Upatikanaji wa maji safi na salama kupunguza magonjwa ya mlipuko
Na WAF – Simiyu
Wizara ya Afya, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU), kwa pamoja kupitia mradi wa kupambana na Magonjwa ya Mlipuko wamewezesha vijiji vya Nyanguge na Bunamhala Wilayani Bariadi, Mkoani Simiyu, kufikiwa na huduma ya maji safi na salama.
Kupitia mradi huo Visima vimekarabatiwa na kuwekwa pampu za umeme na kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama mabadiliko ambayo yameleta furaha kwa wananchi kwa kuchochea ustawi wa afya na kupunguza hatari ya magonjwa ya mlipuko.
Mwenyekiti wa kamati ya maji katika Wilaya ya Bariadi, Swales Ngusa, amesema kuboreshwa kwa ubora wa maji kumechochewa na gharama za uendeshaji kupungua kufuatia upatikanaji wa umeme.
Kwa upande wake, Afisa Afya na Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoani Simiyu, Bashiri Salum, amethibitisha kuwa matumizi ya dawa ya Klorini yamekuwa muhimu katika kuhakikisha maji yanakuwa safi na salama.
Mradi huo unaotekelezwa katika wilaya kadhaa za Mkoa wa Simiyu unalenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme vijijini na kuwezesha huduma za maji safi na salama, huku ikilenga kuboresha afya na ustawi wa jamii awali wananchi walikabiliwa na changamoto za kuchota maji katika vyanzo visivyokuwa salama, hali iliyosababisha kuongezeka kwa magonjwa ya mlipuko kama vile Kipindupindu.