Ticker

6/recent/ticker-posts

Hospitali zilizosalia za Gaza haziwezi kukabiliana na idadi ya watu waliojeruhiwa



Hospitali zilizosalia za Gaza haziwezi kukabiliana na idadi ya watu waliojeruhiwa.

Mtaalam wa masuala ya dharura wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Sean Casey amesema hospitali zilizosalia za Gaza haziwezi kukabiliana na idadi ya watu waliojeruhiwa, ambapo Wizara ya Afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas ikikadiria kuwa zaidi ya watu 60,000 wamejeruhiwa tangu kuanza kwa vita hivyo huku mamia ya wengine wakijeruhiwa kila siku.

Casey ambaye pia ni mratibu wa kikosi cha Matibabu ya Dharura anasema madaktari na wauguzi watano au sita wanawashughulikia mamia ya wagonjwa kwa siku na kwamba alishuhudia wagonjwa wengi waliolala sakafuni na huwezi kutembea katika hospitali hizo bila kukanyaga mikono au miguu ya wagonjwa hao.”

Aidha Casey, ambaye hivi majuzi alifanya ziara ya wiki tano katika eneo hilo la Palestina lililokumbwa na vita amesema:

” Nimeshuhudia mara kadhaa maafa ya kibinadamu yanayotokea. Tunayashuhudia kila siku huko Gaza, na hali ikizidi kuwa mbaya zaidi, huku tukishuhudia kusambaratika kwa mfumo wa afya siku baada ya siku. Hospitali zinafungwa, wahudumu wa afya wanakimbia huku majeruhi wakiendelea kumiminika. Kunashuhudiwa pia ukosefu wa dawa na vifaa vya matibabu pamoja na ukosefu wa mafuta kwa ajili ya jenereta za hospitali zinazowezesha kupata umeme na mashine kufanya kazi.”

Mtaalam huyo wa WHO amesema Hospitali kubwa zaidi ya Gaza ya Al-Shifa ambayo ilikuwa na jumla ya vitanda 700, kwa sasa hutoa matibabu kwa majeruhi na wagonjwa wenye uhitaji wa dharura. Hospitali hiyo imekuwa pia kimbilio la maelfu ya watu ambao wanaishi katika vyumba vya upasuaji na sehemu zengine.

Hali mbaya ambayo haijawahi kushuhudiwa

Daktari wa Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu (ICRC) ameielezea hali katika hospitali za Gaza kuwa mbaya zaidi na ambayo haijawahi kushuhudiwa.  Kulingana na WHO ni hospitali 15 pekee kati ya 36 ndizo zinazofanya kazi huko Gaza.

Hayo yakiarifiwa , Rais wa Israel Isaac Herzog akizungumza katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos amesema Israel “inaomba” shehena ya dharura ya dawa inayotumwa kwenye mpaka wa Gaza kupitia Misri itawafikia mateka ambao bado wanashikiliwa na kundi la Hamas.

Wakati huo huo nchi ya Jordan imesema Israel inapaswa kuwaruhusu Wapalestina waliokimbia makazi yao huko Gaza kurejea makwao. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi katika mkutano na waandishi wa habari akiwa na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan mjini Amman. Kulingana na Safadi, ni muhimu kukomesha vita huko Gaza na kuepusha kuongezeka kwa ghasia katika eneo hilo.

(Vyanzo: Mashirika)



Post a Comment

0 Comments