Ebola
Mlipuko wa Ebola DRC wazidi kushika kasi, WHO yataka hatua za haraka kuzuia maambukizi
Kinshasa, DRC – 1 Agosti 2026: Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo (Bundibugyo virus disease – BVD) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unaendelea kuongezeka kwa kasi huku ukisambaa katika maeneo mapya, hali inayoongeza hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa WHO, hadi 30 Julai 2026, DRC ilikuwa imerekodi wagonjwa 3,605 waliothibitishwa maabara, huku watu 1,587 wakifariki dunia, sawa na kiwango cha vifo cha asilimia 44. Wagonjwa 651 walikuwa wamepona.
Mlipuko mkubwa zaidi kuwahi kurekodiwa DRC
WHO imesema huu sasa ndiyo mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola kuwahi kutokea nchini DRC, ukiupita mlipuko wa mwaka 2018–2020, ambao ulisababisha wagonjwa 3,317 waliothibitishwa.
Katika wiki ya 30 ya ufuatiliaji wa ugonjwa huo, mamlaka zilirekodi wagonjwa wapya 567 na vifo 296, idadi kubwa zaidi kuwahi kuripotiwa ndani ya wiki moja tangu mlipuko huo uanze.

Maambukizi yasambaa hadi mikoa mitano
Mwanzoni mlipuko ulikuwa umejikita katika eneo la afya la Mongbwalu mkoani Ituri, lakini sasa umesambaa katika majimbo matano ambayo ni:
- Ituri
- North Kivu
- South Kivu
- Haut-Uélé
- Tshopo
Kwa sasa jumla ya maeneo 49 ya afya (health zones) yameathirika, huku 33 kati yake yakiendelea kuripoti wagonjwa wapya ndani ya siku saba zilizopita.
Mkoa wa Ituri bado unaongoza kwa kuwa na asilimia 88 ya wagonjwa wote na zaidi ya asilimia 82 ya vifo vyote vilivyoripotiwa nchini humo.
Wahudumu wa afya nao waathirika
WHO imeeleza kuwa wahudumu wa afya wanaendelea kuambukizwa kutokana na kazi zao.
Hadi sasa:
- Wahudumu wa afya 151 wameambukizwa.
- 44 wamefariki dunia.
- 68 wamepona.
Hali hiyo inaonyesha changamoto zinazoendelea katika kudhibiti maambukizi ndani ya vituo vya kutolea huduma za afya na kulinda wafanyakazi wa sekta hiyo.
Changamoto zinazochochea kuenea kwa Ebola
WHO imebainisha sababu kadhaa zinazofanya mlipuko huu kuwa mgumu kudhibiti, ikiwemo:
- Mapigano na ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo.
- Wananchi kuhama makazi kutokana na migogoro.
- Usafiri wa mara kwa mara kati ya DRC na nchi jirani.
- Upatikanaji mdogo wa huduma za afya.
- Msongamano katika makambi ya wakimbizi wa ndani.
Changamoto hizo zimekuwa zikikwamisha timu za afya kufikia maeneo yaliyoathirika na kufanya ufuatiliaji wa wagonjwa pamoja na watu waliokutana nao.
Maelfu ya watu wanafuatiliwa
Mamlaka za afya zimewatambua watu 17,863 waliokutana na wagonjwa wa Ebola na wanaendelea kuwafuatilia kwa kipindi cha siku 21 ili kubaini kama wataonyesha dalili za ugonjwa huo.
WHO imesema hatua hii ni muhimu ili kukatiza mnyororo wa maambukizi mapema.
Dalili za Ebola ya Bundibugyo
Virusi vya Bundibugyo ni aina ya virusi vya Ebola vinavyoaminika kuanzia kwa wanyama, hasa popo wanaokula matunda, kabla ya kusambaa kwa binadamu kupitia kugusana na damu au majimaji ya mwili wa aliyeambukizwa.
Dalili za awali ni pamoja na:
- Homa kali
- Uchovu mkubwa
- Maumivu ya misuli
- Maumivu ya kichwa
- Koo kuuma
Baadaye mgonjwa anaweza kupata:
- Kutapika
- Kuharisha
- Kushindwa kufanya kazi kwa baadhi ya viungo vya mwili
- Kutokwa damu katika baadhi ya wagonjwa.
Kipindi cha kuibuka kwa dalili ni kati ya siku 2 hadi 21.
#Soma Zaidi hapa kuhusu Ugonjwa wa Ebola,Dalili zake,jinsi unasambaa
Hakuna chanjo wala tiba maalumu iliyoidhinishwa
WHO imeeleza kuwa hadi sasa hakuna chanjo au tiba maalumu iliyoidhinishwa dhidi ya Ebola ya Bundibugyo.
Udhibiti wa mlipuko unategemea:
- Kugundua wagonjwa mapema.
- Kuwatenga na kuwapatia huduma za matibabu.
- Kufuatilia waliokutana nao.
- Mazishi salama.
- Ushirikiano wa jamii.
Wataalamu wa WHO wanaendelea kutathmini chanjo na dawa zinazoweza kutumika dhidi ya aina hii ya Ebola.
Uganda yatangaza mwisho wa mlipuko wake
Habari njema ni kwamba Uganda ilitangaza rasmi tarehe 28 Julai 2026 kumalizika kwa mlipuko wake wa Ebola ya Bundibugyo baada ya kupita siku 42 bila kurekodi maambukizi mapya ya ndani ya nchi.
Hata hivyo WHO imeonya kuwa Uganda bado ipo kwenye hatari ya kupata wagonjwa wapya kutokana na maambukizi yanayoendelea nchini DRC.
Aidha, mgonjwa mmoja aliyekuwa amesafiri kutoka DRC kwenda Ufaransa alipona kabisa na hakukuwa na maambukizi ya watu wengine waliokutana naye.
WHO yatathmini hatari kuwa kubwa
WHO imeendelea kutathmini hatari ya mlipuko huu kuwa:
- Kubwa sana (Very High) ndani ya DRC.
- Kubwa (High) nchini Uganda na nchi zinazopakana na DRC.
- Ndogo (Low) kwa nchi nyingine za Afrika na duniani kwa ujumla.
Pamoja na hali hiyo, WHO haijapendekeza kuwekwa kwa vizuizi vya safari au biashara dhidi ya nchi zilizoathirika, bali imezitaka nchi zote kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa, maandalizi ya kukabiliana na mlipuko na ushirikiano wa kuvuka mipaka.
