Ticker

6/recent/ticker-posts

Kinara wa mtandao wa Wafanyabiashara wa dawa za kulevya Akamatwa



Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imemkamata kinara wa mtandao wa Wafanyabiashara wa dawa za kulevya aina cocaine nchini pamoja na kukamata jumla ya gramu 692.336 za cocaine zinazowahusisha Watuhumiwa wanne katika operasheni maalum zinazoendelea Nchini.

Mfanyabishara huyo wa mtandao wa cocaine ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu amekamatwa katika eneo la Boko Jijini Dar es Salaam pamoja na
washirika wake watatu ambapo kati yao wawili walikamatwa jijini Dar es Salaam na mmoja alikamatwa katika kijiji cha Shamwengo Wilaya ya Mbeya vijijini Mkoani Mbeya.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo akiongea leo Jijini Dar es salaam amesema Mamlaka imebaini Wafanyabiashara wa matandao wa cocaine wamekuwa wakisafirisha dawa hizo kwa kutumia Watu ambao humeza dawa hizo tumboni au kuweka
kwenye maungo mengine ya mwili, Mfanyabiashara aliyekamatwa ana mtandao mkubwa wa Wabebaji (punda) kutoka Nchi mbalimbali ambao huwatumia kusafirisha dawa hizo kwa njia ya kumeza, hivyo makosa yake yanaangukia katika uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka.

“Mamlaka inatoa onyo kwa wote watakaoendelea kujihusisha na uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha kwani, Serikali imeendelea kuiwezesha Mamlaka kwa kununua vifaa vya kisasa na mafunzo kwa Watumishi wa Mamlaka na hivyo kuwajengea ujasiri na weledi katika kutekeleza operasheni kwa ufanisi mkubwa, hivyo kwa wale wote watakaoendelea na kilimo cha bangi, mirungi na biashara ya dawa za kulevya za viwandani watashughuliwa ipasavyo”.



Post a Comment

0 Comments