Wanasayansi wasema wanaweza kukata chembechembe za HIV kutoka kwenye seli
Wanasayansi wasema wanaweza kukata chembechembe za HIV kutoka kwenye seli
Wanasayansi wanasema wamefanikiwa kuondoa Virusi vya Ukimwi kutoka kwenye chembechembe zilizoambukizwa, kwa kutumia teknolojia ya uhariri wa jeni ya Crispr iliyoshinda Tuzo ya Nobel.
Inafanya kazi kama mkasi, lakini katika kiwango cha molekuli, hukata DNA ili chembechembe”mbaya” ziweze kuondolewa au kuzimwa.
Matumaini ni hatimaye kuweza kuondoa kabisa virusi mwilini, ingawa kazi nyingi zaidi inahitajika ili kuangalia kama itakuwa salama na yenye ufanisi.
Dawa zilizopo za VVU zinaweza kuzuia virusi lakini sio kuviondoa.
Timu ya Chuo Kikuu cha Amsterdam, ikiwasilisha muhtasari wa matokeo yao ya mapema katika mkutano wa kitabibu wiki hii, inasisitiza kwamba kazi yao inabaki kuwa “uthibitisho wa dhana” tu na haitakuwa tiba ya VVU hivi karibuni.
Na Dk James Dixon, profesa msaidizi wa teknolojia ya seli shina na tiba ya jeni katika Chuo Kikuu cha Nottingham, anakubali, akisema matokeo kamili bado yanahitaji kuchunguzwa.
“Kazi zaidi itahitajika ili kuonesha matokeo katika majaribio haya ya seli yanaweza kutokea katika mwili mzima kwa tiba ya siku zijazo,” alisema.
“Kutakuwa na maendeleo zaidi yanayohitajika kabla ya kuwa na athari kwa wale walio na VVU.”
‘Changamoto kubwa’
Wanasayansi wengine pia wanajaribu kutumia Crispr dhidi ya VVU.
Na Excision BioTherapeutics inasema baada ya wiki 48, watu watatu wa kujitolea wenye VVU hawana madhara makubwa.
Lakini Dk Jonathan Stoye, mtaalamu wa stadi za virusi katika Taasisi ya Francis Crick, huko London, alisema kuondoa VVU kutoka kwenye seli zote ambazo zinaweza kuvihifadhi mwilini ni “changamoto kubwa”.
“Athari zisizolengwa za matibabu, pamoja na athari zinazowezekana za muda mrefu, zinabaki kuwa wasiwasi,” alisema.
“Kwa hivyo inaonekana uwezekano kwamba miaka mingi itapita kabla ya tiba kama hiyo ya Crispr kuwa ya kawaida, hata ikizingatiwa kuwa inaweza kuoneshwa kuwa nzuri.”
Watu wengi walio na VVU wanahitaji matibabu ya muda mrefu ya dawa za kupunguza makali ya VVU. Ikiwa wataacha kutumia dawa hizi, virusi vilivyolala vinaweza kuamka na kusababisha matatizo tena.
Wachache wameonekana kuwa “wameponywa”, baada ya tiba kali ya saratani kufuta baadhi ya seli zao zilizoambukizwa, lakini hii pekee haiwezi kupendekezwa kutibu VVU.
0 Comments
WEKA COMMENT HAPA..!!!