Ticker

6/recent/ticker-posts

Mafuriko Dar,Mvua kubwa yaleta balaa Dar



Mafuriko Dar,Mvua kubwa yaleta balaa Dar

Daladala zikiwa zimezima katika barabara iliyofurika maji eneo la Tazara, kufuatia mvua zilizoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam leo Januari 21, 2024. Picha na Edwin Mjwahuzi

Barabara hazipitiki, nyumba zazingirwa maji, wananchi wapata adha ya usafiri.

Dar es Salaam. Mvua inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam leo Jumapili Januari 21, 2024 imesababisha mafuriko na baadhi ya barabara kujaa maji, hivyo kutopitika.

Zaidi ya hilo, baadhi ya nyumba zilizo maeneo ya bondeni zimejaa maji, hivyo kuwalazimu wakazi wake kutoa mali nje.

Kuanzia saa nne asubuhi hadi saa 6.15 mchana eneo la Ubungo External, magari yaliyokuwa yakitokea Buguruni hayakuweza kupita kutokana na mitaro kando mwa  Barabara ya Mandela kujaa maji na kusababisha barabara kufurika.

Wananchi wakipita katika reli ambayo imefunikwa na maji kufuatia barabara inayotoka Tabata Mwananchi kwenda Tabata Kisiwani kufurika maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.  Picha na Edwin Mjwahuzi

Adha hiyo ilisababisha usafiri hasa kwa watumiaji wa dalalala zinazofanya safari Kawe, Mwenge, Makumbusho, Ubungo na Mbezi kuwa mgumu.

“Kupita kwenye hayo maji ni ‘riski’, unaweza kuharibu gari, bora kutokwenda kabisa, tusikilizie yapungue,” amesema Juma Hassan, dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Mbagala na Mbezi.

Kwa upande mwingine, athari ya mvua inayoendelea kunyesha tangu saa moja asubuhi leo Jumapili Januari 21, 2024 imesababisha daraja la Tabata Kisiwani kufurika maji, hivyo kusababisha mawasiliano yakatike kati ya Tabata Relini na Tabata Kisiwani.

Kwa wakazi wa Kimara Mwisho, kituo cha daladala eneo hilo kimejaa maji, hivyo kusababisha abiria kupanda daladala kwa tabu, baadhi ya madereva wakiogopa kuingiza magari kituoni.

Tabata Segerea nako mvua imesababisha changamoto ya usafiri wa umma katika stendi ya Tabata Segerea kwani abiria wamelazimika kusubiri muda mrefu kituoni kabla ya kupata usafiri.

Kutokana na mvua, abiria wenye miamvuli ndio walioweza kuingia kwenye magari wengine wakilazimika kusubiri mvua ipungue ndipo waweze kupanda dalalala.

“Konda tuondoke basi, tunachelewa kanisani,” amesikika abiria mmoja akimwambia kondakta wa daladala aliyekuwa amekaa nje ya gari yake.

“Gari inaondokaje tupu hivi, subiri gari ijae, kama una haraka angalia usafiri mwingine,” alisema kondakta wa daladala hiyo inayofanya safari kati ya Segerea na Kawe alijibu.

Kutokana na mvua, barabarani hakuna foleni isipokuwa maeneo yenye makutano ya barabara kama vile Baracuda na Tabata Bima.

Kwa wanaofanya safari za Posta na viunga vyake jijini Dar es Salaam, unaweza kuhisi ndipo ulipo ufukwe wa Coco, kwani maji yamejaa.

Baadhi ya wanaotembea mjini, mkono mmoja wameshika viatu na mwingine wameshikilia mavazi yao ambayo ni marefu ili kuendelea na safari.

Mwananchi Digital leo Januari 21, 2024 imeshuhudia baadhi ya chemba za majitaka eneo la Posta zikiwa zinatiririsha maji yalichanganyika na ya mvua.

Eneo kati ya jengo la Shirika la Bima la Taifa (NIC) hadi Wizara ya Afya, maji yametuama, pia kukiwa na matawi ya mti yaliyoangushwa kutokana na upepo ulioambatana na mvua.

Eneo jirani na ofisi za ubalozi wa Msumbiji pia barabara imejaa maji.

Katika tukio jingine, mti ulioanguka jirani na ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje umevunja ukuta.

Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2018 kuhusu athari za mafuriko Dar es Salaam, inasema miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Dola 5.3 bilioni (Sh13.3 trilioni) ipo hatarini kuharika kutokana na athari za mvua na mafuriko.

“Ingawa gharama hazijulikani, mafuriko yanaleta mzigo wa kiuchumi kwa kaya. Tafiti za kukadiria zinasema athari za hali ya hewa katika Jiji la Dar es Salaam ina mali ya miundombinu yenye thamani takriban Dola bilioni 5.3 iliyo katika hatari kutokana na athari za mafuriko,” imesema ripoti hiyo inayoitwa ‘Mazingira magumu na kustahimili mafuriko jijini Dar es Salaam’



Post a Comment

0 Comments