magonjwa ya wanawake
Kutokwa na Hedhi nyingi si Jambo la Kawaida
Kutokwa na Hedhi nyingi si Jambo la Kawaida: Wataalamu Wasema Hali Hii Imekuwa Ikipuuzwa kwa Miaka Mingi
Kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi (Heavy Menstrual Bleeding – HMB) ni tatizo la kiafya linalowakumba mamilioni ya wanawake duniani, lakini kwa muda mrefu limekuwa likichukuliwa kama sehemu ya kawaida ya maisha ya mwanamke. Sasa tafiti zinaonyesha kuwa hali hiyo inaweza kuwa ishara ya magonjwa mengine makubwa na kusababisha madhara makubwa kiafya, kijamii na kiuchumi.
Wataalamu wa afya wanasema wanawake wengi huishi kwa miaka mingi wakiamini kuwa maumivu makali na kutokwa na damu nyingi ni jambo la kawaida, hali inayochelewesha utambuzi na matibabu.
Tatizo linaathiri wanawake wengi
Makadirio ya tafiti mbalimbali yanaonyesha kuwa kati ya asilimia 10 hadi 30 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa hupata hedhi nzito au hupata tatizo la kuvuja damu nyingi wakati wa hedhi. Hata hivyo, baadhi ya tafiti zinaonyesha idadi hiyo inaweza kufikia karibu nusu ya wanawake wote kutokana na wengi kutoripoti dalili zao au kutofahamu kuwa wanachokipitia si cha kawaida.
Madaktari wanaeleza kuwa kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi kunamaanisha kiwango cha damu kinachozidi mililita 80 kwa mzunguko mmoja wa hedhi, hedhi inayodumu zaidi ya siku saba, au kutokwa na mabonge makubwa ya damu. Lakini katika mazingira halisi, utambuzi mara nyingi hutegemea ikiwa hedhi hiyo inaathiri maisha ya kila siku ya mwanamke.
Dalili zinazoweza kuashiria hedhi nzito
Wanawake wanaopata hedhi nzito wanaweza kuwa na dalili kama:
- Kulazimika kubadilisha pedi kila baada ya muda mfupi.
- Kutokwa na damu hadi kuchafua nguo au mashuka.
- Kutokwa na mabonge makubwa ya damu.
- Hedhi kudumu zaidi ya siku saba.
- Maumivu makali ya tumbo.
- Uchovu usioelezeka.
- Kizunguzungu na kupungukiwa nguvu.
Athari kwa afya
Wataalamu wanaonya kuwa kutokwa na damu nyingi kunaweza kusababisha upungufu wa madini ya chuma mwilini (iron deficiency), hali ambayo baadaye inaweza kuendelea na kuwa upungufu wa damu (anaemia).
Dalili za upungufu wa madini ya chuma ni pamoja na:
- Uchovu wa kudumu.
- Kizunguzungu.
- Kupumua kwa shida.
- Ngozi kuwa dhaifu.
- Nywele kunyonyoka.
- Kushindwa kuzingatia vizuri(focus loose).
- Kuhisi baridi mara kwa mara.
Tafiti zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya wanawake wenye hedhi nzito pia huwa na upungufu wa madini ya chuma.
Huenda ikawa ishara ya ugonjwa mwingine
Madaktari wanasema hedhi nzito au kutokwa na damu nyingi ya Hedhi(Heavy Menstrual bleeding) mara nyingi si ugonjwa wenyewe bali ni dalili ya tatizo jingine la kiafya, ikiwemo:
- Uvimbe kwenye mfuko wa uzazi (fibroids).
- Endometriosis.
- Adenomyosis.
- Saratani za mfumo wa uzazi.
- Matatizo ya homoni.
- Matatizo ya kuganda kwa damu.
- Polipu kwenye mfuko wa uzazi.
Kwa wasichana wanaoanza hedhi na wanawake wanaokaribia kukoma hedhi, mabadiliko ya homoni yanaweza pia kuchangia kutokwa na damu nyingi.
Madhara kwa maisha ya kila siku
Mbali na afya, hedhi nzito huathiri elimu, ajira na maisha ya kijamii.
