Hii ni notisi ya kwanza rasmi iliyotolewa na WHO baada ya kuthibitisha baadhi ya ripoti hizo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari WHO imeeleza kuwa tahadhari hiyo ni kwa ajili ya makundi matatu ya bidhaa ya Semiglutide hususan kwa chapa ya Ozempic ambayo wameeleza imegundulika huko nchini Brazili mwezi Oktoba 2023, Uingereza na Ireland Kaskazini mwezi Oktoba 2023, na Marekani mwezi Desemba 2023.
Mfumo wa Ufuatiliaji na Uangalizi wa WHO (GSMS) umekuwa ukiangalia ongezeko la ripoti kuhusu bidhaa zisizo halisi (feki) za semaglutide katika maeneo yote ya kijiografia tangu mwaka 2022.
Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO wa Upatikanaji wa Dawa na Bidhaa za Afya Dkt. Yukiko Nakatani
Amewashauri wataalamu wa afya na mamlaka za udhibiti na umma kufahamu kuhusu makundi haya ya dawa zisizo halisi, “Tunatoa wito kwa wadau kuacha matumizi yoyote ya dawa zinazotiliwa shaka na kutoa taarifa kwa mamlaka husika”.
Uhaba wa dawa wachangia bidhaa bandia
Dawa hizi za Semaglutides, pamoja na bidhaa maalum za chapa ambayo si halisi zinatolewa kwa wagonjwa wa kisukari cha aina ya 2 ili kupunguza viwango vyao vya sukari kwenye damu. Semaglutides pia hupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa.
Bidhaa nyingi za semaglutide zinapaswa kudungwa chini ya ngozi kila wiki lakini pia zinapatikana kama vidonge vya kumeza kila siku.
Katika nchi nyingine dawa hizi zimeonesha kupunguza hamu ya kula pamoja na kupunguza viwango vya sukari ya damu, na kwa hivyo zinazidi kuagizwa kwa ajili ya matumizi ya kusaidia kupunguza uzito wa mwili kwa watu.
WHO imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu ongezeko la mahitaji ya dawa hizi pamoja na ripoti kuhusu bidhaa bandia. Bidhaa hizi zisizo halisi zinaweza kuwa na madhara kwa afya ya watu; dawa bandia zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.
Katika hali nyingine, kiungo tendaji ambacho hakijatangazwa kinaweza kuwa kwenye kifaa cha sindano, kama insulini, na kusababisha anuwai isiyotabirika ya hatari za kiafya au shida.
Semaglutides si sehemu ya matibabu yanayopendekezwa na WHO kwa ajili ya udhibiti wa kisukari kutokana na gharama yake kuwa ya juu kwa sasa. Kizuizi cha gharama kinafanya bidhaa hizi kutofaa kama mbinu ya afya ya umma.
Pia, kuna matibabu ya bei nafuu zaidi yanayopatikana kwa ugonjwa wa kisukari, na yana matokeo sawa na yale ya semaglutides kwenye sukari ya damu na hatari ya moyo na mishipa.
Wito kwa watu wote
Ili kujilinda dhidi ya dawa zisizo halisi na madhara yake, wagonjwa wanaotumia bidhaa hizi wanaweza kuchukua hatua kama vile kununua dawa kutoka kwa madaktari walio na leseni na kuepuka kununua dawa kutoka kwa vyanzo visivyojulikana au ambavyo havijathibitishwa.
Watu wanapaswa kuangalia vifungashio na tarehe za mwisho wa matumizi ya dawa wanapozinunua, na watumie bidhaa kama ilivyoelekezwa.
Watumiaji wa semaglutides ya sindano, wanapaswa kuhakikisha kuwa wamehifadhiwa kwenye jokofu.
Iwapo utagundua dawa uliyonunua ni bandia unaweza kuwajulisha WHO kupitia barua pepe rapidalert@who.int.