Uzalishaji wa chanjo ya Mpox barani Afrika wajadiliwa

Uzalishaji wa chanjo ya Mpox barani Afrika wajadiliwa

Kampuni ya dawa ya Afrika, Aspen Pharmacare, inafanya mazungumzo na washirika wake kuhusu uzalishaji wa chanjo za Mpox katika viwanda vyake, alisema Mkurugenzi Mtendaji Stephen Saad alipoongea na Reuters Jumanne.

Bara la Afrika lipo chini ya shinikizo la kudhibiti mlipuko wa maambukizi hayo hatari, ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa dharura ya afya ya umma duniani mnamo katikati ya Agosti, baada ya aina mpya ya virusi kuanza kusambaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda nchi jirani.

Nchi kumi na tatu za Afrika zimeripoti zaidi ya kesi 22,800 za Mpox na vifo 622 mwaka huu, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) mwezi uliopita.

“Tunaongea na watu,” alisema Saad bila kutaja kampuni zinazohusika, akiongeza kuwa Aspen ina uwezo wa kuzalisha chanjo hizo na wanahisi wako tayari kufanya uzalishaji huo.

Hata hivyo, Aspen imetoa masharti mawili ili kuepuka hali ya kukosa kazi kama ilivyotokea wakati walipotengeneza chanjo za COVID-19 ambazo hazikuhitajika kwa kiasi kikubwa. Kwanza, kampuni inataka ahadi ya kiasi cha maagizo yatakayofanywa, na pili, inahitaji kufidiwa gharama za kuhamisha teknolojia ya uzalishaji wa chanjo hizo kwenye kiwanda chao.

Mpox, ambayo inaweza kusambaa kupitia mawasiliano ya karibu, kwa kawaida huwa si hatari sana lakini inaweza kusababisha vifo kwa nadra. Inasababisha dalili kama za mafua na majipu yenye usaha mwilini.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!