Kwanini uwezo wa kupata mimba hupungua baada ya miaka 35?

Kwanini uwezo wa kupata mimba hupungua baada ya miaka 35?

Wanasayansi wanasema, hadi umri wa miaka 35, wanawake wengi hawana matatizo kwenye uzazi, lakini baada ya umri huo uwezekano wa kupata mimba huanza kupungua kwa kasi.

Ni kweli kwamba wanawake wengi wenye umri wa zaidi ya miaka 35 hupata ugumu wa kushika mimba na wakati mwingine wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo yanayohusiana na ujauzito na uzazi kuliko wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 35.

Hata hivyo, kupungua kwa uwezo wa kupata mimba ni mchakato wa polepole sana, sio jambo la ghafla, na mchakato huo unatofautiana kutoka kwa mwanamke mmoja hadi mwingine.

“Kuanzia umri wa miaka 35, ubora na wingi wa mayai hupungua kwa kasi,” anasema Lorraine Casavant, daktari wa uzazi na mtafiti katika Chuo cha Imperial London.

Lakini Profesa Anja Bisgaard Pinborg, mkuu wa idara ya uzazi katika kliniki ya Rigshospitalet huko Copenhagen, anasema, “wanawake wengi wana matatizo ya kupata mimba baada ya umri wa miaka 40, hata kama wanakoma hedhi wakiwa na umri wa wastani wa miaka 51.”

Ni vigumu kupata ujauzito

Wataalamu wanaelezea hasa sababu ni mbili; wingi na ubora wa mayai.

Wakati wa kuzaliwa, wanawake huzaliwa na mayai yote ambayo watakuwa nayo. Ni idadi ya mayai karibu milioni mbili, lakini wakifika kubalehe idadi ya mayai ni 600,000 tu.

Na idadi hiyo inazidi kupugua kadiri umri unavyosonga. Umri unaposonga wanawake wanakuwa na mayai machache na ubora wao pia hushuka.

Kwa hivyo inakuwa vigumu zaidi kupata mimba kwa njia ya kawaida na, hata kama utafanya matibabu ya uzazi, kiwango cha mafanikio kwa ujumla kinaweza kuwa chini kuliko ungekuwa mdogo.

Ubora wa yai pia ni muhimu. Umri unaposonga idadi ya mayai yasiyofaa kwa uzazi pia huongezeka.

Hatari ya kuharibika mimba

Uzazi wa wanaume pia huanza kupungua baada ya miaka 30.

“Karibu na umri wa miaka 40, chromosomes 21 hubadilika zaidi, ambayo huongeza hatari ya matatizo ya mimba. Na ndiyo sababu ya mimba nyingi huharibika,” anaeleza Bi. Pinborg.

Utafiti uligundua kwamba hatari ya kuharibika kwa mimba ni karibu asilimia 10% kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24, lakini hatari huongezeka kwa kasi unapokaribia umri wa miaka 35, ambapo ilizidi asilimia 20%.

Kwa umri wa miaka 42, zaidi ya nusu ya mimba – karibu asilimia 55% – huisha kwa kuharibika. Changamoto za uzazi na mtoto kufa tumboni hutokea zaidi.

Katika utafiti nchini Norway, hatari ya kuzaa mtoto aliyekufa huongezeka kutoka umri wa miaka 35-39 na hatari ni kubwa zaidi katika kundi la umri wa miaka 45-49.

Hata hivyo, hatari ya kuzaliwa mtoto aliyekufa inachangiwa na mambo mengine pia. Mambo kama vile uvutaji sigara, unywaji pombe na unene wa kupindukia huathiri ubora wa yai.

Kwa Wanaume hali Ipoje?

Zaidi ya hayo, kwa kuzingatia sana uzazi wa kike hutufanya tusahau kwamba umri wa mwanaume pia ni muhimu.

Uchunguzi wa wanandoa wa Ulaya ulionyesha kuwa, umri wa mwanaume chini ya miaka 35 hauathiri uwezekano wa kupata mimba, hali hubadilika unapokaribia miaka 40.

“Kati ya wanawake wenye umri wa miaka 35, idadi ya ambao hushindwa kupata mimba huongezeka kwa 18% ikiwa mpenzi wa kiume ana umri wa miaka 35. 28% ikiwa mpenzi wa kiume ana umri wa miaka 40,” utafiti unaonyesha.

Ikiwa mwanaume ni zaidi ya miaka 40, hatari ya kuharibika kwa mimba pia huongezeka. Uchunguzi umeonyesha kuwa ubora wa manii huzorota kadiri umri unavyoongezeka.

Ingawa, ni tofauti na mayai, manii huzaliwa upya kila baada ya miezi miwili hadi mitatu, kupungua kwa ubora kunaweza kutokana na uharibifu wa DNA, sumu ya mazingira na kupungua kwa homoni.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!