Dk Ndugulile: Nimepewa miezi sita kujipanga WHO

 Dk Ndugulile: Nimepewa miezi sita kujipanga WHO

Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile wakati akitoa salamu za shukrani bungeni jijini Dodoma leo Jumanne, Septemba 3, 2024.

Dk Ndugulile amesema hayo leo Jumanne, Septemba 3, 2024 wakati akitoa salamu za shukurani bungeni jijini Dodoma, baada ya kukaribishwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu

Mteule wa nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndugulile amesema anatarajia kuanza kazi rasmi ifikapo Machi 2025, baada ya kupewa miezi sita kujipanga.

Dk Ndugulile amesema hayo leo Jumanne, Septemba 3, 2024 wakati akitoa salamu za shukurani bungeni jijini Dodoma, baada ya kukaribishwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu.

“Niwaombe mniombee, tuendeleze sala na dua nyingi kwani nafasi hii imebeba maono ya Watanzania na Waafrika wanatarajia makubwa, kikubwa niishukuru Serikali nzima na wabunge kwa kuniunga mkono, nitakuwepo katika kipindi cha mpito napokea maoni na ushauri kutoka kwenu,” amesema Dk Ndugulile.

Dk Ndugulile anakuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo wa kwanza Afrika Mashariki kushika nafasi hiyo.

Amesema amepewa kipindi cha miaka mitano kuonyesha utendaji wake na iwapo atafanikiwa kufanya vizuri, anaweza kuchaguliwa tena kwa miaka mitano jumla akaitumikia nafasi hiyo kwa miaka 10.

“Kituo changu cha kazi kitakuwa Congo Brazzaville, utaratibu ulivyo unapewa miezi sita ya kujipanga hivyo natarajia kuanza kazi mwishoni mwa Februari au Machi 2025,” amesema.

 “Wale waliokuwa wanahoji Jimbo la Kigamboni lipo wazi jibu ni hapana! Bado niponipo na wananchi wangu wote waliniunga mkono na walikuwa na dua zao pia.”

Akizungumzia namna alivyojinadi wakati wa kugombea amesema miongoni mwa mambo aliyogusia ni pamoja na namna Afrika inavyohitaji kuwa na uongozi imara na wenye maono kuhakikisha bara linaweza kufanikiwa, inahitaji mtu mwenye uwezo wa masuala ya kitaaluma, uongozi na sifa zingine.

Amesema katika nafasi hiyo alishindana na watu wabobevu, lakini anashukuru mawaziri wa afya waliona aina gani ya uongozi wanaouhitaji Afrika kwa sasa, hivyo walimchagua.

Amesema WHO ina malengo mahususi: “Tunataka kuhakikisha huduma za afya zinapatikana barani Afrika, lakini kuona tunajindaa vizuri na kuimarisha taasisi mbalimbali zinazofanyika katika bara letu; katika uongozi wangu tunakwenda kuboresha WHO kuhakikkisha inakuwa imara.”

Awali akitoa salamu zake, Dk Ndugulile amewashukuru wabunge, spika na naibu spika na katibu wa Bunge kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati wote wa kampeni zake wa uchaguzi huo.

“Nitoe shukrani zangu kwa katibu na watumishi wa Bunge, walinipa ushirikiano mkubwa ilibidi wakati mwingine nisishiriki baadhi ya vikao vya Bunge.

“Mawaziri nilipata meseji nyingi kabla na baada ya uchaguzi nilienda na mawaziri wawili akiwamo Waziri wa Afya ambaye alikuwa na wiki tatu tu naomba nimpongeze Waziri wa Afya Jenista Mhagama, mawaziri wote, naibu mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na wananchi wa Kigamboni kwa kunibeba mbunge wao kwa miaka 15 sasa,” amesema Dk Ndugulile.

Aidha, amewapongeza wabunge, January Makamba (Bumbuli) na Ummy Mwalimu wa Tanga Mjini walioshiriki kwenye harakati za awali za kampeni wakiwa mawaziri.

Makamba alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ummy wa Waziri wa Afya ambao waliwekwa kando kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, Julai 21, 2024.

Via Mwananchi.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!