Ticker

6/recent/ticker-posts

Jumaa Aweso,Dawasa mkipiga chafya nchi nzima inaugua mafua



DAR ES SALAAM: SERIKALI imeziagiza  Mamlaka za Maji nchini  kuwaunganishia maji wananchi wenye uhitaji kwa mkopo.

Agizo hilo limetolewa na  Waziri wa Maji, Jumaa Aweso leo Novemba 17,2023 katika hafla ya  utiaji saini utekelezaji wa mradi wa maji eneo la Kusini mwa Mkoa wa Dar es Salaam maarufu kama mradi wa Bangulo.

Amesema mkakati wa serikali ni kusambaza maji kwa asilimia 95 kwa mijini na asilimia 85 kwa vijijini  ifikapo 2025.

“Mwananchi anayetaka kuunganishiwa maji muhakikishe ndani ya wiki mbili kashapata huduma, hata kama hana hela muunganishieni kwa mkopo mumkate kidogo kidogo anapolipa bili yake ya maji,” amesema.

Mradi huo wa Bangulo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira ( Dawasa) unagharimu Sh bilioni 40 unatarajiwa kunufaisha  wananchi 450,000.

Aweso amesema  upatikanaji wa maji mwezi Julai 2022 hadi Juni 2023 kwa mjini umepanda kwa wastani  asilimia 88 na inatarajia kufika asilimia  91 mwezi Desemba 2023, wakati kwa upande wa vijijini  hali ya huduma imeongezeka kutoka asilimia 77 na inatarajiwa kufika asilimia 80 mwezi Desemba mwaka huu

“Dawasa mkipiga chafya nchi nzima inaugua mafua, hampoi, hamboi, nawapenda mpaka naumwa, mtoto akifanya vizuri kazi ya mzazi ni kumuombea dua tu, naamini mradi huu utatekelezwa na kumalizika kabla ya muda, ” amesema na kuongeza

“Mkandarasi alipwe fedha kwa wakati, vijana ambao wanaishi mradi unapotekelezwa wapewe ajira,   mkiaminiwa aminika sio mnaiba sementi, mara misumari, “amesema

Awali akizungumza Kaimu Mkurugenzi wa Dawasa, Kihula Kingu alisema mradi huo utanufaisha wananchi wa Wilaya tatu za  Ubungo, Temeke na Ilala  na majimbo manne ya uchaguzi  Ukonga, Segerea, Ubungo, Kibamba na Ilala.

Amesema,  awamu ya kwanza ya mradi itanufaisha wananchi wa Kata za Kwembe, Kitunda, Pugu Stesheni, Kipunguni na Mzinga.

Awamu ya pili ya mradi itanufaisha wananchi wa Kata ya Kivule, Kinyerezi, Zingiziwa, Majohe, Charambe, Kwembe, Buza, Msongola, Msigani na Mbezi.



Post a Comment

0 Comments