Ticker

6/recent/ticker-posts

Athari za kutibu ugonjwa wa macho kwa njia asili



Athari za kutibu ugonjwa wa macho kwa njia asili

Kukamulia maziwa ya mama kwenye jicho, kuliosha kwa maji yenye chumvi au kwa chai ya rangi, si miongoni mwa tiba za maambukizo ya ugonjwa wa macho mekundu ‘Red Eyes’ kama wengi wanavyodhani, wataalamu wanafafanua.

Tangu kuzuka kwa ugonjwa huo nchini, zimeshuhudiwa imani mbalimbali zikitumika kusaka suluhu ya maambukizo ya red eyes, hapo ndipo wengine hutumia dawa hizo wanazoziita za asili.

Kwa taarifa yako, bado hakuna tiba ya moja kwa moja ya maambukizo hayo na unapoambukizwa yatadumu kwa wiki mbili au sita kabla ya kupotea, kama inavyofafanuliwa na wataalamu wa ugonjwa huo.

Katika mahojiano yake na Mwananchi, Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio anasema zipo hatua zinazochukuliwa na wananchi ambazo ni hatari kwa afya ya macho yao.

Miongoni mwa hatua hizo, anasema ni kukamulia maziwa ya mama anayenyonyesha kwenye jicho lililoambukizwa ugonjwa huo, kuliosha kwa maji yenye chumvi au kwa chai ya rangi.

“Hairuhusiwi kutumia maji ya chumvi wala chai ya rangi, wengine wanatumia kunawa uso au macho na mama anayenyonyesha huwa anaweka maziwa yake, vyote hivyo haviruhusiwi na vinaweza kuleta madhara kwenye macho,” anasema.

Unapopatwa na maambukizi hayo kwa mujibu wa Dk Bernadetha, unapaswa kuendelea na utaratibu wa siku zote wa kujisafisha, kama kuoga na kuosha uso kawaida.

“Mtu akipata shida anaoga kama kawaida, anatumia taulo lake kujifuta uso kama kawaida lakini asichangie na mtu yeyote taulo hiyo.
“Kama kuna tongotongo au machozi yanayotoka machoni, unashauriwa kujifuta kwa tishu tena pembeni ya jicho na sio katikati,” anasema.

Kufuta katikati au kutumia nguo ngumu, anasema kunaweza kusababisha uvimbe zaidi au macho kuuma, kisha unapaswa kutupa hicho unachotumia kujifutia na unawe mikono.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, haishauriwi kutumia kitambaa kwa kuwa utakihifadhi na baadaye kukitumia tena, jambo linalosababisha kujiongezea ugonjwa.

Hata hivyo, anasema matumizi ya kitambaa yanaweza kusababisha maambukizo ya bakteria jichoni au jeraha la kemikali na hivyo kupoteza uwezo wa kuona kabisa.

Kulingana na mtaalamu huyo, inashauriwa mgonjwa asikimbilie hospitali haraka, labda pale anapokabiliwa kiasi cha kushindwa kuvumilia.

Msingi wa ushauri huo ni kile kilichoelezwa na Dk Bernadetha kuwa, kuna hatari ya kusambaza zaidi ugonjwa huo kwa kuwa hospitali unakutana na watu wengi lakini pia mwanga.

“Mtu akipata hiyo shida, atulie, augulie mwenyewe, azingatie kunawa mikono kwa vitakasa mikono au sabuni na inapotokea unapiga chafya funika pua pamoja na mkono ili usisambaze.

“Kwa sababu kuna uhusiano mikubwa kati ya ugonjwa wa macho na pua na mdomo kwa kuwa ugonjwa unaweza kuenea kwa njia mbalimbali,” anasema.

Hakuna tiba

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo anasema bado hakuna tiba maalum ya maambukizi hayo, badala yake dalili zake zinakadiriwa kuisha kwa muda wa wiki mbili hadi sita kwa baadhi ya watu.

“Wagonjwa wanashauriwa kufika katika kituo cha kutolea huduma za afya kwa ajili ya kupimwa na kupatiwa dawa ya kupunguza madhara kulingana na ishara zinazoonwa na daktari,” anasema.

Profesa Rugajjo anasema kuna namna lukuki zitakazowezesha kuzuia ugonjwa huo, ikiwemo kuepuka kugusa macho na iwapo utafanya hivyo unapaswa kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.

Anasema vile vinavyogusa macho yako unapaswa ama kuvitupa au kuvisafisha kwa maji ya moto na sabuni, lakini haupaswi kuchangia vipodozi, taulo za karatasi, nguo na dawa za macho.

“Funika mdomo na pua wakati wa kukohoa au kupiga chafya, pia tumia taulo tofauti na leso kwa kila mwanafamilia,” anasema.
Mtu anaambukizwa ugonjwa huo, kwa kugusa machozi au tongotongo kutoka kwenye macho yenye ugonjwa huo.

Anasema kugusana mikono na mtu mwenye maambukizo hayo ni sababu nyingine ya kuambukizwa ugonjwa huo na kwamba, dalili zake huanza kujitokeza kuanzia siku tano hadi 14 baada ya kupata vimelea.

Hata hivyo, anasema wanafunzi wanaougua wanashauriwa kukaa nyumbani hadi dalili zinapoisha kwa kuwa ni ngumu kuzuia maambukizo yasisambae kwenye mazingira ya shule.

Profesa Rugajjo anasema unapoona jicho linakuwa jekundu, linawasha na kuchomachoma, macho yanavimba, yanaogopa mwanga, yanatoa matongotongo meupe na ya njano ujue una dalili za ugonjwa huo.

“Uwezo wa kuona unakuwa kama kuna ukungu na unasikia maumivu ya macho hizi zote ni dalili za Red Eyes,” anasema. Kwa ujumla wake, anasema ugonjwa huo unasababishwa na kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho ‘Viral Keratoconjunctivitis’ na husambaa kwa kasi kubwa.

Kwa asilimia 80 mlipuko huo, anasema unasababishwa na kirusi cha ‘Adenovirus’.

Angalizo

Iwapo umebainika kuwa na ugonjwa huo, anasema ni vema kuepuka kutumia dawa zisizo rasmi na ambazo hazikuandikwa na daktari kwa wakati huo.

“Usitumie dawa za macho anazotumia mgonjwa mwingine au alizoandikiwa yeye awali alipokuwa na tatizo la jicho ili kuepuka madhara kwa kuwa dawa za macho ni tofauti kwa matumizi,” anasema.



Post a Comment

0 Comments