Ticker

6/recent/ticker-posts

Idadi ya walioambukizwa kipindupindu mkoani Mwanza yafikia watu 34



Idadi ya walioambukizwa kipindupindu mkoani Mwanza imeongezeka kutoka watu 20 na kufikia watu 34.

Akizungumza leo Jumatano Januari 10, 2024 katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya msingi mkoani Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla amesema hadi kufikia jana usiku, wagonjwa walikuwa 26 lakini leo asubuhi wagonjwa wameongezeka wapya sita na hivyo kufanya idadi wafikie 34.

Mwanza. Idadi ya walioambukizwa kipindupindu mkoani Mwanza imeongezeka kutoka watu 20 na kufikia watu 34.

Akizungumza leo Jumatano Januari 10, 2024 katika kikao cha wajumbe wa Kamati ya Huduma ya Afya ya msingi mkoani Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla amesema hadi kufikia jana usiku, wagonjwa walikuwa 26 lakini leo asubuhi wagonjwa wameongezeka wapya sita na hivyo kufanya idadi wafikie 34.

Ametaja wilaya zenye maambukizi kuwa ni Ilemela, Nyamagana na Magu.

Kufuatia mlipuko huo, Makalla ameagiza wataalam wa afya kila wilaya kutengeneza mkakati wa kudhibiti ugonjwa huo usiendelee kusambaa sambamba na kuwahudumia wagonjwa wote kwa kasi.

Pia, ameagiza mamlaka za maji mkoani humo kuhakikisha maji yanatibiwa ipasavyo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa kile alichodai maji yasiyotibiwa hayatofautiani na maji ya kwenye mto ama lambo.

“Tukitoka hapa nataka tudhibiti ugonjwa huu usienee mkoani hapa na ili kufanikisha hilo ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya makusudi ya kudhibiti tatizo hili lisisambae tena kwa ushirikiano mkubwa,” amesema Makalla.

Ametahadharisha uuzwaji na ulaji holela wa chakula kwa mamalishe wanaofanya biashara zao maeneo yasiyo rasmi kuwa usipodhibitiwa itachangia ugonjwa huo kuenea na kuagiza hatua zichukuliwe.

“Nataka miwaambie wananchi kwamba hakuna gharama zozote kwa mgonjwa wa kipindupindu kutibiwa, mtu yeyote mwenye dalili za Ugonjwa wa Kipindupindu afikishwe hospitalini haraka na sio kumhudumia nyumbani au kwa waganga wa kienyeji na serikali tumejipanga kuwahudumia,” amesisitiza Makalla.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa ametaja wilaya zilizokumbwa na mlipuko huo kuwa ni Magu, Nyamagana na Ilemela huku Magu ikiathirika zaidi kwa kuwa na wagonjwa 21 hadi sasa na kwamba tayari kuna vituo vitatu vya kutolea huduma.

“Dalili za kipindupindu zinaanza kujitokeza ndani ya masaa 24 hadi 72 baada ya kupata maambukizi na mtu hukosa maji mwilini kutokana na kutapika na kuharisha hivyo jamii lazima iwe na matumizi sahihi ya vyoo, kuosha chakula kama matunda kwa maji ya moto, kutumia maji yaliyochemshwa na kuchunjwa vizuri,” Dk Rutachunzibwa.

Ulivyoibuka Mwanza
Januari 9,2024, Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Pima Sebastian na Mkuu wa Wilaya ya Magu (DC) mkoani humo,Rachel Kasanda walithibitisha kuwepo mlipuko huo mkoani Mwanza.

DC Kasanda, alisema mtu mmoja alifariki huku wengine 19 wakiendelea kutibiwa katika wilaya ya Magu, Ilemela na Nyamagana kutokana na ugonjwa huo huku 18 waliochangamana nao wakifiatiliwa.

Taarifa hiyo ilikuja zikiwa zimepita siku tano tangu watu watano waripotiwe kuugua ugonjwa huo uliolipuka katika eneo la mji mdogo wa Kagonga mkoani Shinyanga huku 13 wakilazwa na 452 waliochangama nao wakifuatiliwa.

DC Kasanda alisema aliyefariki ni mwanamme (Jina halikuanikwa) ambaye alitoka katika sherehe iliyofanyika kwa mmoja wa wake zake anayeishi Dutwa Mkoani Simiyu.

Alisema marehemu baada ya kutoka Dutwa mkoani Simiyu kurejea kwa mwanamke mwingine anayeishi wilayani Magu akiwa na dalili za kuharisha na kutapika, hali yake ilipobadilika alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani humo kisha kufariki akiwa mapokezi.

“Kwa hiyo baada ya kufariki ndugu wa maeneo mengine walikuja msibani lakini tuliwasambaratisha hakukuwa na matanga. Lakini kumbe kuna ambao walikuwa tayari wamepata maambukizi,” alisema Kasanda.

Via Mwananchi.



Post a Comment

0 Comments