Ticker

6/recent/ticker-posts

Wiki chache zilipita na nilipoenda kwa daktari aliniambia nina ujauzito



‘Nilitaka kujiua baada ya kugundua nimepata ujauzito kutokana na ubakaji’

Alienda kuchota maji mtoni kama kila siku. Ghafla, wanaume wawili walimkamata kwa nyuma, wakamwekea kisu kooni, wakampiga na mmoja wao akambaka.

Kwa sababu ya ubakaji huo, Fausia ambalo siyo jina lake la kweli, alipata mimba.

Kuanzia wakati huo, matatizo yalianza ambayo yangebadilisha maisha yake milele.

Wabakaji, ambao aliwafahamu vyema, walitishia kumuua yeye na familia yake yote ikiwa angesema kilichotokea.

Fausia alitaka kutoa mimba hiyo lakini nchini Honduras utoaji mimba ni kinyume cha sheria bila kujali mhusika yuko katika hali gani. Haijalishi ikiwa mwanamke alibakwa, maisha yake yamo hatarini au ikiwa ujauzito una matatizo yoyote.

Pia hakuwa na uwezo wa kupata tembe ya dharura ya kuzuia mimba, ambayo ingemzuia kupata ujauzito, kwa sababu ilikuwa imepigwa marufuku wakati huo.

Yeye ni mwanamke wa kiasili wa Watu wa Nahua na mtetezi wa haki za binadamu katika nchi yake.

Honduras ni mojawapo ya mataifa sita katika Amerika ya Kusini na Caribbean – pamoja na El Salvador, Nicaragua, Jamhuri ya Dominika, Haiti na Suriname – ambapo utoaji mimba ni marufuku kabisa.

Kituo cha Haki za Uzazi na Kituo cha Haki za Wanawake kiliwasilisha kesi mbele ya Kamati ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kwa lengo la kutaka “haki kwa Fausia” na Honduras kurekebisha mfumo wa kisheria ambao unaharamisha kabisa utoaji wa mimba.

BBC Mundo iliwasiliana na serikali ya Honduras ili kujua maoni yake lakini hadi wakati wa kuchapishwa kwa makala haya tulikuwa hatujapata jibu.

Huu ni ushuhuda wa Fausia alioeleza wakati wa mahojiano. Baadhi ya maelezo ya simulizi yake yameachwa ili kulinda utambulisho wake.

“Kwa kuwa nyumbani hatukuwa na huduma ya maji ya kunywa, nilienda mtoni kutafuta maji ili kuandaa chakula cha jioni. Nilipokuwa nikifanya hivyo, wanaume wawili waliokuwa wamejificha kwenye kichaka cha nyasi, walinivamia kwa nyuma. Wakaniwekea kisu kooni kisha wakanishika mikono yangu kwa nyuma.

“Niliwaambia wasinidhuru, waniache tafadhali, kwamba sina pesa, lakini waliniziba mdomo na kunipiga. Mmoja wao alinibaka.”

“Wanaume hawa ni kizazi cha familia iliyonyakua sehemu ya ardhi kutoka kwa baba yangu. Miezi michache kabla, tukio lilikuwa limetokea kuhusu ardhi. Jamaa mmoja wa walionibaka alienda kubomoa uzio wa shamba letu na kuniambia utalipia, nitakutumia genge la watu.”

“Sikuyachukulia maneno yake kwa uzito, lakini baada ya shambulio hilo tuliketi na kutathmini kilichosemwa na kile kilichotokea na tukagundua kwamba yalihusiana na suala la ardhi.”

“Wiki chache zilipita na nilipoenda kwa daktari aliniambia nina ujauzito.

“Ziwezi kueleza nilichohisi wakati huo. Nilijisikia vibaya, nilijiona mchafu, ni jambo ambalo halikuwa katika mipango yangu, ambalo sikutaka, na hasa jinsi lilivyotokea.

“Mwitikio wangu ulikuwa mbaya, ulikuwa kutokubaliana na uhalisia wa mambo, “Sitaki, sitaki, sitaki,” kila wakati nilifikiria hivyo.”

Uavyaji mimba sio tu kwamba hauruhusiwi nchini Honduras, lakini pia umepigwa marufuku na Katiba ya nchi hiyo. Mnamo Januari 2021, Bunge la Kitaifa liliidhinisha katika mjadala, mmoja marekebisho ya katiba ambayo yanapiga marufuku kabisa ya kukatizwa kwa ujauzito.

Kila siku wasichana watatu walio chini ya umri wa miaka 14 hupata mimba kutokana na kubakwa, kulingana na data ya Wizara ya Afya (2022).

Daktari aliniuliza nini kimetokea. “Umewasilisha malalamiko?” aliniuliza, Hapana, nilijibu, kwa sababu walikuwa wamenitishia kuwa wataniua ikiwa nitatoa taarifa.

Alipendekeza nifanye hivyo. Nilienda kwa Wizara ya Umma na daktari wa uchunguzi alinitibu.

Alinichunguza na kusema, “Tunajua tayari una mimba. Ukitoa mimba au tukagundua kuna kitu kimetokea kwenye ujauzito huu, tutakuweka gerezani kwa sababu utoaji wa mimba ni marufuku nchini.”

“Sikutaka kuendelea na ujauzito. Nikawa na uchungu mwingi sana, nikakata tamaa na sikutaka tena kuendelea na mateso hayo.”

“Ilikuwa ni mimba hatari kwangu, kwa miezi tisa nikihisi kichefuchefu, afya yangu ya kimwili ilikuwa mbaya kwa sababu sikuweza kula.”

