WHO, mashirika 11 yaungana kuboresha huduma za afya

WHO, mashirika 11 yaungana kuboresha huduma za afya

Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania Dk Charles Moses katikati  akisaini makubaliano ya kushirikiana na Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Amref Health Afrika -Tanzania Dk Florance Temu, anayeshuhudia kulia ni Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Rachel Changonja.

By Baraka Loshilaa & Mintanga Hunda

Muktasari:

Waingia makubaliano kuimarisha mfumo wa huduma za afya, utoaji wa elimu, na kusaidia utafiti na ubunifu

Dar es Salaam. Katika kuboresha huduma za afya nchini, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeingia makubaliano na mashirika 11 yasiyo ya kiserikali kutekeleza mambo manne, ikiwamo kudhibiti na kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Maeneo mengine ni kuimarisha mfumo wa huduma za afya, utoaji wa elimu ya afya, na kusaidia utafiti na ubunifu.

Baadhi ya taasisi zilizoingia makubaliano na WHO ni Shirika la Afya Amref, Taasisi ya Afya Ifakara, Shirika la Sikika, Tanzania Health Summit, Chuo Kikuu cha Mzumbe, na Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE).

Makubaliano na mashirika hayo yamesainiwa na Mwakilishi Mkazi wa WHO Tanzania, Dk Charles Moses leo Mei 8, 2024 jijini Dar es Salaam.

Dk Moses ameainisha maeneo yatakayoguswa kupitia ushirikiano huo katika udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza ni utoaji wa chanjo kwa wananchi, uchunguzi wa magonjwa, kushughulikia magonjwa ya mlipuko na kuhamasisha mfumo bora wa maisha.

“Eneo lingine ni uimarishaji wa utoaji huduma za afya; tutashirikiana na taasisi zisizo za kiserikali kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya, kuimarisha nguvu kazi na kuhimiza matumizi ya teknolojia kwenye utoaji wa huduma,” amesema.

Dk Moses ametaja eneo lingine la ushirikiano kuwa ni utoaji wa elimu kwa watu kuhusu suala la afya hasa kuzingatia lishe bora, usafi wa mazingira na masuala ya uzazi.

Eneo la ubunifu amesema limepewa kipaumbele, mashirika hayo yakitarajiwa kuja na suluhu ya matatizo kwenye sekta ya afya yanayowakumba wananchi.

Dk Moses amesema watalenga kuwezesha kufanyika kwa utafiti, kubadilishana ujuzi na njia za kukabiliana na maradhi, na kuchochea matumizi ya takwimu katika utoaji wa maamuzi.

“Makubaliano haya ambayo utekelezaji wake ni mwaka 2024-2025 utatusaidia sote kwa pamoja kutengeneza jamii yenye afya bora kwa watu wa Tanzania, kuhakikisha bima ya afya kwa wote inafikiwa kama ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia –SDG,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Rachel Chagonja amesema makubaliano hayo yatasaidia kuimarisha sekta ya afya na kusaidia afya ya wananchi.

“Tunaishuruku WHO kwa kutambua mchango wetu kwenye sekta ya afya, hasa namna tunavyotoa huduma maeneo ambayo rasilimali za Serikali hazitoshi,” amesema.

Amesema makubaliano hayo yataenda kuwaongezea ufanisi wa kutoa huduma katika maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa na kuchochea chachu ya mijadala na mabadiliko ya sera kwenye sekta ya afya.

Menaja wa Maabara ya Taifa, Dk Ambele Mwafulango kwa niaba ya Wizara ya Afya amesema makubaliano hayo yataenda kupunguza changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya.

Amesema hayo yanatokana na maeneo ambayo Wizara ya Afya imeyaainisha, hivyo wadau hao wataenda kuyafanyia kazi hususani upatikanaji wa watumishi wa afya, na bima ya afya kwa wote.

“Tunatarajia wadau hawa watatusaidia elimu ya bima ya afya kwa wote itatolewa na upatikanaji wa bima yenyewe kwa watu wote inapatikana, suala lingine ni huduma bora za afya,” amesema.

Dk Mwafulango ametaja eneo lingine ni suala la magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yapo, Serikali imeyawekea mpango wa kuyagundua haraka na kutibiwa mapema.

Via:Mwananchi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!