Connect with us

magonjwa

Ini kuvimba,kutanuka au kuongezeka Ukubwa,Dalili na chanzo

Doctor Ombeni

Published

on

đŸ©ș
Medically reviewed by Afyaclass Teams, Written by Dr.Ombeni

Ini kuvimba,kutanuka au kuongezeka Ukubwa,ni tatizo ambalo kitaalamu huitwa hepatomegaly, ni hali ambapo Ini linakuwa kubwa kuliko ukubwa unaotarajiwa. Hali hii yenyewe si ugonjwa, bali mara nyingi ni ishara ya tatizo jingine linaloathiri ini au mwili kwa ujumla.

Ini kuongezeka ukubwa au kutanuka au kuvimba kunaweza kusababishwa na magonjwa mbalimbali, yakiwemo magonjwa ya Ini, matatizo ya moyo, baadhi ya maambukizi,saratani n.k. Wakati mwingine mtu anaweza kuwa na tatizo la Ini kuongezeka Ukubwa bila kupata dalili yoyote.

Dalili za Ini kuongezeka Ukubwa

Dalili hutegemea chanzo na ukubwa wa tatizo. Mtu mwingine anaweza asiwe na dalili kabisa, huku mwingine akiwa na dalili mbalimbali.

1. Maumivu au usumbufu upande wa juu kulia wa tumbo

Ini linapatikana zaidi upande wa juu kulia wa tumbo, chini ya mbavu. Linapoongezeka, mtu anaweza kuhisi;

  • maumivu,
  • hali ya uzito,
  • au kubana katika eneo hilo.

2. Tumbo kuhisi kujaa au kubana

Mtu anaweza kuhisi kama tumbo limejaa au kuna kitu kinachobana upande wa juu wa tumbo. Hii inaweza kuonekana zaidi pale Ini linapokuwa limeongezeka kwa kiasi kikubwa.

3. Uchovu na kukosa nguvu

Uchovu unaweza kuonekana kwa watu wenye magonjwa mbalimbali ya ini. Hata hivyo, uchovu pekee hauwezi kuthibitisha kuwa mtu ana tatizo la ini kutanuka au kuongezeka ukubwa, kwa sababu hali hii inaweza kusababishwa na matatizo mengine mengi ya kiafya.

4. Kichefuchefu na kutapika

Baadhi ya magonjwa yanayosababisha ini kuongezeka ukubwa yanaweza kuambatana na kichefuchefu, kutapika au kutopenda chakula. Hivo kichefuchefu na kutapika ni miongoni mwa dalili zinazoweza kuonekana ikiwa ini limetanuka au kuongezeka ukubwa kutokana na Ugonjwa wa ini.

5. Kupungua hamu ya kula

Mtu anaweza kuanza kutopenda chakula kama kawaida. Ikiwa hali hii inaendelea kwa muda na kuambatana na kupungua uzito, inapaswa kuchunguzwa na mtaalamu wa afya.

6. Macho na ngozi kuwa njano

Hii huitwa jaundice. Macho au ngozi kuwa njano inaweza kutokea wakati bilirubin inapoongezeka mwilini kutokana na matatizo ya ini au njia ya nyongo. Jaundice ni dalili muhimu inayohitaji uchunguzi wa kitabibu.

7. Mkojo kuwa mweusi

Katika baadhi ya magonjwa ya ini, mkojo unaweza kuwa na rangi nyeusi au kahawia. Dalili hii inaweza kuonekana pamoja na macho au ngozi kuwa njano.

8. Kinyesi kuwa na rangi tofauti na rangi yake

Baadhi ya matatizo ya ini au njia ya nyongo yanaweza kufanya kinyesi kuwa na rangi nyingine kuliko kawaida. Kinyesi chepesi kikifuatana na jaundice au mkojo mweusi kinapaswa kuchunguzwa.

9. Kuwashwa kwa ngozi

Baadhi ya magonjwa ya ini, hasa yale yanayoathiri mtiririko wa nyongo, yanaweza kusababisha muwasho wa ngozi. Muwasho unaweza kutokea hata bila kuwa na upele unaoonekana.

10. Kupungua uzito bila Sababu

Kupungua uzito bila kubadilisha chakula au mazoezi kunaweza kuonekana katika baadhi ya magonjwa makubwa yanayoathiri ini. Hata hivyo, kupungua uzito kunaweza kuwa na sababu nyingi nyingine, hivyo si ushahidi wa moja kwa moja wa ini kuongezeka ukubwa.

