Baada ya Homa ya Nyani ama mpox kutangazwa kuwa dharura ya afya ya umma na Shirika la Afya Duniani kutokana na kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo, macho yote yameelekezwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambayo inakadiria karibu maambukizi yote yalizorekodiwa mwaka huu na zaidi ya vifo 450.
Ilipotembelea vituo vya matibabu mashariki mwa nchi hiyo, BBC imegundua watoto wameathiriwa zaidi na ugonjwa huo, ambao unaweza kusababisha kifo.
“Ilianza kama kipele kidogo mwilini. Mamake alipokitumbua kilitoa kitu kama maji maji hivi. Mara kipele kingine kikatokea, na baada ya muda mfupi vipele hivyo vikamjaa mwili mzima,” anasema Alain Matabaro, anaelezea jinsi mwanawe wa kiume Amani, mwenye umri wa miaka sita alivyopatwa na homa ya nyani.
Alainza kupona baada ya kutibiwa kwa siku nne katika kliniki moja huko Munigi, karibu na mji wa Goma mashariki mwa Congo.
Asilimia 75 ya wanaopewa huduma ya matibabu ni watoto walio na chini ya umri wa miaka 10, kulingana na Dk Pierre-Olivier Ngadjole anayefanya kazi na shirika lisilo la kiserekali linalotoa matibabu la Medair.
Watoto wanaonekana kuathiriwa sana na mlipuko wa mpox kwa sababu ya mfumo wao mdogo wa kinga.
Dkt Ngadjole pia anasema msongamano wa watu katika kambi ya wakimbizi wa ndani iliyowekwa kwa ajili ya kuwahifadhi wato waliotoroka makwao kutokana na migogoro katika eneo hilo imechangia kuenea kwa maambukizi. Njia moja ya kueneza virusi vya mpox ni kupitia mawasiliano ya karibu na watoto “wanacheza pamoja kila mara. Hawajali sana suala la kutokaribiana,” anaambia BBC.
“Hata nyumbani wanalala kitanda kimoja. Utapata watoto watatu, wanne, watano. Kwa hiyo maambukizi yanaongezeka kila siku.”
Tangu Juni, zahanati ya Munigi, ambayo inatoa matibabu ya bure ikiwa ni pamoja na antibiotiki kutibu maradhi ya ngozi, paracetamol na maji safi ya kunywa, imeshughulikia wagonjwa 310 wa mpox. Sasa inawahudumiwa kati ya wagonjwa watano na kumi wapya kila siku.
Hakuna mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa huo na Dk Ngadjole anaamini ni kwa sababu watu wanatafuta msaada wa matibabu mapema .
“Nadhani ni muhimu sana kutoa huduma za afya bila malipo hasa katika muktadha huu … [Inamaanisha] watu hawakabiliwi na kizuizi chochote cha kifedha, wanakuja mapema kwenye kituo cha afya.”
Je, tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu Homa ya Nyani?
Homa ya Nyani: Mlipuko wa Mpox Afrika watangazwa kuwa dharura ya kiafya – nini kitakachofuata?
Homa ya Nyani: Je, kuna chanjo ya mpox?
Hali ni tofauti kilomita 80 kusini-magharibi mwa Munigi, upande wa pili wa Ziwa Kivu, katika hospitali ya Kavumu.
Wagonjwa 800 wamefika katika kituo cha matibabu tangu Juni na wanane wamekufa – wote wakiwa chini ya umri wa miaka mitano.
Ansima Kanigo mwenye umri wa miaka miwili aliambukizwa mpox na mmoja wa ndugu zake wanne, ambao wote wameugua ugonjwa huo.
Mamake, Nzigire Kanigo, 35, mwanzoni hakujua ilikuwa ni nini.
“Hii ndiyo mara yangu ya kwanza kuiona, mtoto wangu alipoumwa wazazi wengine waliniambia huenda ni surua, lakini tulianza kutibu surua tukashindwa, ndipo tukaamua kuja huku.
“Mungu ambariki daktari ambaye ameleta dawa… [watoto] watatu wamepona – wako nyumbani. Nimelazwa na watoto wawili tu katika hospitali hii. Namshukuru Mungu.”
Mkurugenzi wa matibabu katika hospitali hiyo, Dkt Robert Musole, anasema mkurupuko huo haufai kupuuzwa na mamlaka.
“Hali ni mbaya sana, na tumezidiwa sana, kwa sababu tuna uwezo mdogo, lakini tunauhitaji mkubwa.
“Changamoto ya kwanza tunayokabiliana nayo katika mwitikio huu ni malazi ya wagonjwa. Changamoto ya pili ni upatikanaji wa dawa ambazo hatuna.”
Kote mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, kuna kambi kadhaa za mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao huku makundi mbalimbali ya waasi yakiendesha harakati zao katika eneo hilo.
Watu mara nyingi husongamana katika miundo ya kubahatisha na kuishi katika hali duni bila usafi wa mazingira – mahali pazuri pa kueneza mpox.
Wahudumu wa afya wamekuwa wakitembelea maeneo kama kambi ya Mudja karibu na Mlima Nyiragongo, ili kuwahamasisha watu nini cha kufanya wanapoona dalili, kama vile kujiepusha na maeneo yenye msongamano.
“Ugonjwa huu umetuletea hofu kubwa tunahofia sote tutaugua,” anasema Josephine Sirangunza, ambaye anaishi katika kambi hiyo na watoto wake watano.
Anasema serikali inahitaji kutoa baadhi ya vifaa vya msingi kusaidia kukomesha kuenea kwa ugonjwa huo.
“Tunapoona mtu akiugua, tunahangaikia jinsi ya kujilinda.”
Ni maoni ya Bosco Sebuke, 52, ambaye ana watoto 10.
“Tumehamasishwa [kuhusu mpox], lakini tuna hofu kwa sababu tumesongamana katika makazi yetu. Tunalala katika mazingira duni sana, tunalala pamoja kitandani, hivyo kinga ni ngumu na kwa sababu hiyo, tunaogopa,” anasema.
Mlipuko huo mashariki mwa DR Congo ni wa aina mpya ya mpox uitwao Clade 1b na sasa umeenea katika nchi jirani.
Wiki iliyopita, serikali ya Congo ilisema inatumai kuwa chanjo zitaanza kuwasili kutoka Marekani na Japan hivi karibuni. Hadi wakati huo, nchi hiyo haina chanjo yoyote licha ya kuwa kitovu cha virusi hivyo.
Bw Matabaro, babake Amani ambaye sasa anapata nafuu kutokana na homa ya nyani, anasema ana matumaini na habari kuwa chanjo inaweza kuwa njiani.
Lakini usambazaji utakuwa mdogo sana na, kama Dk Ngadjole anasema, chanjo ni kipengele kimoja tu cha kupunguza kuenea kwa virusi.
“Hatua [rahisi] zaidi ya kudhibiti maambukizi ni kuboresha usafi. Tunapoboresha usafi nyumbani, tunapoboresha usafi katika ngazi ya jamii, ni rahisi sana kupunguza hatari ya maambukizi.”
Bi Sirangunza anarejelea kauli ya daktari: “Waambie viongozi wetu watutumie dawa, sabuni, na hatua zingine za kujikinga ili tusiambukizwe.”
Maelezo zaidi:BBC