Afya za watu bilioni 1.8 duniani matatani kwa kutokufanya Mazoezi – WHO

Je wewe ni mtu ambaye unafanya mazoezi? Kama la, ni vema ufahamu kuwa wewe ni sehemu ya watu bilioni 1.8 duniani kote ambao wako hatarini kupata magonjwa kwa sababu tu ya kutofanya mazoezi.

Shirika la Afya ulimwenguni(WHO) kupitia taarifa yake iliyotolewa leo Geneva, Uswisi , linasema idadi hiyo ni sawa na theluthi moja au asilimia 31 ya watu wazima duniani kote kwani kwa utafiti uliofanyika mwaka 2022 watu hao hawakidhi viwango vinavyotakiwa vya kufanya mazoezi.

Idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 5 kati ya mwaka 2010 na 2022.

WHO inapendekeza kuwa watu wazima wanapaswa kuwa na angalau dakika 150 kila wiki za mazoezi ya kawaida au dakika 75 za mazoezi mazito kidogo ya mwili ili kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa kama vile ya moyo, kiharusi, kisukari aina ya II, kusahau, na saratani ya titi na utumbo mpana.

Utafiti huo ulifanywa na watafiti kutoka WHO pamoja na wanazuoni na kuchapishwa katika jarida la kitabibu la Lancet.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus anasema matokeo haya mapya ya utafiti yanaangazia fursa zinazopotea za kupunguza saratani, na magonjwa ya moyo na kuimarisha afya ya akili na mwili kwa kuongeza mazoezi ya mwili.

Amesema ni wakati sasa wakurejelea azma ya kuongeza kiwango cha mazoezi na kupatia kipaumbele hatua za kijasiri ikiwemo kuimarisha sera, ufadhili na kubadili mwelekeo huu unaotia wasiwasi.

Kiwango cha juu cha mazoezi kilibainika kwenye ukanda wa kipato cha juu Asia na Pasifiki, (48%) kisha Asia Kusini (45%) huku viwango vya ukosefu wa mazoezi ya mwili vikianzia asilimia 28 kwenye nchi za kipato cha juu za magharibi hadi asilimia 14 huko Ocenia.

Wanawake kama kawaida hawashiriki zaidi kwenye mazoezi kama ilivyo kwa wanaume.

“Ukosefu wa mazoezi ya mwili ni tishio lililo kimya dhidi ya afya duniani, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye mzigo wa magonjwa sugu,” amesema Dkt. Rüdiger Krech, Mkurugenzi wa WHO Idara ya kuendeleza afya.

Hivyo amesema ni vema kusaka mbinu bunifu za kuhamasisha watu kufanya mazoezi ya mwili kwa kuzingatia umri, mazingira na utamaduni wao, na kuwezesha huduma za mazoezi kufikiwa, ziwe nafuu kwa kila mtu na hivyo kupunguza hatari ya mtu kupata magonjwa kwa kukosa mazoezi.

Soma taarifa nzima hapa.

0 Comments

WEKA COMMENT HAPA..!!!