Baadhi ya wanawake hulazimika kukosa shule au kazi kutokana na maumivu na kutokwa na damu nyingi. Wengine huishi kwa hofu ya kuchafua nguo hadharani, jambo linalopunguza kujiamini na kushiriki shughuli mbalimbali.
Nchini Uingereza, tafiti zinaonyesha wasichana wenye hedhi nzito hukosa wastani wa siku tisa za masomo kila mwaka kutokana na tatizo hilo.
Kwa wanawake wanaofanya kazi, hedhi nzito inaweza kusababisha kupungua kwa uzalishaji na kukosa siku nyingi za kazi, jambo linaloathiri pia uchumi.
Kwa nini wanawake wengi hawapati matibabu mapema?
Sababu kadhaa huchangia:
- Kuamini kuwa maumivu makali ni sehemu ya kawaida ya hedhi.
- Aibu ya kuzungumzia hedhi.
- Kukosekana kwa elimu kuhusu kiwango cha damu kinachochukuliwa kuwa cha kawaida.
- Wahudumu wa afya kutouliza maswali ya kina kuhusu hedhi.
Matokeo yake, baadhi ya wanawake hukaa kwa miaka mingi kabla ya kupata utambuzi sahihi.
Matibabu yanapatikana
Aina ya matibabu hutegemea chanzo cha tatizo.
Madaktari wanaweza kupendekeza:
- Dawa za kupunguza maumivu.
- Dawa za kudhibiti homoni.
- Dawa za kupunguza damu wakati wa hedhi.
- Upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye mfuko wa uzazi.n.k
Je,Unachangamoto hii? Kwa Ushauri Zaidi&Tiba tuwasiliane +255758286584.
Utafiti mpya unalenga kuboresha huduma
Wanasayansi duniani sasa wanawekeza zaidi katika kuelewa chanzo cha hedhi kutoka nyingi sana na kuboresha utambuzi wake.
Mradi wa kimataifa unaoitwa The Missed Vital Sign, unaongozwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Edinburgh, unalenga kupunguza muda wa kusubiri utambuzi wa tatizo hili kutoka wastani wa miaka mitano hadi miezi mitano.
Watafiti wanachunguza mbinu mpya kama:
- Kutafuta alama za kibaolojia (biomarkers) kwenye damu ya hedhi.
- Kutengeneza pedi zenye vihisi (smart sensors) vinavyoweza kupima kiwango cha damu.
- Kutumia simu janja na vifaa vinavyovaliwa mwilini kutambua hatari ya upungufu wa madini ya chuma.
Uzoefu wa wagonjwa
Michelle Alston kutoka Marekani alieleza kuwa alianza kupata hedhi nyingi tangu akiwa na umri wa miaka 12, lakini aliambiwa kuwa hali hiyo ni ya kawaida. Baada ya karibu miaka 30 ndipo aligundulika kuwa alikuwa na uvimbe mkubwa kwenye mfuko wa uzazi (fibroids) na huenda pia alikuwa na endometriosis. Hatimaye alifanyiwa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi na tatizo lake likatatuliwa.
Mtafiti Emily Young, ambaye pia aliwahi kukumbwa na tatizo hili la hedhi kutoka nyingi sana, anasema wanawake wengi hulazimika kubadilisha maisha yao yote kulingana na siku zao za hedhi kutokana na hofu ya kutokwa na damu nyingi na maumivu makali.
Facts Check:
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa hedhi kutoka nyingi haipaswi kuonekana kama jambo la kawaida. Ikiwa mwanamke anatokwa na damu nyingi kiasi cha kuathiri maisha yake ya kila siku, hupata uchovu usioisha au hedhi hudumu zaidi ya siku saba, anapaswa kuongea na Wataalam wa afya Mapema au kufika hospitali kwa uchunguzi mapema.
Utambuzi na matibabu ya mapema yanaweza kuzuia madhara makubwa kama upungufu wa damu,kugundua magonjwa mengine yanayosababisha tatizo hilo,n.k…
References:
- BBC Future: “It’s not just an inconvenience”: We’ve underestimated the health impacts of heavy periods (24 Julai 2026).
- American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG): Heavy Menstrual Bleeding.
- World Health Organization (WHO): Endometriosis.
- International Journal of Gynecology & Obstetrics.
- The Lancet: Tafiti kuhusu upungufu wa damu na afya ya wanawake.


