Kutokupata choo au Kupata Choo Kigumu sana chanzo chake
Kutokupata choo au kuhisi kwenda kujisaidia haja kubwa na kutofanikiwa kutoa choo au mtu kupata choo chini ya mara tatu kwa wiki hujulikana kitaalamu kama constipation.Mtu mwenye tatizo hili la kufunga choo hupata choo kigumu,kikavu na chenye kupita kwa taabu kwenye njia ya haja kubwa.
Tafiti nyingi zinaonyesha kwamba angalau kila mtu katika maisha yake huwa anapata tatizo hili la kufunga choo. Kufunga choo ni tatizo ambalo watu wengi bado huhisi ni jambo la aibu sana hata kulizungumzia na hubaki na tatizo kwa muda mrefu mpaka pale wanapopata madhara ya kiafya ndio hutafuta msaada wa kitabibu.
Dalili zifuatazo zinaweza kutumika kuelezea tatizo la choo kufunga;
- Kupata choo kigumu na kinachoambatana na maumivu makali wakati wa kwenda haja kubwa
- Kutokupata choo kwa muda mrefu (infrequent bowel movements)
- Mtu kuhisi kama hajamaliza haja kubwa licha ya kupata choo
Tafiti nyingi zilizowahi kufayika zinaonyesha kwamba takribani asilimia 16 (16%) ya watu wazima hupata tatizo hili la kufunga choo,waathirika wengi wakiwa ni watu wenye umri kati ya 60-110 (asilimia 35%).
Kwa nini wazee hupata tatizo hili la kufunga choo?
Sababu zifuatazo huchangia wazee kutokupata choo au kufunga choo;
- Hali ya uzee husababisha mmeng’enyo wa chakula kufanyika taratibu (slow metabolism)
- Ukosefu wa lishe bora
- Kutokunywa maji ya kutosha
- Kutofanya mazoezi
- Magonjwa ya uzee kama pelvic floor prolapse na utumiaji wa dawa aina ya antacids na dawa za kupunguza maumivu
- Pia uzee husababisha meno kung’oka hivyo wazee huchagua vyakula laini na vyenye ufumwele (fiber) kidogo
Wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu wanaopata tatizo hili la kufunga choo mara kwa mara.
Visababishi vya choo kufunga (constipation) ni kama ifuatavyo;
- Kutokula mlo wenye ufumwele (fiber) wa kutosha
- Kutokunywa maji ya kutosha
- Kutumia sana dawa za kulainisha choo
- Kutokufanya mazoezi au
- kuishi maisha ya unyongovu (stressful life)
- Madawa kama aspirin (NSAID), morphine, dawa za presha(thiazides, verapamil, furosemide), dawa za sonono (antidpressants), madawa ya saratani n.k
- Magonjwa ya mfumo wa mmengenyo wa chakula au vichocheo vya mwili (hormonal disorders) kama hypothyroidism
- Ujauzito- Mama mjamzito yupo kwenye hatari zaidi ya kupata choo kigumu au constipation hasa katika miezi ya mwisho ya ujauzaito wake kwa sababu ya kuongezeka kwa vichocheo mwili aina ya sex hormones, kupungua kwa mmeng’enyo kwenye tumbo na kuchelewa kwa tumbo kupitisha chakula (delayed interstinal emptying)
- Magonjwa ya tumbo kama colorectal dysfunction, diverticulitis, irritable bowel syndrome, saratani za matumbo hasa utumbo mkubwa
- Chronic Idiopathic constipation– Sababu zisizojulikana
Kama ambavyo tumejifunza sababu na makundi wa watu ambao wapo kwenye hatari zaidi. Tatizo hili linaweza kumpata mtu yoyote wa rika lolote hata watoto wachanga. Hivyo fuatilia makala zetu zijazo ili kujua uchunguzi,matibabu na jinsi ya kuepukana na tatizo hili la kufunga choo.Kama tayari una tatizo hili tafadhali fika kituo cha afya kilichokaribu nawe kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri wa kitaalamu.
Cr:Dr. Hamphrey
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!