Red Eyes yapofusha Saba Dar wakati wakiitibu
Idadi inafanya jumla ya wagonjwa waliougua macho mekundu na kupata madhara kwa Tanzania Bara na Zanzibar kufikia 14.
Wizara ya Afya imesema watu saba jijini Dar es Salaam wamepata upofu kutokana na kutibu ugonjwa wa macho mekundu kwa njia za kienyeji, huku wawili kati yao vioo vya jicho vikitoboka.
Ugonjwa huo wa maambukizi kwenye ngozi ya juu ya gololi la jicho unaoitwa Conjunctivitis, maarufu Red eyes umesambaa mikoa 26 nchini.
Februari 7, 2024, mratibu wa huduma za afya msingi na matibabu ya macho Zanzibar, Dk Rajab Muhammed Hilali alitoa takwimu za watu saba kupata upofu baada ya matumizi ya dawa za kienyeji kutibu ugonjwa huo.
Athari za kutibu ugonjwa wa macho kwa njia asili
Idadi hiyo inafanya jumla ya wagonjwa waliopata madhara hasi kwa Tanzania Bara na Zanzibar kufikia 14.
Ugonjwa huo ulioripotiwa kwa mara ya kwanza Januari 13, 2024 athari zake hasi ni vidonda kwenye kioo cha jicho vinavyoweza kusababisha kovu kwenye jicho litakalomfanya mgonjwa apate uoni hafifu au kupoteze uwezo wa kuona kabisa.
Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumapili Februari 18, 2024, Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, Profesa Paschal Ruggajo amesema hadi Februari 15, watu saba walitolewa taarifa ya kupata madhara kwenye vioo vya jicho.
“Watano wamepata vidonda kwenye kioo cha jicho na wawili walikutwa vioo vya jicho vimetoboka. Wagonjwa wote walionwa kwenye vituo vya tiba vilivyopo Dar es Salaam na umri wao ni kati ya miaka 21 hadi 42.
“Baadhi ya vitu vilivyotumika na waathirika hao ni pamoja na maji ya chumvi, tangawizi, maji ya majani ya mbaazi, vitunguu swaumu, chai ya rangi, vicks na dawa zenye viambata vya steroids,” amesema Ruggajo.
Profesa Ruggajo amesema wizara imeendelea kufuatilia mwenendo wa maambukizi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujikinga na ugonjwa huo.
Amesema hadi Februari 15 2024, jumla ya wagonjwa 14,641 wametolewa taarifa, walioonwa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwenye mikoa 26.
Dar es Salaam inaongoza kwa idadi ya wagonjwa 6,940, Pwani (4,480), Morogoro (630) na Dodoma (550).
Profesa Ruggajo amesema wizara inaendelea na hatua mbalimbali za kinga na udhibiti wa ugonjwa huo, ikiwamo utoaji wa elimu kwa kutumia wataalamu wa afya kupitia vyombo vya habari.
“Elimu inatolewa maeneo yenye mikusanyiko hususani shule, magereza na vyuo, nyumba za ibada, usambazaji wa vipeperushi na utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa kupitia vituo vyetu vya tiba na mitandao ya kijamii,” amesema.
Amesema wizara pia inaendelea kuratibu na kusimamia huduma mkoba za macho kwenye maeneo mbalimbali nchini na kubaini wagonjwa wenye shida ya macho mekundu na kuwapatia elimu.
“Hadi sasa vipindi vya kwenye runinga zaidi ya 20 vimetolewa na wataalamu wetu wa afya, redio za kijamii zaidi ya 25 kwenye mikoa mbalimbali, ikiwemo ambayo haina wagonjwa,” amesema.
Amesema wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zaidi ya 25,000 wamefikiwa kwenye shule zao pamoja na walimu wao.
Profesa Ruggajo amesema wanaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya kutofuata kanuni zilizotolewa, baada ya kupata taarifa ya wagonjwa kutumia tiba zisizo rasmi na kupata madhara.
Kutokana na hilo, amesema wizara iliandaa video na kuirusha kwenye vyombo mbalimbali vya kuelimisha.
Akizungumza na Mwananchi Februari 8, 2024, Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho, Wizara ya Afya, Dk Bernadetha Shilio alisema baadhi ya wagonjwa wanaopokewa kioo cha jicho kinabainika kumeharibika.
Amesema wagonjwa wa aina hiyo wanapotibiwa bado kunakuwa na kovu lenye rangi nyeupe kama karatasi ambalo likibaki hivyo moja kwa moja hupata ulemavu wa kutoona.
Matibabu sahihi:
Wizara inaelekeza hatua za kuchukua kwa kuosha uso kwa maji safi na sabuni mara kwa mara.
Tumia dawa ya paracetamol kumeza kwa ajili ya kupunguza maumivu
Nenda kituo cha tiba kwa ajili ya uchunguzi, kama hupati nafuu.
Hakikisha mikono na uso inakuwa safi muda wote.
Jizuie kugusa macho yako kadri uwezavyo.
Tumia vipukusi (vitakasa mikono) mara kwa mara.
Epuka kushikana mikono au kugusa vitu vinavyoguswa na wengi.
Tumia taulo au leso za karatasi kufuta tongotongo au machozi.
Nenda kituo cha kutolea huduma mara upatapo dalili.
Kumbuka kufua mashuka na mataulo kila siku.
Via:Mwananchi
Soma Zaidi kuhusu Red eyes;
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!