Uzazi/Ujauzito
Kutokwa na Damu Ukeni Kipindi cha Ujauzito
Kutokwa na damu ukeni wakati wa ujauzito ni hali inayoweza kuwatokea baadhi ya wajawazito. Inaweza kuwa ni matone machache ya damu au kutokwa na damu nyingi. Ingawa wakati mwingine si ishara ya tatizo kubwa,ila mara nyingi ni dalili inayohitaji uchunguzi wa haraka kutoka kwa mtoa huduma wa afya.
Je, ni kawaida kutokwa na damu wakati wa ujauzito?
- Takribani asilimia 15–25 ya wanawake hupata tatizo hili la kutokwa na damu katika miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito.
- Kutokwa na damu hakumaanishi moja kwa moja kwamba ujauzito utaharibika, lakini ni muhimu kuchunguzwa ili kubaini chanzo.
Sababu za kutokwa na damu katika miezi mitatu ya kwanza (First Trimester)
1. Damu inayotokana na kujishikiza kwa mimba (Implantation bleeding)
- Hutokea yai lililorutubishwa linapojishikiza kwenye ukuta wa mji wa mimba.
- Mara nyingi ni matone machache ya damu ya rangi ya pinki au kahawia.
- Hudumu kwa saa chache hadi siku 1–2.
2. Tishio la kuharibika kwa mimba (Threatened miscarriage)
- Hapa Dalili ni kutokwa na damu pamoja na maumivu ya tumbo au mgongo.
- Baadhi ya mimba huendelea salama, lakini nyingine zinaweza kuharibika.
3. Mimba kutunga nje ya mfuko wa uzazi (Ectopic pregnancy)
- Yai lililorutubishwa hukua nje ya mji wa mimba, na mara nyingi hutokea kwenye mirija ya uzazi(Fallopian tubes) ingawa huweza kutokea kwenye maeneo mengine pia.
- Dalili ni:
- Maumivu makali upande mmoja wa tumbo.
- Kutokwa na damu.
- Kizunguzungu au hata kuzimia.
- Hii ni hali ya dharura inayohitaji matibabu ya haraka.
4. Mimba iliyoharibika (Miscarriage)
- Hutokea kwa kutokwa na damu nyingi, maumivu makali ya tumbo na wakati mwingine kutoka kwa mabonge ya damu au tishu.
Sababu za kutokwa na damu baada ya miezi mitatu ya kwanza
1. Kondo la nyuma kushuka chini (Placenta previa)
- Kondo la nyuma hufunika sehemu au mlango wa kizazi.
- Dalili kuu ni kutokwa na damu nyekundu bila maumivu.
- Inaweza kuhitaji uangalizi maalumu au upasuaji wa kujifungua.
2. Kondo la nyuma kujitenga mapema (Placental abruption)
- Kondo la nyuma hujitenga na ukuta wa mji wa mimba kabla ya kujifungua.
- Dalili:
- Kutokwa na damu.
- Maumivu makali ya tumbo.
- Tumbo kuwa gumu au kukaza zaidi.
- Ni dharura inayoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.
3. Uchungu wa kujifungua mapema
- Kutokwa na damu kunaweza kuambatana na mikazo ya mara kwa mara na maumivu ya mgongo.
4. Mabadiliko kwenye shingo ya kizazi
- Wakati wa ujauzito, shingo ya kizazi huwa na mishipa mingi ya damu.
- Baada ya tendo la ndoa au uchunguzi wa daktari, damu kidogo inaweza kutoka.
Dalili zinazohitaji kuwahi hospitali mara moja
Nenda hospitali haraka ikiwa:
- Unatokwa na damu nyingi.
- Una maumivu makali ya tumbo.
- Unazimia au unahisi kizunguzungu kikali.
- Damu ina mabonge makubwa au tishu.
- Mtoto ameacha kucheza (kwa ujauzito mkubwa).
- Unavuja damu pamoja na maji kutoka ukeni.
- Una homa au harufu mbaya kutoka ukeni.
Daktari anaweza kufanya vipimo gani?
- Ultrasound kuangalia hali ya ujauzito.
- Vipimo vya damu.
- Kupima mapigo ya moyo ya mtoto.
- Uchunguzi wa shingo ya kizazi pale inapofaa.
Unapaswa kufanya nini ukiona damu?
- Tulia na uwasiliane na kituo cha afya haraka au Mtoa huduma wa afya.
- Tumia pedi kufuatilia kiasi cha damu.
- Usiingize kitu chochote ukeni bila ushauri wa daktari.
- Epuka kujitibu mwenyewe.
- Fuata maelekezo ya mtoa huduma wa afya.
Tahadhari:
Kutokwa na damu wakati wa ujauzito si jambo la kupuuzwa. Wakati mwingine inaweza kuwa hali isiyo na madhara makubwa, lakini pia inaweza kuwa ishara ya tatizo linalohitaji matibabu ya haraka. Uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kulinda afya ya mama na mtoto.
Kwa Ushauri Zaidi,Elimu na Tiba tuwasiliane +255758286584.
References:
- World Health Organization (WHO): https://www.who.int/news-room/fact-sheets/detail/maternal-mortality
- American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG) – Bleeding During Pregnancy: https://www.acog.org/womens-health/faqs/bleeding-during-pregnancy
- NHS – Bleeding in Pregnancy: https://www.nhs.uk/pregnancy/related-conditions/common-symptoms/bleeding/
- MSD Manual Consumer Version – Vaginal Bleeding During Pregnancy: https://www.msdmanuals.com/home/women-s-health-issues/complications-of-pregnancy/vaginal-bleeding-during-pregnancy

