Ugonjwa wa kisukari husababishwa na nini,Chanzo,Aina,Dalili pamoja na Tiba
Ugonjwa wa kisukari ni ugonjwa ambao huhusisha kuwepo kwa kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko kawaida au kuwa na kiwango kidogo sana cha sukari kwenye damu kuliko kawaida.
Hivo hapa tunapata aina mbili za kisukari;
(i) Kisukari cha kupanda au kwa kitaalam tunaita Hyperglycemia
(ii) Na kisukari cha kushuka au kwa kitaalam tunaita Hypoglycemia
Katika Makala hii tutazungumzia zaidi kuhusu kisukari cha kupanda,hivo kila tutakapozungumzia Ugonjwa wa Kisukari kwenye Makala hii tunazungumzia Sukari ya kupanda.
Ugonjwa wa Kisukari
Ugonjwa wa kisukari- huu ni ugonjwa ambao hutokea wakati sukari yako kwenye damu (glucose) iko juu sana. Na mara nyingi hutokea wakati;
- kongosho lako likishindwa kutengeneza insulini ya kutosha
- au Kongosho kutokutengeneza Insulini kabisa,
- au hutokea wakati mwili wako haujibu matokeo ya utendaji kazi wa Insulini ipasavyo.
Ugonjwa wa kisukari huathiri watu wa umri wowote. Aina nyingi za ugonjwa wa kisukari ni sugu, na aina zote zinaweza kudhibitiwa kwa dawa pamoja na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Fahamu Kwa Asilimia kubwa Glukosi (sukari) hasa hutoka kwenye wanga au carbohydrates katika vyakula unavyokula na vinywaji unavyokunywa. Ni chanzo cha nishati kwa mwili wako. Damu yako hubeba glukosi hadi kwenye seli zote za mwili wako ili kutumia kwa ajili ya nishati.
Glucose inapokuwa kwenye mfumo wako wa damu, inahitaji usaidizi "au ufunguo" - ili kufikia lengo la mwisho. Ufunguo huu ni insulini (homoni). Ikiwa kongosho yako haitengenezi insulini ya kutosha au mwili wako hauitumii ipasavyo, glukosi hujilimbikiza kwenye damu yako, na kusababisha sukari kuwa juu kwenye damu (hyperglycemia).
Baada ya Muda, kuwa na kiwango cha juu cha Sukari kwenye damu mfululizo kunaweza kusababisha shida za kiafya, kama vile ugonjwa wa moyo, uharibifu wa neva na shida za macho.
Aina za Ugonjwa wa Kisukari
Kuna aina kadhaa za Ugonjwa wa kisukari. Tunapozungumzia Sukari ya kupanda kuna aina kadhaa ikiwemo:
- Kisukari aina ya kwanza(Type 1 diabetes)
- Kisukari aina ya Pili(Type 2 diabetes)
- Kisukari cha Mimba(Gestational diabetes)
- Pamoja na aina Zingine kadhaa ambazo watu wengi hawazizungumzii kabsa ila zipo,mfano; Tuna; Type 3 diabetes,Latent autoimmune diabetes in adults (LADA),Maturity-onset diabetes,Neonatal diabetes n.k
1. Kisukari aina ya Kwanza(Type 1 diabetes)
Aina hii ya Ugonjwa huhusisha kongosho au Pancrease kutokuzalisha na kutoa Insulin kabisa.
Hapa kongosho haitengenezi Insulini kabsa, kwa sababu mfumo wa kinga ya mwili hushambulia seli za kongosho zinazotengeneza insulini.
Aina hii ya 1 ya kisukari kwa Kawaida hugunduliwa kwa watoto na vijana, lakini inaweza kutokea katika umri wowote pia.
2. Kisukari Aina ya Pili(Type 2 diabetes)
Kwa aina hii, mwili wako hautengenezi insulini ya kutosha au seli za mwili wako hazitumii vizuri ipasavyo insulini iliyopo. Hii ndiyo aina ya Ugonjwa wa kisukari ambao huwapata Watu Wengi Zaidi. Na Inaathiri zaidi watu wazima, lakini watoto wanaweza kuwa nayo pia.
Katika aina ya 2 ya kisukari, kongosho hutengeneza insulini kidogo kuliko ilivyokuwa hapo awali, na mwili wako unatengeneza ukinzani dhidi ya insulini ndogo iliyopo.
3. Kisukari cha Mimba(Gestational diabetes):
Aina hii ya kisukari inatokea wakati wa ujauzito, na kawaida hupotea baada ya ujauzito au baada ya kujifungua. Ingawa baadhi ya tafiti zinaonyesha ikiwa una kisukari wakati wa ujauzito, uko katika hatari kubwa ya kupata kisukari cha Aina ya 2 baadaye maishani.
Dalili Za Ugonjwa wa kisukari
Ukali wa dalili unaweza kutofautiana kulingana na aina ya ugonjwa wa kisukari uliyo nao. Dalili hizi kawaida huwa kali zaidi katika aina ya 1 ya kisukari kuliko kisukari cha Aina ya 2.