11. Tumbo kuvimba kutokana na maji

Katika baadhi ya magonjwa makubwa ya ini, maji yanaweza kukusanyika tumboni. Hali hii huitwa ascites na inaweza kufanya tumbo lionekane limevimba.

12. Miguu au vifundo vya miguu kuvimba

Ugonjwa wa Ini pia unaweza kuathiri usawa wa maji na protini mwilini na kusababisha kuvimba kwa miguu au vifundo vya miguu.

Ni nini husababisha Ini kuongezeka ukubwa?

Kuna sababu nyingi zinazoweza kufanya ini liongezeke ukubwa. Mayo Clinic inagawanya sababu hizo kama magonjwa ya ini, saratani pamoja na matatizo ya moyo na mishipa ya damu.

(i) Magonjwa ya ini

Ini linaweza kuongezeka kutokana na matatizo kama vile:

  • Ugonjwa wa homa ya Ini-Hepatitis A, B au C
  • Tatizo la Cirrhosis
  • Mafuta mengi kwenye ini, yanayojulikana sasa kama metabolic dysfunction-associated steatotic liver disease (MASLD)
  • Ugonjwa wa ini unaohusiana na matumizi ya pombe
  • Hemochromatosis, ambapo madini ya chuma hujikusanya mwilini
  • Wilson’s disease, ambapo shaba hujikusanya mwilini
  • Baadhi ya magonjwa ya kurithi
  • Vivimbe maji kwenye Ini(Liver Cysts)
  • Uvimbe usio wa saratani kwenye ini
  • Kuziba kwa njia ya nyongo
  • Toxic hepatitis, yaani kuharibika kwa ini kutokana na baadhi ya dawa,Sumu au kemikali.

(ii) Maambukizi

Baadhi ya maambukizi yanaweza kuathiri ini na kusababisha liwe kubwa. Haya yanaweza kuwa maambukizi ya virusi, bakteria au vimelea vingine kulingana na ugonjwa husika.

Maambukizi ya Virusi, hasa hepatitis B na C, ni miongoni mwa sababu muhimu za ugonjwa wa ini duniani.

(iii) Matatizo ya moyo

Ini kuongezeka si tatizo linalotokana na ini pekee. Tatizo la Moyo kushindwa kufanya kazi(Heart failure), kwa mfano, inaweza kusababisha damu kurudi nyuma kwenye mishipa inayohusiana na ini na kusababisha ini kujaa damu na kuongezeka ukubwa.

Pia kwa mujibu wa Mayo Clinic, inataja matatizo kama Budd-Chiari syndrome, ambapo mishipa inayotoa damu kutoka kwenye ini huziba, kama sababu nyingine inayoweza kuhusishwa na ini kuongezeka ukubwa.

(iv) Saratani

Saratani inaweza kusababisha ini kuongezeka, hasa ikiwa saratani imeanzia kwenye ini au imesambaa kutoka sehemu nyingine ya mwili kwenda kwenye ini.

Fahamu, saratani ya ini, leukemia, lymphoma na saratani kutoka sehemu nyingine za mwili zinazosambaa hadi kwenye ini ni miongoni mwa sababu zinazowezekana kuchangia tatizo hili la Ini kutanuka au kuongezeka Ukubwa.

Nani yuko katika hatari zaidi?

Hatari inaweza kuongezeka kwa mtu mwenye sababu zinazoweza kuharibu ini. Miongoni mwa sababu hizo ni matumizi makubwa ya pombe, uzito mkubwa, lishe isiyo bora, maambukizi ya hepatitis, matumizi yasiyo sahihi ya dawa na baadhi ya virutubisho au dawa za mitishamba.

NB:Kutumia dozi kubwa kuliko inavyopendekezwa kwenye baadhi ya dawa, vitamini au supplements kunaweza kuongeza hatari ya kuharibika kwa ini. Baadhi ya bidhaa za mitishamba pia zinaweza kuhusishwa na madhara kwenye ini.

Je, Ini kuongezeka Ukubwa ni sawa na mafuta kwenye ini?

