Ticker

6/recent/ticker-posts

Mfahamu aliyebuni bunduki ya AK-47, akafa maskini huku akijuta



Mfahamu aliyebuni bunduki ya AK-47, akafa maskini huku akijuta

Moja kati ya picha maarufu za aliyewahi kuwa kiongozi wa kundi la Al Qaeda Osama bin Laden,  ni ile ambayo pembeni yake inaonekana bunduki aina ya   ‘AK-47’.
Inawezekana jina la bunduki hii sio geni kwenye masikio ya watu wengi. Pia hupendelewa kuiitwa ‘Mrusi’, ikiwa na maana ya kule ilipotokea.

Imekuwa ikitumika na majeshi, magaidi, wahalifu na watu mbalimbali kwenye kutekeleza majukumu yanayohitaji silaha aina ya bunduki kwa  sababu ya ubora wake.
Kwa mara ya kwanza bunduki hii ilianza kutumika kwenye jeshi la umoja wa Soviet mwaka 1948 na hadi kufikia sasa kwa mujibu wa mtandao wa Fobres,  kuna zaidi ya bunduki milioni 200 za aina hii.

Kwa mujibu wa mtandao wa Global Financial Integrity, silaha hii inauzwa kati ya Dola 600(Sh1.5 milioni) kule Afghanstan, pia inauzwa kwa Dola 1200(Sh3 milioni) kule nchini Mexico lakini kwenye baadhi ya maeneo silaha hii inauzwa hadi dola 3000(Sh7.6 milioni), ingawa pia kuna huuzwa hadi kwa dola 15(Sh38,103).
Fobres pia imeripoti kwamba  AK-47 hii huzalisha hadi dola 1.7 bilioni(Sh4.3 trilioni) kila mwaka.

Wakati bunduki hii ikionekana kuzalisha kiasi hicho kikubwa cha pesa, mwanadamu Mikhail Kalashnikov aliyeibuni  alifariki akiwa maskini  mwaka 2013,  huko  Izhevsk licha ya ubunifu wake  kuuzwa na kuzalishwa kiasi kikubwa cha pesa duniani.

Kalashnikov alizaliwa mwaka 1919, miaka kadhaa baada ya  mapinduzi ya Bolshevik kwenye familia ya watoto 19, baba na mama yake wote walikuwa ni wakulima huko kusini mwa Russia eneo la  Altai.

Akiwa na umri mdogo alikuwa na ndoto ya kuwa mwana mashairi na hadi anafariki alikuwa na vitabu sita vya mashairi licha ya kubuni bunduki hii hatari.
Ripoti kutoka tovuti ya Radio Free Europe/Radio Liberty zinaeleza kwamba Kalashnikov alipokea medali nyingi kutokana na ubunifu wake ikiwemo tatu za Order of Lenin awards, pia rais wa mstaafu wa Russia Dmitry Medvedev aliwahi kumuita shujaa wa nchi hiyo.

Lakini mwenyewe alithibitisha kwamba hakuwahi kupata chochote kwa kutengeneza bunduki hiyo na hadi anafariki maisha yake yalikuwa magumu, akiishi kwa pensheni za jeshi na kiasi kidogo cha pesa alizopata kwa kuruhusu jina lake kutumika kwenye vinywaji na bidhaa  mbalimbali kama vodka, umbrellas, na knives.
Mbali ya umasikini pia Kalashnikov alifariki huku akiwa na majuto kwa kutengeneza bunduki hiyo inayotumika kwenye masuala mbalimbali ya kigaidi.

Alivyoibuni silaha hii

Hadithi  ya kubuni bunduki hii ilianzia mwaka 1938 pale alipochaguliwa kujiunga na jeshi la Russia mwaka 1938 ambalo kwa wakati huo lilikuwa likiitwa Red Army.
Alianza kazi kama dereva na fundi wa kifaru  na akapanda cheo hadi kufikia kamanda wa kifaru.

Oktoba, 1941 akiwa kwenye vita ya pili ya dunia alipata majeraha ambayo ilibidi apelekwe hospitali kwa ajili ya matibabu.

Wakati anapatiwa matibabu hospitali alisikia baadhi ya askari wa jeshi la Russia wakilalamika juu ya ubora wa bunduki walizokuwa wanatumia.

Yeye hakuwa anatumia sana bunduki hizo kwa sababu muda mwingi alikuwa kwenye kifaru,  lakini baada ya kusikia mazungumzo hayo, aliingiwa na shauku ya kutaka kutengeneza bunduki itakayokuwa na ubora zaidi.

Alichora mchoro na kupeleka kwa baadhi ya makamanda wake, lakini hawakuonyesha kushawishika.

Hakukata tamaa na ilipofika mwaka 1942 alifanikiwa kuingizwa kwenye kikosi cha ubunifu wa silaha cha jeshi mwaka 1942.