“Muda ulipita na mara kadhaa nilifikiria kujiua kwa sababu nilijiona sina thamani. Mpaka nilipojaribu kujitoa uhai.”

Nakumbuka kulikuwa na mwembe na kwenye mti huo kulikuwa na chandarua. Mama yangu hakuwepo wakati huo, alikuwa ameenda mtoni kufua nguo na mtoto wangu mdogo.

Nilikuwa peke yangu. Hapo ndipo nilipojaribu kujiua. Kwa sababu sikuwa nala vizuri, nilikuwa dhaifu sana, sikuwa na nguvu. Niliweka kiti, lakini kiti kilianguka na sikufanikiwa kutimiza lengo langu.

Hapo ndipo yule binti yangu aliponiona na kukimbia kumwambia mama yangu kwamba nilikuwa ninaning’inia. Kisha mama yangu akaja kuniokoa. Nadhani nilipoteza fahamu, sikumbuki kilichotokea baada ya hapo.

Nakumbuka tu kwamba niliamka nikiwa kitandani. Binti yangu na mama yangu walikuwa karibu na kitanda. Msichana alisema huku akilia: “Mama, usife, mama, usife.”

Hilo lilikuwa gumu sana kwa sababu nilikuwa na hamu ya kutoroka uhalisia unaonikabili, lakini pia nilitaka kuwa pamoja na watoto wangu. Nilihisi kama nilipaswa kutafuta nguvu ili niweze kusonga mbele na maisha.

Wakati wa kujifungua mambo yalikuwa magumu sana. Siku hiyo nilifika nikiwa na uchungu, waliniambia kuwa njia tayari imeanza kufunguka na kuniingiza kwenye chumba cha upasuaji. Sikuwa tayari kujifungua kwa sababu nilikuwa nimeenda kupangiwa siku ya kufanyiwa upasuaji.

Muda huo daktari alifika akiwa na karatasi na kuniambia nisaini karatasi hiyo, aliniambia kuwa ni lazima nisaini kwa sababu walikuwa wakinifunga mirija ili nisizae tena.

Nilimwambia hapana, kwamba sitaki kusaini, kisha akakasirika sana na kuniambia: “Sawa, usisaini lakini nitakuona hapa baada ya miaka miwili tena kujifungua.”

Nilimsisitiza kuwa sitaki kusaini kwa sababu sikujua inahusu nini, kwa sababu sikuwa nimepewa taarifa kabla. Alitaka nisaini kwa lazima hati hiyo. Alikasirika sana hadi akaanza kunitukana.

Walikuwa wanaenda kunipa dawa ya ganzi na daktari akaniuliza kwa nini nilikuwa nalia. Kisha nikamwambia kuwa mimba hiyo ni matokeo ya kubakwa. Aliniambia: “Tulia na kunipapasa kichwa changu.”

“Baada ya hapo, mtoto wa kike alipozaliwa, muuguzi mmoja aliniambia nimbusu. Nikakataa. Nikamwambia sitaki kumuona, na kwamba amuondoe machoni pangu.”

Kisha wakanihamisha kwenye chumba cha kupona. Wakati ulifika ambapo msichana alipaswa kunyonyeshwa.

Walimleta tena kwangu na kumlaza kwenye kitanda changu ili nimnyonyeshe. Alilia na kulia kwa sababu alikuwa na njaa na sikutaka kumnyonyesha.

Muuguzi alinifokea, na kuniuliza mimi ni mama wa aina gani!, yaani ni mnyama kiasi gani kwa kutotaka kumnyonyesha binti yangu.

“Hawakunikubalia njia mbadala ya kumnyonyesha kwa chupa wakati na mimi naendelea kufikiria kilichokuwa kikitokea.”

Nilikaa hospitalini kwa siku mbili, kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani. Sikurudi kwa jamii yangu kwa sababu tuliondoka nyumbani nikiwa na ujauzito.

Tulihamishwa na vitisho vya kuuawa kutoka kwa wabakaji. Waliniambia kwamba wangeniua, wangeua watoto wangu na familia yangu.

Pia, nyumba yetu iliporwa na kuharibiwa. Na hatukurejea tena huko.

Ubakaji huo ulitokea Novemba 13, 2015. Wabakaji hao walikamatwa mwaka wa 2017 na kupelekwa gerezani kwa miezi 4, na kuachiliwa huru.

Mnamo Juni 2022, kibali cha kuwakamata tena kilitolewa.

Tangu Desemba 2023, mbakaji anatumikia kifungo cha miaka 14 na mshirika wake anatumikia kifungo cha miaka 9.

Hata hivyo, mashirika yanayomwakilisha Fausia yanahofia kwamba upande unaotetea wabakaji hao utakata rufaa siku zijazo ambayo inaweza kubatilisha hukumu hiyo na wakaachiliwa huru.

Miaka minane imepita. Matarajio yangu baada ya niliyopitia, ni serikali kufikiria upya sheria za nchi hii juu ya utoaji wa mimba.

Tunaendelea kuishi katika jamii ambayo imetawaliwa na mfumo dume, utoaji mimba ni mwiko, dunia ambayo dini inawaambia watu kwamba kutoa mimba ni dhambi, ukifanya hivyo unabadilika na kuwa muuaji, kwamba huwezi kupata msamaha wa Mungu.

Natumai mambo yatabadilika kwa sababu niliyopitia yanaweza kutokea kwa mwanamke mwingine yeyote wa Honduras.

Imetafsiriwa na Asha Juma.

Via:BBC



Post a Comment

0 Comments