Dalili za kisukari kwa Ujumla ni zipi?
Dalili za ugonjwa wa kisukari ni pamoja na:
- Kuongezeka kwa kiu na kinywa kuwa kikavu zaidi.
- Kukojoa mara kwa mara.
- Kupata sana Uchovu wa mwili
- Macho kutokuona vizuri au kuona marue rue
- Kupunguza Uzito kwa kasi bila Sababu inayoeleweka,
- Mtu kukonda
- Kupata Ganzi au hali ya kuchoma choma katika mikono au miguu yako.
- Vidonda kuponya polepole au kuchelewa zaidi kupona
- Kuwa kwenye hatari ya kupata Maambukizi ya mara kwa mara ya ngozi, Maambukizi ya Fangasi ukeni n.k
Ni muhimu kuzungumza na mtoa huduma wako wa afya ikiwa wewe au mtoto wako ana dalili hizi.
Ugonjwa wa Kisukari husababishwa na nini?
Uwepo wa Glucose nyingi inayozunguka katika mfumo wako wa damu husababisha ugonjwa wa kisukari, bila kujali aina. Ingawa, sababu kwa nini viwango vya sukari kwenye damu yako ni vikubwa hutofautiana kulingana na aina ya ugonjwa wa kisukari.
Hizi hapa ni Sababu mbali mbali zinazochangia hali hiyo:
- Tatizo la Insulin resistance:
Aina ya 2 ya kisukari hutokana hasa na ukinzani wa insulini. Ukinzani huu wa insulini hutokea wakati seli kwenye misuli, mafuta na ini hazitoi matokeo inavyopaswa dhidi ya insulini.
Sababu na hali kadhaa huchangia viwango tofauti vya ukinzani wa insulini, Sababu hizo ni pamoja na;
- Uzito mkubwa au kunenepa kupita kiasi,
- Kutokufanya Mazoezi ya mwili
- Mabadiliko ya Vichocheo au homoni mwilini
- Swala la kimaumbile au Genetics factor
- Matumizi ya baadhi ya dawa fulani.n.k
- Tatizo kwenye Mfumo wa kinga mwili(Autoimmune disease):
Kisukari aina ya kwanza(Type 1 diabetes) pamoja na Latent autoimmune diabetes in adults (LADA) ambapo nilitaja aina hii hapo awali, hutokea wakati mfumo wako wa kinga unaposhambulia seli zinazozalisha insulini kwenye kongosho lako.
- Tatizo la Hormonal imbalances:
Wakati wa Ujauzito, placenta huweza kutoa homoni zinazosababisha ukinzani wa insulini. Unaweza kupata kisukari wakati wa ujauzito ikiwa kongosho yako haiwezi kutoa insulini ya kutosha kushinda ukinzani wa insulini uliojitokeza. Hali nyingine zinazohusiana na homoni kama vile tatizo la akromegali pia zinaweza kusababisha kisukari cha Aina ya 2.
- Uharibifu wa kongosho(Pancreatic damage):
Uharibifu wa kongosho lako - kutokana na hali kama vile ajali, upasuaji au jeraha - unaweza kuathiri uwezo wake wa kutengeneza insulini, na kusababisha ugonjwa wa kisukari hasa Aina ya 3 ya kisukari(Type 3 diabetes).
- Matatizo ya kimaumbile au kigenetic(Genetic mutations):
Mabadiliko fulani ya kijenetic yanaweza kusababisha Ugonjwa wa kisukari hasa kuanzia kwa watoto wachanga,aina hii ya kisukari hufahamika kama neonatal diabetes.
- Utumiaji wa muda mrefu wa baadhi ya dawa:
Unachotakiwa kufahamu matumizi pia ya baadhi ya dawa kwa muda mrefu sana yanaweza kusababisha ugonjwa wa kisukari hasa Aina ya 2, Dawa hizo ni pamoja na dawa jamii ya corticosteroids..n.k.
Madhara ya Ugonjwa wa Kisukari
Yapo madhara mbali mbali ambayo unaweza kuyapata hasa ikiwa Ugonjwa huu wa kisukari umekuwa wa muda mrefu, Madhara hayo ni pamoja na;
- Kupata tatizo la Macho kutokuona
- Kupata Magonjwa au matatizo mbali mbali ya moyo kama vile;Coronary artery disease,Shambilio la moyo(Heart attack),kiharusi au Stroke.n.k.
- Kupata Uharibifu wa Neva,Nerve damage au neuropathy ambapo matokeo yake huleta dalili kama vile, kupata ganzi,kuhisi hali ya kuchoma choma mwilini,maumivu n.k
- Kukatwa viungo mbali mbali vya mwili kama vile Miguu,vidole n.k
KWA USHAURI ZAIDI,ELIMU AU TIBA TUWASILIANE KWA NAMBA +255758286584.