Ilipofika mwaka 1946 tayari alishaunda silaha hii na akaiingiza kwenye shindano la bunduki za kushambulia ambapo aliita  “Avtomat Kalashnikova 1947” (AK-47), ikashinda.

Baada ya kushinda ilingizwa rasmi kwenye mfumo wa jeshi la Russia na ndani ya miaka miwili bunduki hii tayari ilikuwa kipenzi cha wanajeshi wote wa jeshi hilo na ilipofika mwaka  1956, ndio ilikuwa bunduki bora zaidi.

Ubora wa AK-47 ulichagizwa na uwezo wake wa kufanya kazi vizuri kwenye mazingira mbalimbali hususani yale ya baridi na hata joto kali.

Bunduki hii ilitumika sana kwenye vita ya  Vietnam, pia ipo kwenye bendera ya  Msumbiji ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa silaha hiyo kwenye kuipa uhuru nchi hiyo.

Tangu kutengenezwa kwake hadi sasa ikiwa imepita miaka zaidi ya 60,  tafiti mbalimbali  zinadai bunduki hii imesababisha vifo na madhara kwa watu wengi kuliko yake yaliyosababishwa na bomu la nyuklia lililopigwa katika Jiji la  Hiroshima na Nagasaki.

Majuto

Ukiacha sehemu mama iliyokuwa inatumika hapo zamani, kwa  sasa bunduki hii imesambaa sana na inatumika na baadhi ya wafanya biashara wa dawa za kulevya na magaidi mbalimbali.

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa,  Kofi Annan mwaka 2001, aliwahi kusema:”Baadhi ya maeneo, AK-47 inauzwa kwa dola 15, na muda mwingine hubadilishwa kwa gunia la ngano, ni rahisi kuzitumia na unaweza kufundishwa ndani ya muda mfupi tu, ndio maana hata watoto wadogo wanazitumia, ni rahisi kubeba na hata kuzisafirisha, pia zinahitaji matengenezo madogo, hivyo huwa zinadumu kwa muda mrefu sana.”

Hili ni moja kati ya jambo linalomtesa sana Kalashnikov ambaye mwaka 2002, alipofanya mahojiano na Reuters alieleza kwamba hajisikii vizuri akiona bunduki hii inatumika vibaya.

“Pale ninapomuona kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden  akiwa ameshika AK-47, huwa napatwa na huzuni, lakini nitafanya nini? watu sio wajinga, wao wenyewe wanachagua bunduki nzuri kwa matumizi yao. Niliitengeneza bunduki hii ili itumike kwa ajili ya kulinda mipaka ya nchi yangu, sio kosa langu bunduki niliyoitengeneza kutumika vibaya.”

“Muda mwingine nawaza labda ningevumbua mashne  ambayo ingeweza kusaidia wakulima kufanya kazi zao, kama vile mashine ya kukata nyasi.”

“Kuna muda watu wananiuliza nawezaje kulala wakati watu wengi wamekufa kwa sababu ya silaha niliyoitengeneza, lakini ukweli ni kwamba sio mimi ninayepaswa kulaumiwa bali wanasiasa ambao wameshinswa kukubaliana kwa amani ili silaha yangu isitumike.

Baada ya uvumbuzi wake, mnamo 1949, Kalashnikov alihamia Izhevsk, ambako alikuwa akifanya kazi kama mbunifu mkuu wa moja ya kambi, akasimamia utengenezwaji wa  AK-47 na marekebisho yake.

Mkewe  Yekaterina, alifariki mwaka 1977, alikuwa akiishia na mwanawe  wa kiume Viktor na watoto wake wawili wa kike  Nelly na Elena hadi kufikia kifo chake, ingawa aliwahi kubahatika watoto watatu wa kike lakini mmoja aliyeitwa  Natasha, alifariki mwaka  1983.

Desemba 23, 2013 Kalashnikov alifariki kutokana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo, viongozi mbalimbali ikiwemo rais wa sasa wa Russia Vladimir Putin walituma salamu za rambirambi.

Baada ya kifo chake Januari, 2014, gazeti  Izvestia la nchini humo lilichapisha barua aliyoiandika ndani ya miezi sita kabla ya kifo chake aliyokuwa ameituma kwenye moja ya kanisa alilokuwa akifanya ibada.

Moja kati ya mistari ya barua hiyo Kalashnikov alieleza kwamba ana maumivu ya kiroho,: ‘’Bado naendelea kuwa na maswali ambayo sijapata majibu yake, kutokana na bunduki yangu kutumika kuua watu, je natakiwa nilaumiwe kwa vifo vyao”
Alizikwa Desemba  27 katika makaburi ya kijeshi  nje kidogo ya Jiji la  Moscow

Via:Mwananchi.



Post a Comment

0 Comments