Hapana. Ini kuongezeka ukubwa au kutanuka ni hali ya ini kuwa kubwa kuliko kawaida, wakati mafuta kwenye ini ni hali ambapo mafuta yanajikusanya ndani ya seli za ini.

Hata hivyo, mafuta kwenye ini yanaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazofanya ini liongezeke ukubwa.

Ini kuongezeka ukubwa hugunduliwaje?

Daktari anaweza kuanza kwa kumuuliza mgonjwa kuhusu dalili, historia ya afya, matumizi ya pombe, dawa na sababu nyingine zinazoweza kuathiri ini.

Anaweza pia kulipapasa tumbo wakati wa uchunguzi wa mwili ili kuona kama ini linaonekana kuwa kubwa.

Vipimo vinavyoweza kutumika kutafuta sababu ni pamoja na;

  • vipimo vya damu vya ini,
  • vipimo vya Homa ya Ini(hepatitis)
  • na vipimo vya picha kama ultrasound, CT scan au MRI.
  • Katika baadhi ya mazingira, daktari anaweza kuhitaji vipimo vingine zaidi, ikiwemo liver biopsy, kulingana na kinachoshukiwa.

Je, ini kuongezeka ukubwa linaweza kupona?

Hii inategemea chanzo. Kwa sababu hepatomegaly ni ishara ya tatizo jingine, matibabu hulenga kutambua na kutibu chanzo chake.

Kwa mfano, kama tatizo linatokana na hepatitis, mafuta kwenye ini, matumizi ya pombe, dawa fulani, tatizo la moyo au ugonjwa mwingine, matibabu yatategemea hali hiyo.

Kwa hiyo, si sahihi kutumia dawa za “kusafisha ini” bila kujua sababu ya ini kuongezeka.

Jinsi ya kupunguza hatari ya magonjwa ya ini

Zipo hatua kadhaa za kusaidia kulinda afya ya ini. Hatua Hizo ni pamoja na kula lishe yenye uwiano mzuri, kudhibiti tatizo la Uzito Mkubwa, kutumia dawa kwa kufuata maelekezo, kuepuka matumizi makubwa ya pombe na kutumia virutubisho au dawa za mitishamba kwa tahadhari.

Ni muhimu pia kuchukua tahadhari dhidi ya hepatitis, hasa kwa kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu chanjo pale inapopatikana, uchunguzi na kinga dhidi ya maambukizi.

Wakati gani unapaswa kumuona daktari?

Ikiwa una maumivu au usumbufu unaoendelea upande wa juu kulia wa tumbo, uchovu usioelezeka, kichefuchefu kinachoendelea, kupungua uzito bila sababu, macho au ngozi kuwa njano, mkojo kuwa mweusi, kinyesi kuwa na rangi isiyoyakawaida au tumbo kuvimba, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.

Muhimu zaidi, usiweke hitimisho kwamba Una tatizo la Ini kutanuka au kuongezeka Ukubwa kwa kuangalia dalili pekee. Vipimo vya kitabibu ndivyo vinavyoweza kusaidia kuthibitisha kama ini limeongezeka na kutafuta sababu yake.

Facts Check:

Ini kuongezeka ukubwa, au hepatomegaly, ni ishara inayoweza kutokana na sababu nyingi, kuanzia magonjwa ya ini kama hepatitis na mafuta kwenye ini hadi matatizo ya moyo, maambukizi na baadhi ya saratani.

Jambo muhimu ni kwamba ini kuongezeka ukubwa si ugonjwa unaopaswa kutibiwa kwa dawa moja maalumu bila kujua chanzo. Mtu mwenye dalili zinazotia wasiwasi anapaswa kufanyiwa uchunguzi ili kubaini chanzo na kupata matibabu yanayofaa.

References:

  1. Mayo Clinic – Enlarged liver (Hepatomegaly): Symptoms & Causes
    Mayo Clinic
  2. Cleveland Clinic – Hepatomegaly (Enlarged Liver)
  3. Johns Hopkins Medicine – Common Characteristics of Liver Disease
  4. NHS – Liver Diseases

🏆Certified| Doctor from Afyaclass.Hapa utapata Ushauri & Tiba juu ya magonjwa mbali mbali. Kwa msaada Zaidi Tuwasiliane kupitia namba: +255758286584.Pata dondoo za afya kila siku kwa kufuatilia kupitia: @Facebook | @Instagram | @YouTube.