Ticker

6/recent/ticker-posts

Ajali ya Baltimore: Mabaharia 21 bado wamekwama kwenye meli



Ajali ya Baltimore: Mabaharia 21 bado wamekwama kwenye meli

Takriban wiki moja baada ya Daraja kuu la Francis Scott mjini Baltimore kuporomoka nchini Marekani, zaidi ya mabaharia 20 bado wamekwama kwenye meli iliyohusika kwenye ajali.

Wafanyakazi wengi wa meli ya Dali, yenye urefu wa futi 948 (289m), wanatoka India. Mmoja alijeruhiwa kidogo wakati meli hiyo ilipogonga daraja.

Watu sita waliuawa katika ajali hiyo.

Wachunguzi wanajitahidi ili kubaini ni nini hasa kilichosababisha mgongano huo, na haijulikani ni lini wafanyakazi wataweza kuondoka kwenye chombo hicho.

Haya ndiyo tunayojua kuhusu wanaume walio kwenye Dali na hali zao za sasa.

Tunajua nini kuhusu wafanyakazi?

Kwa jumla, wafanyakazi 21 walikuwa kwenye Dali wakati wa ajali, ambayo ilitokea dakika chache tu baada ya safari ya siku 27 ya meli hiyo kuelekea Sri Lanka.

India imethibitisha kuwa 20 kati yao ni raia wake. Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa Wahindi 315,000 wameajiriwa katika tasnia ya kimataifa ya bahari, karibu karibu asilimia 20 ya jumla. Wahindi wanachukua nafasi ya pili baada ya Wafilipino katika sekta hii.

Mfanyakazi mmoja anatoka Sri Lanka, kulingana na walinzi wa pwani ya Marekani.

Afisa mmoja wa India alisema wiki iliyopita kuwa wafanyakazi wote wako katika afya njema, ikiwa ni pamoja na mmoja aliye na jeraha dogo, ambalo lilihitaji kushonwa.

Ni machache yanajulikana kuhusu wafanyakazi, historia yao au uzoefu wao.

Wafanyikazi wanaendeleaje?

Miongoni mwa watu wachache ambao wamekuwa wakiwasiliana ni Joshua Messick, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Kimataifa cha Baharini cha Baltimore, shirika lisilo la faida ambalo linafanya kazi kulinda haki za mabaharia.

Bw Messick aliambia BBC kwamba amewasiliana kwa njia ya WhatsApp na wafanyakazi baada ya kupanga utoaji wa kifurushi cha huduma ambacho kilijumuisha maeneo yenye WiFi.

Aliwataja kuwa “wamechanganyikiwa” na kwa kiasi kikubwa kukaa kimya kuhusu hali yao wakati uchunguzi ukiendelea.

“Hawasemi mengi hata kidogo kwa mtu yeyote ambaye amekuwa akiwasiliana nao,” Bw Messick alisema.

“Hawakuwa na WiFi hadi Jumamosi na hawakujua kwa hakika mtazamo wa watu wengine duniani ulikuwaje. Hawakuwa na uhakika kama walikuwa wanalaumiwa. Hawakujua walichotarajia.”

“Pia wako katika hali ya tahadhari. Wanachoweza kusema kinaweza kuihusu kampuni. Nafikiri kwamba wameshauriwa kuwa watulivu kwa wakati huu.”

Andrew Middleton, ambaye anaendesha huduma ya injili baharini – mpango unahudumia meli zinazopitia Baltimore – alisema amekuwa akiwasiliana na wafanyakazi “mara kadhaa kwa siku” tangu ajai hiyo itokee.

“Wanasema kwamba wote wako sawa,”

Ni lini wataruhusiwa kutoka kwenye meli?

Mamlaka yamesema kwamba – kwa sasa – hakuna mpango wa kuwashusha wafanyakazi wa Dali, ambao bado wanafanya kazi ya kutunza meli hiyo. Haiwezekani wataondoka kwenye chombo hadi kihamishwe – mchakato mgumu na unaoweza kuchukua muda mrefu.

Siku ya Ijumaa, Mkuu wa Walinzi wa Pwani Shannon Gilreath alisema kuwa kuhamisha Dali ni kipaumbele cha pili kwa kufungua tena bandari ya Baltimore na njia ya usafirishaji.

Hata katika hali ya kawaida, kuwashusha wafanyakazi raia wa kigeni kutoka kwa meli katika bandari za Marekani kunahitaji nyaraka muhimu.

Mbali na visa, mabaharia wanahitaji kuwa na pasi halali za ufukweni zinazowaruhusu kushuka kwenye meli. Pia wanahitaji wasindikizaji wa kuwapeleka kutoka meli hadi lango, ingawa kazi hiyo inaweza kufanywa na mashirika yasiyo ya faida ambayo hufanya kazi na mabaharia katika eneo hilo.

Haijabainika iwapo wafanyakazi wa Dali wana nyaraka zinazohitajika kuondoka kwa meli.

Kituo kinachosimamia huduma kwa ajali ya Baltimore kiliiambia BBC siku ya Jumatatu kwamba haijulikani ni muda gani uchunguzi utaendelea na “hadi mchakato ukamilike, wafanyakazi wataendelea kubaki ndani ya meli”.

Chirag Bahri, mkongwe wa safari za baharini wa India ambaye sasa anahudumu kama meneja wa mtando wa kimataifa wa Ustawi na Usaidizi kwa wasafiri wa kimataifa wenye makao yake makuu Uingereza, alisema kuwa anaamini kuwa huenda itachukua muda wa miezi kadhaa hadi mabaharia wote waweze kurejea nyumbani.

Wafanyakazi wanahitaji nini?

Wafanyakazi wa Dali wamepewa chakula, maji na vifaa vingine vilivyokusudiwa kwa safari yao ya kwenda Sri Lanka.

Wafanyakazi hao pia wataweza kupokea vifurushi kutoka kwa mashirika yasiyo ya faida ambayo yanafanya kazi na mabaharia, ambavyo Bw Messick alisema vitajumuisha bidhaa za kuoka na vitu vingine

Bw Messick anasema mahitaji makubwa zaidi ni ya kisaikolojia.

Anasema kuwa kupambana na uchovu na kuchoka wakati haufanyi kazi ni miongoni mwa changamoto kubwa wakati mabaharia wanatengwa kwa muda mrefu. Wengi wa mabaharia ambao mara nyingi ni wachanga watageukia michezo ya video na mitandao ya kijamii ili kupitisha wakati.

“Meli zenye furaha zaidi ni zile ambapo wafanyakazi wanaweza kuja pamoja na kufurahia kuwa pamoja,” Bw Messick alisema. “Lakini sio hivyo kila wakati.”

Bw Bahri alisema anatarajia kuwa wafanyakazi wa meli hiyo watahitaji usaidizi wa afya ya akili kutokana na tukio hilo na umulikaji wa vyombo vya habari kuhusu nini kilienda vibaya na ni nani, kama kuna mtu yeyote, wa kulaumiwa.

“Kila mtu sasa anajaribu kufuatilia mkasa. Hilo lazima likome,” alisema.

“Wasafiri wa baharini huenda tayari wamepatwa na kiwewe na mkazo. Bado wako kwenye meli katika nchi ya kigeni. Tunapaswa kusimama nao na kuwafanya wajiamini kuwa hawatahukumiwa wakati huu wanahitaji msaada.” Bbc



Post a Comment

0 Comments