Ugonjwa wa Duchenne,Ugonjwa unaodhoofisha misuli
Mtoto 1 wa kiume kati ya watoto 5000 duniani anaugua ugonjwa wa Duchenne
Kwa viwango vya sasa vya huduma, watu wenye Duchenne wanaweza kuishi hadi umri wa miaka 30.
Kwa sasa ugonjwa huu hauna tiba.
Kwa mara ya kwanza hii leo dunia inaadhimisha siku ya kimataifa ya kuhamasisha uelewa kuhusu ugonjwa utokanao na misuli kuzorota na kudhoofika au kwa lugha ya kiingereza, Duchenne Muscular Dystrophy (DMD).
Umoja wa Mataifa unasema maudhui ya mwaka huu yanasisitiza umuhimu wa kupaza sauti za wachechemuzi wa haki za wagonjwa, ujumuishaji na ustawi wa watu wanaoishi na ugonjwa huo na mengine yanayohusiana na ukosefu wa protini hiyo.
Umoja wa Mataifa kupitia wavuti mahsusi wa siku hii, unasema wagonjwa wenye tatizo hili, misuli yao huzorota na kudhoofika taratibu kutokana na kukosa protini ya kulinda misuli.
Chanzo cha misuli kudhoofika
Hali hiyo inasababishwa na tatizo kwenye jeni inayotengeneza daistofini ambayo ni protini muhimu ya kuimarisha misuli tangu mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake.
Misuli inaanza kudhoofika taratibu hadi pale inapoathiri mwili mzima. “Inasababishwa na kubadilika kwa kromosomu X, na ndio maana wanaume ndio wengi wanaoathirika na ugonhwa huu,” limesema chapisho kwenye wavuti wa Umoja wa Mataifa.
Kromosomu X ni moja ya kromosomu zinazotumika kubaini jinsia ya kiumbe. Wanyama wakiwemo binadamu wana kromosomu X na Y ambapo muunganiko wake ndio hubaini jinsia ya kike au kiume.
Athari za ugonjwa wa kudhoofika na kuzorota kwa mifupa
Kwanza ni maumivu wakati wa kutembea, kisha mienendo yote ya neva na misuli mwilini inaathiriwa na hatimaye mgonjwa anapata shida kupumua. Moyo nao unashindwa kufanya kazi vizuri kwa kuwa nao una misuli.
Protini inayokosekana nayo ina jukumu muhimu kwenye ubongo, hivyo mwenendo wa mtu kujifunza unaweza kuonesha kiashiria cha ugonjwa huu wa DMD.
Dalili za ugonjwa wa misuli kuzorota na kudhoofu
Katika nchi nyingi, wastani wa umri wa kutambua ugonjwa huu kwa mtu ni kuanzia miaka 4 na kuendelea.
Wazazi wakati mwingine wanaona dalili mapema na baadhi ya dalili tayari zinakuwa dhahiri hata mtoot anapokuwa bado ni mdogo zaidi.
Dalili za awali ni pamoja na mtu kupata taabu kusimama au kutembea. Wengine wanapata shida kupanda ngazi na wakitembea wanayumba. Katika hali nyingine sehemu ya msuli chini ya goti inatanuka na kuwa kubwa kwa sababu tishu za msuli zimegeuka kuwa mafuta.
Kwa watoto wenye Duchenne, wengi wao wanachukua muda kuweza kutembea, kurukaruka au kutambaa. Baadhi yao, dalili za awali ni kuchelewa kuanza kuzungumza. Pindi kutembea inapokuwa ni vigumu zaidi, watoto hao huanza kutembelea kwa kutumia vidole.
Jina la ugonjwa huu linatokana na Duchenne de Boulogne, ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kuripoti kuhusu ugonjwa huu kw akina miaka ya 1860.
Baraza la Kuu la Umoja wa Mataifa, tarehe 30 mwezi Novemba mwaka 2023 lilipitisha azimio namba RES/78/12 la kutambua tarehe 7 Septemba kuwa siku ya kuhamasisha kuhusu ugonjwa wa Duchenne.
Je wajua?
Mtoto 1 wa kiume kati ya watoto 5000 duniani anaugua ugonjwa wa Duchenne
Kwa viwango vya sasa vya huduma, watu wenye Duchenne wanaweza kuishi hadi umri wa miaka 30.
Kwa sasa ugonjwa huu hauna tiba.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!