi wake mkubwa katika kuzuia majeraha yanayohusiana na aina hii ya ugonjwa,”

Kuongezeka kwa visa

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, idadi ya juu zaidi ya visa vya maambukizi duniani imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Mnamo 2022, jarida la JMIR la Afya ya Umma lilichapisha matokeo ya uchambuzi mkubwa unaohusisha habari kutoka angalau nchi 43.

Idadi ya juu zaidi ya wagonjwa wa saratani ya uume kati ya 2008 na 2012 iligunduliwa kuwa nchini Uganda (2.2 kwa wanaume 100,000) ikifuatiwa na Brazil (2.1 kwa 100,000) na Thailand (1.4 kwa 100,000).

Nchi iliyo na visa vya chini zaidi vya maambukizi ilikuwa Kuwait (0.1 kwa 100,000)

“Ingawa nchi zinazoendelea ni mahali ambapo visa nyingi hutokea, viwango vya ongezeko kubwa katika miaka ya hivi karibuni huonekana katika nchi za Ulaya,” unaeleza utafiti kutoka Chuo Kikuu cha China, kinachoongozwa na wasomi Leiwen Fu na Tian Tian.

Kwa mfano, ripoti hiyo inasema kuwa Uingereza imeshuhudia ongezeko la visa vya saratani ya uume kutoka visa i 1.1 kwa wanaume 100,000 hadi 1.3 kwa 100,000 katika kipindi cha miaka 30.

Ujerumani ilishuhudia ongezeko la asilimia 50 ya visa vya maambukizi kati ya mwaka 1961 na 2012.

Ukweli ni kwamba idadi hiyo inaongezeka na ikiwa hii itaendelea, ifikapo 2050 kutakuwa na kesi zaidi ya 70% ikilinganishwa na idadi ya sasa.

Mabadiliko haya yanaweza kuhusishwa kwa kiasi kikubwa na kuzeeka kwa idadi ya watu, kulingana na wataalam, ambao wanasema kuwa matukio ya juu zaidi yalitokea kwa wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

“Ugonjwa wa saratani ya uume ni ugonjwa adimu lakini pia unaweza kuzuilika sana. Ni muhimu kwa wanaume wa rika zote kuosha uume wao kwa sabuni na maji kila siku na baada ya tendo la ndoa,” anabainisha Cordeiro.

Kwa sasa, João anasubiri matokeo ya vipimo vyake vya hivi karibuni, ambavyo atapokea mwishoni mwa mwaka huu. “Nina uhakika kwamba vipimo hivi vitaonyesha kuwa nitapona,” anasema.

Kulingana na Utafiti wa Saratani Uingereza, zaidi ya 90% ya wanaume wanaogunduliwa na saratani ya uume ambayo haijaeneawana uwezekano wa kuishi karibu miaka mitano au zaidi.

“Sasa kwa kukatwa viungo, maumivu yamekwenda na ninahisi vizuri zaidi. Lakini nitalazimika kukabiliana na kukatwa sehemu ya uume wangu kwa siku zangu zote.”.



Post a Comment

0 Comments