Wakunga ni matumaini kwa wajawazito na watoto wachanga

Yemen: Wakunga ni matumaini kwa wajawazito na watoto wachanga licha mzozo na janga la tabianchi

UNFPA ilikarabati kituo cha afya cha Shahir mwaka wa 2021 kwa kuongeza dawa na vifaa vya matibabu, pamoja na makumi ya wakunga waliofunzwa na sasa wanatoa huduma mbalimbali za kina.

Mona alipoanza kufanya kazi ya ukunga katika kituo cha afya mtaani anapoishi miaka 30 iliyopita, alikuwa wa kwanza katika jimbo la Hadramout nchini Yemen.

“Wakati huo, eneo letu lilikuwa nyuma sana katika huduma za afya ukilinganisha na ulimwengu wa sasa,” aliliambia shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA. Kwa sasa Mona ni kiongozi wa idara ya wataalam wa ukunga katika kituo cha afya cha Shahir huko Hadramout.  Aliielezea jinsi jamii yake ilivyokuwa masikini, kukosa shule, vituo vya matibabu na wahudumu wa afya.

“Wanawake walikumbana na ujauzito bila huduma au ufuatiliaji unaofaa. Licha ya nia njema ya mkunga wa jadi, alikumbwa na vikwazo vya rasilimali,” aliongeza Mona. “Huduma nyingi za uzazi zilikumbwa na matatizo. Haikuwezekana kufika hospitali iliyopo mjini kutokana na gharama, usafiri, na kutokuwepo kwa ufahamu wa kutosha.”

Fatima, si jina lake halisi, ni mgonjwa katika kituo cha afya anakofanya Mona, alithibitisha maelezo haya ya hali ilivyokuwa awali: “Uhai kwa mama na mtoto ulitegemea bahati tu”.

Yemen ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi vya vifo vya uzazi duniani, na ni kituo kimoja tu kati ya vitano vinavyofanya kazi kwa sasa kinatoa huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga.

Yemen ina viwango vya juu vya vifo vya wajawazito

Yemen ina mojawapo ya viwango vya juu zaidi ya vifo vya akinamama duniani, na ni kituo kimoja tu kati ya vitano kinachotoa huduma za afya ya akinamama wanaojifungua . Takribani watu milioni 17.8 wanahitaji msaada wa huduma za afya, kati yao wakiwa ni wanawake milioni 5.5 wanaohitaji huduma za afya ya uzazi, mwaka huu.

Baada ya kumaliza shule, Mona alipata hamasa ya kubadilisha hali hiyo na akajisajili katika mafunzo ya ukunga katika mji jirani wa Mukalla. Mara tu kituo cha afya cha Shahir kilipofunguliwa kitongojini mwake, hakusita kuomba kazi.”Licha ya ufadhili mdogo na wafanyakazi wachache, tulipigania kwa udi na uvumba ustawi wa wanawake wetu.”

Wakiwa msingi wa huduma za afya za uzazi na jinsia katika jamii, wakunga wana umuhimu mkuu kwa kufanikisha huduma za afya katika mazingira yenye migogoro, hususan kwa walio katika mazingira magumu zaidi.

Ukosefu wa usawa katika mabadiliko ya tabianchi

Mona alikumbuka siku ya kutisha mwaka 2015, wakati kimbunga Chapala kilipiga Yemen mapigano yalipokuwa yakianza. Yeye pamoja na timu kutoka kituo afya anakofanya kazi, alisema, “tulivuka maeneo hatari kwa miguu ili kufikia watu waliokuwa katika madhila.”

Licha ya upepo mkali na ukosefu wa umeme , “wazo la maisha ya watu watatu yaliyokuwa hatarini, yaani mwanamke aliyekuwa katika maumivu ya kujifungua mapacha, lilichochea azimio letu na tuliwafikia kwa wakati.”

Wakati majanga ya tabianchi yanapotokea au mzozo unapoibuka, wakunga mara nyingi huwa wa kwanza kutoa msaada, ikiashiria njia moja yenye ufanisi zaidi ya kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika vya kina mama. Utafiti unaonyesha kuwa janga la tabianchi huleta tishio la kipekee kwa wanawake na wasichana, kwani majanga haya yanaweza kusababisha matatizo ya ujauzito na yanaongeza hatari kama mtoto kuzaliwa njiti au mimba kuharibika.

Huduma za mama na mtoto Yemen sasa ni bure

Kwa ufadhili kutoka Muungano wa Ulaya (EU), UNFPA iliimarisha kituo cha afya cha Shahir mwaka 2021 kwa kukipatia dawa, vifaa vya  matibabu na kufadhili mafunzo kwa wafanyakazi wa afya. Tangu wakati huo, viwango vya vifo vya akinamama wajawazito katika eneo hilo vimepungua. Hii ni kwa sababu  wakunga waliofundishwa sasa wanatoa huduma kamili – ikiwa ni pamoja na elimu ya afya ya uzazi na huduma za upasuaji kwa wajawazito. Wana gari la kubebea wagonjwa, chumba cha upasuaji kilichojaa vifaa, na dawa zinazotolewa bure.

“Baada ya uharibifu kutokana migogoro na majanga ya tabianchi, ilikuwa kama ndoto,” alisema Mona. “Familia katika eneo hili, watu waliotawanywa wakikimbia mapigano na mafuriko, waliweza kupata faraja hapa.”

Mona alipoanza kufanya kazi kama mkunga katika kituo cha afya cha eneo lake miaka 30 iliyopita, alikuwa wa kwanza katika Jimbo la Hadramout la Yemen.

Sababu za uwekezaji: Idadi ya wakunga inapungua

Tangu mwanzo wa 2024, UNFPA imewafikia zaidi ya watu 350,000 nchini Yemen na kuwapa huduma za dharura za afya, ulinzi na maarifa ya uzazi na jinsia, pamoja na kuunga mkono zaidi ya vituo 100 vya afya.

Wakunga ni sehemu muhimu ya huduma hii, wakiwa  watunzaji wenye ufahamu wa kitamaduni,  na viongozi wa jamii wanaotoa msaada wa dharura. Lakini dunia imepungukiwa na wakunga takriban milioni moja: Kutokuwepo kwa dhamira ya kimataifa ya kuwekeza katika mafunzo yao, maendeleo na uungaji mkono kunapunguza uwezo wao na kuwaweka wanawake na wasichana wanaowategemea katika hatari.

Mazingira  ya kazi kwa wakunga ni dhalili

Kama Mona, wakunga wengi wanakabiliwa na mazingira magumu ya kazi, malipo duni na ukosefu wa maendeleo ya kazi – yote haya yakisababisha upungufu wa kimataifa. Ilhali utafiti wa UNFPA unaonyesha kuwa kuongeza idadi ya wakunga kwa asilimia 25 kunaweza kuokoa zaidi ya maisha milioni 2 kila mwaka ifikapo 2035.

Leo, Mona anakaribia kustaafu, lakini anasema amehisi faraja kulikabidhi kwa mwingine, jukumu la kituo chake cha afya. “Ni timu ya wakunga walio na maarifa ya hali ya juu sana, wataalamu, walio na uwezo wa kuongoza mustakabali wa huduma za afya ya uzazi.”

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!