Shirika la afya duniani WHO limesema limepoteza mawasiliano kabisa na wafanyakazi wa hospitali kubwa ya Gaza ya Al Shifaa huku mashambulio ya Israel yakiendelea karibu na hospitali hiyo iliyozingirwa
Mapigano makali kati ya wanajeshi wa Israel na wapiganaji wa Hamas yamesababisha maelfu ya watu kunasa katika mahospitali ya Gaza,leo Jumapili,huku madaktari na wafanyakazi wa mashirika ya misaada wakionya kwamba wagonjwa watakufa ndani ya mahospitali hayo ikiwa mapigano hayatositishwa.Picha za shirika la habari la AFP zimeonesha namna makombora yanavyovurumishwa dhidi ya mji wa Gaza.Shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka limeonya leo kwamba mahospitali yatageuka kuwa majumba ya kuhifadhi maiti ikiwa vita havitositishwa. Soma pia: Israel yaendelea kuishambulia Gaza angani na ardhini
Mkurugenzi wa hospitali kubwa kabisa,Gaza hii ya Al-Shifah, Mohammad Abu Salmiya amesema hospitali hiyo imezingirwa kila upande na mashambulio ya mabomu yanaendelea katika maeneo ya karibu.
Jeshi la Israel limesema liko tayari kuwahamisha watoto wachanga kutoka hospitali hiyo hii leo.Tayari watoto wachanga wawili wameshakufa na wengine wengi wako hatarini baada, hospitali kuishiwa mafuta wakati mapigano makali yakiendelea kwenye eneo hilo.Na shirika la afya duniani WHO limesema limepoteza mawasiliano na wafanyakazi wa hospitali hiyo ya al Shifaa.