Sababu za mtoto kuchelewa kuota meno
Watoto wanapozaliwa, tayari wanakuwa na meno ambayo yamefunikiwa kwa fizi. Meno huanza kutoka kwa mara ya kwanza mtoto akiwa na umri wa miezi sita ( 6) japo umri huu unaweza tofautiana kutoka kwa mtoto mmoja hadi mwingine.
Meno mawili ya kwanza yanayoonekana mara nyingi ni yale ya kinywa cha chini katikati yakifuatiwa na ya kinywa cha juu katikati. Watoto wengi hufikisha meno yote 20 ya kwanza wakiwa na umri wa miaka 3.
Baadhi ya watoto hawaoti meno kama watoto wengine, yao huchelewa au kutokuota kabisa. Hii husababishwa na vitu mbalimbali. Kama mtoto wako hajaota jino hata moja hadi umri wa miezi 18 basi ni muhimu umpeleke hospitali aonane na daktari wa kinywa na meno kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Sababu za meno kuchelewa kuota
Zipo sababu nyingi za meno kuchelewa kuota. Wakati mwingine tatizo la meno kuchelewa kuota huwa ni tatizo la kwenye familia hivyo linaweza kurithishwa kwa vizazi vinavyokuja. Mzazi pia ujiulize kama meno yako yalichelewa kuota, kama ni ndio basi tambua kwamba hata ya mwanao yataota tu japo kwa kuchelewa.
Sababu zinazochangia meno kuchelewa kuota kwa mtoto ni kama zifuatazo;
– Utapia mlo na upungufu wa madini na vitamini mwilini,
Watoto wenye utapia mlo meno huchelewa kuota kwa sababu ya kukosa virutubisho muhimu vya ukuaji wa meno. Aidha madini ya calcium na vitamini D ni muhimu sana katika ukuaji wa meno. Hivyo mtoto akipungukiwa na virutubisho hivi meno huchelewa kuota.
– Ugonjwa wa jeni unaofahamika kama Down Syndrome,
Huu ni miongoni mwa mgonjwa wa kuzaliwa nayo (congenital).Ugonjwa huu unatokana na hitilafu kwenye kinasaba cha 21 (chromosome 21). Ugonjwa huu huambatana na tatizo la meno kuchelewa kuota.
– Magojwa yatokanayo na hitalifu kwenye chromosomes (chromosome anomalies)
– Mtoto kuzaliwa njiti-Kuzaliwa njiti au na kuzaliwa na uzito mdogo kupita kawaida (chini ya 1.5kg) kunahusishwa na kuchelewa kuota kwa meno kwa mtoto. Watoto hawa wanaweza kuwa na matatizo ya meno yenyewe.
– Magonjwa kama Amelogenesis na Regional Odontodysplasia
Amelogenesis ni ugonjwa wa kuzaliwa nao (congenital disease) ambapo mtoto anazaliwa na hitilafu kwenye kwenye protini zinazotengeneza enameli (nyeupe ngumu ya jino) hii hupelekea kuwa na enameli isiyo ya kawaida na meno yanakuwa ya njano. Hii huambatana na meno kuchelewa kuota.
Regional odondodysplasia ni hitilafu katika ukuaji inayohusisha mesodermal na ectoderm (hizi ndizo zinazotengeneza jino la ndani na nje) za meno. Ugonjwa huu huwa unaathiri sehemu moja tu ya kinywa (localized). Huu sio ugonjwa wa kurithi.
Kwanini uwe na wasiwasi kuhusu meno ya mtoto yanapochelewa kuota?
Watoto ambao hawajaota meno hadi umri wa miezi 18 wapelekwe kumuona daktari wa meno. Watoto wengi huwa na meno manne wakifikia umri wa miezi 12 na huwa na yote 20 wakiwa na miezi 27.
Kama meno ya mtoto wako hayajaota kwa wakati inaweza kuwa ni ishara ya ugonjwa au upungufu wa madini au vitamini fulani mwilini.
Je, meno kuchelewa kutoa ni dalili mbaya?
Meno kuchelewa kuota sio jambo kubwa sana ila linaweza kuongeza uwezekano wa mtoto kupata matatizo ya meno ukubwani. Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa watoto waliopata tatizo la meno kuchelewa kuota wana nafasi kubwa ya kuhitaji matibabu ya meno wakiwa na umri wa miaka 30.
Meno kuota kwa wakati kwa mtoto humsaidia kutafuna vizuri na husaidia meno ya pili kujipanga vizuri kwenye kinywa.
Meno yakichelewa kuota husababisha mtoto kukosa au kupata virutubisho vichache maana atakuwa hawezi kutafuna vizuri hivyo kupata shida ya kumeng’enya chakula.
Jinsi ya kutunza meno mapya ya mtoto wako
✓ Epuka vyakula na vinywaji vyenye sukari
✓ Safisha fizi kwa kutumia kutambaa kisafi mara mbili kwa siku
✓ Epuka kumlaza mtoto na chupa ya maziwa kitandani
✓ Kumbuka kuswaki na kusafisha meno yaliyoota
✓ Utaanza kutumia dawa ya meno pindi mtoto akifikisha miaka 2.
By Dr Hamphrey