Ticker

6/recent/ticker-posts

Familia yajitenga mazishi ya Ally Dangote



Siku moja baada ya kutokea kifo cha Ally Ramadhani (19) maarufu kwa jina la Dangote, familia yake imejitenga na mazishi yake ikiiachia Serikali imalizie kazi hiyo.

Dangote aliuawa juzi jijini Arusha baada ya kujaribu kuwatoroka polisi alipokuwa amekamatwa.

Mamia ya wakazi wa jiji la Arusha walifurika katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Mkoa Mount Meru kushuhudia mwili wake, huku wengi wakionyesha kufurahia kifo chake wakitaja matukio ya kihalifu anayohusishwa nayo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Salvas Makweli amewaeleza waandishi wa habari jana kuwa Dangote alifariki baada ya kupigwa risasi na kupata jeraha la risasi wakati akiwatoroka polisi.

Kufuatia kifo hicho, babu yake anayejulikana kwa jina la Ally Kombo anayeishi eneo la Sokoni One jijini hapa, amesema hawajui taratibu za mazishi ila wanaiachia Serikali.

“Kama kumuaga nadhani taratibu zote zitafanyika hukohuko hospitali kwa sababu watu wengi wana hasira naye,” amesema.

Dangote aliyezaliwa mwaka 2004 mtaa wa Kaburimoja Unga Ltd jijini hapa, alipelekwa kulelewa kwa babu yake Kombo na bibi yake Khadija Kombo, baada ya kushindikana kulelewa na wazazi wake.

Kombo ameeleza kuwa Dangote alikuwa na tabia ya wizi tangu alipompokea na haikuwa rahisi kumdhibiti.

“Ni kweli huyu kijana alikuwa mhalifu hata mimi aliwahi kuniibia pesa. Tulipata taarifa amekamatwa kutokana na kusakwa na polisi na baadaye tulielezwa ameuawa,” anasema.

Kombo amesema sio kweli kuwa kijana huyo alikuwa anafanya uhalifu kwa kutumia ushirikina bali alijifunza kutokana na marafiki zake na hasa baada ya kukaa magereza muda mrefu.

“Alikuwa amekamtwa kwa uhalifu alikaa sana magereza ndio ametoka hivi karibuni na kuanza tena uhalifu wake,” amesema.

Hassan Abbas anayeishi eneo la Sokoni One jirani na kwa kina Dangote  amesema tabia za kijana huyo zilibadilika sana baada ya kutoka gerezani.

“Hata sisi tulikuwa tunamuogopa usiku hatutoki nje kwani alikuwa anachoma watu na bisibisi hadi kuwauwa,” amesema.

Amesema anajua Ally alikuwa anavuta bangi na kutumia dawa za kulevya huenda pia vilichangia awe mhalifu.

Enzi za uhai wake Dangote anadaiwa nyakati za usiku alikuwa akivaa nguo za kike aina ya dera na kuwakaba watu na kuwapora vitu huku akituhumiwa  kusababisha  vifo vya watu watatu na kumjeruhi 15.

Taarifa ya Polisi imemtaja Dangote kuhusika na kifo cha mtu mmoja, Ally Mbondei ambaye aliokotwa maeneo ya Unga Ltd jijini Arusha na kujeruhi watu kadhaa.

Hata hivyo, baada ya msako wa takribani mwezi mmoja na picha zake kubandikwa maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha, Polisi kwa kushirikiana na wananchi juzi walifanikiwa kumkamata na baadaye alifariki kwa kupigwa risasi akiwa anawakimbia polisi.

Katika Operesheni hiyo pia, polisi imemkamata mtuhumiwa mwingine, Hashimu Kibwerezi (20) mkazi wa Oysterbay jijini hapa na baada ya kuhojiwa alikiri kujihusisha na matukio ya uporaji na kuonyesha baadhi ya mali walizokuwa wakipora ambazo zimekamatwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Polisi Jamii Mtaa wa Kanisani, Abubakari Seif amesema kukamatwa kwa vibaka hao ni mafanikio makubwa kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakisumbua.

“Hasa huyu Dangote amesumbua sana wananchi kwa kupora na wizi wa vitu vyao nyakati za mchana na usiku, leo kukamatwa na kufariki ni faraja kwa wakazi wa Arusha,” amesema.



Post a Comment

0 Comments