Ticker

6/recent/ticker-posts

Madaktari wa upasuaji wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)



Kuzuiwa kwa timu za misaada ni tishio la karibuni kwa hospitali za Gaza: OCHA

Madaktari wa upasuaji wakimfanyia upasuaji mgonjwa katika hospitali ya Al-Quds huko Gaza. (Maktaba)

Kitendo cha kukataa mara kwa mara kwa mamlaka za Israel kuruhusu timu za misaada za Umoja wa Mataifa kupeleka misaada ya kibinadamu inayohitajika sana ndani ya Gaza kumezizuia hospitali tano za kaskazini mwa Gaza kupata “vifaa na vitendea kazi vya kuokoa maisha”, imeonya leo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya  kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA.

Huku kukiwa na ripoti mpya za kuongezeka kwa mashambulizi ya mabomu na mapigano katika Ukanda huo leo Jumatano, OCHA imesema maombi yamekataliwa mara tano tangu tarehe 26 Desemba ya kufika bohari kuu ya dawa katika mji wa Gaza na Hospitali ya Al Awda huko Jabalya, kaskazini zaidi mwa Gaza.

“Wakati huo huo, kuendelea kunyimwa mafuta kupeleka kwenye vituo vya kusukuma maji na usafi wa mazingira kunaacha makumi ya maelfu ya watu bila kupata maji safi na kuongeza hatari ya kufurika kwa maji taka, na hivyo kuongeza hatari ya kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza,” imesema OCHA.

Pia imebainisha katika tarifa yake ya hivi karibuni iliyotolewa jana jioni juu ya athari za vita huko Gaza.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, “Hospitali 15 kati ya 36 za Gaza zinasalia kufanya kazi kwa kiasi kidogo, tisa kusini na sita kaskazini.”

Tangu kuanza kwa uhasama, Umoja wa Mataifa na washirika wa afya wametoa huduma za afya na matibabu kwa takriban watu 500,000.

Hakuna dalili za kukoma kwa mashambulizi

Maendeleo hayo yamekuja kwa vile sehemu kubwa ya Ukanda wa Gaza na hasa maeneo ya kati na kusini katika majimbo ya Deir al Balah na Khan Younis, yalikumbana na mashambulizi makali zaidi ya Israel kutoka angani, nchi kavu na baharini katika saa 24 zilizopita, limesema shirika la OCHA.

Ufyatulianaji wa maroketi nchini Israel na makundi yenye silaha ya Palestina pia uliendelea, pamoja na mapigano yanayoendelea kati ya wanajeshi wa Israel na wanamgambo wa Hamas, hasa katika majimbo ya Deir al Balah na Khan Younis.

Ikinukuu mamlaka ya afya ya Gazan, OCHA imebainisha kuwa Wapalestina 126 waliuawa kati ya alasiri ya tarehe 8 na 9 Januari, wengine 241 wameripotiwa kujeruhiwa. Idadi ya jumla ya waliouawa ni takriban Wapalestina 23,210 na 59,167 kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya Israel, ambayo yalianza kwa kujibu mashambulizi ya kigaidi yanayoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na kusababisha vifo vya watu 1,200 wakiwemo watoto 36 na wengine 240 kuchukuliwa mateka.

OCHA inasema “Mamlaka ya Israel inakadiria kuwa takriban Waisraeli 136 na raia wengine wa kigeni wanasalia mateka huko Gaza.”

NGOs nazo hazijasalimika 

Kwa mujibu wa OCHA mashambulizi yanayoendelea ya Israel yamesababisha matukio mengi mabaya na matokeo mabaya kwa makumi ya maelfu ya raia OCHA ikibainisha kuwa wengi tayari wameukimbia mji wa Gaza na kaskazini kuelekea maeneo ya kati na kusini mwa Ukanda huo.

Katika tukio moja huko Khan Younis, mtoto wa miaka mitano wa mfanyakazi wa madaktari wasio na mipaka MSF, alikufa kutokana na majeraha yake baada ya makazi ya MSF kushambuliwa Jumatatu.

Huko Deir al Balah, watu wanne pia waliripotiwa kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa wakati nyumba moja kaskazini magharibi mwa jiji hilo ilipolengwa, na makombora imesema OCHA.

Ikinukuu jeshi la Israel, ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imeripoti kuwa kati ya tarehe 8 na 9 Januari, wanajeshi tisa wa Israel wameuawa huko Gaza, huku 183 wakiuawa tangu kuanza kwa operesheni ya ardhini na wafanyakazi 1,065 kujeruhiwa.

Msongamano husababisha tishio la magonjwa

Wakati huo huo, wasaidizi wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wamerejea kuonya juu ya hatari inayoongezeka ya ugonjwa katika Ukanda huo, haswa katika mji wa kusini wa Rafah, huku raia zaidi wakikimbia uhasama kufuatia maagizo ya Israeli ya kuwahamisha.

Kabla ya vita, Rafah ilikuwa nyumbani kwa takriban watu 280,000, lakini sasa ina idadi ya watu zaidi ya milioni moja, shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada kwa Wapalestina UNWRA lilisema jana katika chapisho la mtandaoni wake wa X.

“Mitaa yenye msongamano wa watu inashuhudia kuenea kwa magonjwa kwa kasi ya kutisha, wafanyikazi wa huduma za afya wamelemewa na mahitaji yanaongezeka”, shirika hilo lilisema.

Watu milioni 1.9 wametawanywa

Baada ya zaidi ya miezi mitatu ya ghasia, karibu asilimia 85 ya wakazi wa Gaza sasa wanaaminika kuwa wameyahama makazi yao ambao ni watu milioni 1.9  kulingana na takwimu za UNRWA.

Shirika hilo linaendelea kuwapa hifadhi karibu watu milioni 1.4 katika vituo vyake 155 kwenye majimbo yote matano lakini vituo hivyo vimezidisha idadi ya watu wa uwezo uliokusudiwa.

Vituo hivyo vya UNWRA pia vimepokea mashambulizi 63 ya moja kwa moja, shirika hilo limesema, huku takriban watu 319 waliokimbia makazi yao wakiuawa katika makazi ya shirika hilo na zaidi ya watu 1,135 kujeruhiwa tangu 7 Oktoba.

Jana tarehe 9 Januari, malori 131 yaliyosheheni vifaa vya msaada yaliingia Ukanda wa Gaza kupitia vivuko vya Rafah na Kerem Shalom, kulingana na OCHA.



Post a Comment

0 Comments