Ticker

6/recent/ticker-posts

Kunyimwa unyumba chanzo mume kumchinja mkewe - Makete



Kunyimwa unyumba chanzo mume kumchinja mkewe – Makete

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani Njombe limesema chanzo cha Juma Kyando (36) kumchinja mkewe Tumaini Luvanda (35), kisha kukata mwili huo vipande vipande na baadhi kuvitu mtoni, ni ugomvi wa kifamilia wa muda mrefu uliosababisha mwanaume huyo kunyimwa unyumba.

Mauaji hayo ambayo yanatajwa kuwa ya kutisha, yalitokea usiku wa kuamkia Januari 8, 2024 katika kitongoji cha Dombwela, wilayani Makete. Ambapo Tumaini ameshazikwa jana Januari 9, 2024 katika makaburi yaliyopo Mamlaka ya Mji mdogo wa Iwawa katika wilaya hiyo.

Hayo yamesemwa leo Januari 10, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema familia hiyo ilikuwa na tatizo la kindoa la muda mrefu na mwanaume alikuwa akinyimwa unyumba na mkewe ambaye kwa sasa ni marehemu.

Amesema siku ya tukio aliondoka nyumbani na kuchelewa kurudi na alipohojiwa na mumewe hakuwa na maelezo mazuri, jambo lililompandisha hasira mwanaume na kutekeleza tukio hilo ambalo siyo zuri kulizungumzia.

Amesema katika ugomvi wa awali kuna baadhi ya majirani walifika na kuwaachanisha lakini inaonekana mtuhumiwa alipata ukichaa wa muda, ambapo jeshi hilo limesema litaendelea  kuthibitisha hilo kupitia madaktari.

“Hata ukiona ni namna gani alivyotekeleza lile tukio unaona kabisa kwamba ni mtu ambaye alikuwa uwezo wake wa kufikiria ulikuwa ni mdogo, ndiyo maana tumemkamata na tunaendelea kupata uchunguzi wa daktari ili kuona huyu mtu wakati anatekeleza hili tukio alikuwa mzima au alikuwa na kichaa,” amesema Banga.

Wakati Kamanda Banga akisema hayo, ndugu wa mtuhumiwa wa mauaji hayo, Medrick Kyando amesema mtuhumiwa hana historia ya kuwa na matatizo ya akili.

Amesema ameshangaa kuona ndugu yake katelekeza tukio hilo la kikatili kwa mke wake huyo, na kusababisha sintofahamu kwa majirani na jamii kwa ujumla.

“Ndugu yetu hana historia ya tatizo la akili ni fundi kujenga alikuwa hana makundi na hata tulipopigiwa simu kuhusu tukio hilo tulishtuka sana” amesema Kyando.

Wakati huo huo; Kamanda Banga amesema jeshi hilo limewakamata watuhumiwa 173 kutokana na kujihusisha na matukio mbalimbali yakiwemo ya wizi, uporaji na mauaji.

Amesema kwenye operesheni hiyo vielelezo mbalimbali vimekamatwa zikiwemo pikipiki tano ambazo ziliporwa katika kipindi hicho, televisheni tatu, simu, na mbolea ya ruzuku mifuko 94 ambayo iliuzwa kinyume na utaratibu.

“Vile vile tumekamata bidhaa nyingine za dukani ikiwemo mtungi wa gesi, solar panel na vifaa vingine” amesema Banga.

Amesema jeshi hilo limemkamata Denis Gadau (27), mkazi wa Ndulamo kwa tuhuma za kuiba pikipiki yenye thamani ya Sh1.8.

Amesema mtuhumiwa huyo aliiba pikipiki hiyo mtaa wa Iwawa kanisani  wilayani Makete,  i ambayo ni mali ya Baraka Mbongela (28) mkazi wa Iwawa mahakamani.

Amesema jeshi hilo linatoa rai kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na imani za kishirikina ambazo zimekuwa zikichangia mauaji na kuacha taharuki kwa jamii.



Post a Comment

0 Comments