magonjwa ya wanaume
Madhara ya UTI kwa mwanaume,Athari 8 zinazoweza kutokea
Madhara Ya Uti Kwa Mwanaume: Athari 8 zinazoweza kutokea na namna ya kuziepuka
Maambukizi ya njia ya mkojo, yanayojulikana kama UTI (Urinary Tract Infection), ni maambukizi yanayoweza kuathiri sehemu mbalimbali za mfumo wa mkojo, ikiwemo mrija wa mkojo (urethra), kibofu cha mkojo (bladder), tezi dume (prostate) na figo (kidneys).
UTI inaweza kutokea kwa wanaume wa rika mbalimbali. Ingawa maambukizi mengi yanaweza kutibika yakigunduliwa mapema na kutibiwa ipasavyo, UTI isiyotibiwa au inayotibiwa bila kufuata utaratibu sahihi inaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.
Kwa mwanaume, ni muhimu kuchunguza UTI mapema kwa sababu wakati mwingine maambukizi yanaweza kuhusishwa na matatizo ya tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo au madhara mengine makubwa ya kiafya.

Madhara Ya Uti Kwa Mwanaume
Kwa mujibu wa taarifa za afya kutoka National Institutes of Health (NIH), NHS na Centers for Disease Control and Prevention (CDC), yafuatayo ni baadhi ya madhara yanayoweza kutokea kutokana na Ugonjwa wa UTI kwa mwanaume.
1. Maambukizi ya figo (Kidney Infection)
Maambukizi haya ya Figo ni mojawapo ya matatizo makubwa yanayoweza kutokea pale bakteria wanaosababisha UTI wanaposambaa kutoka sehemu za chini za mfumo wa mkojo na kupanda hadi kwenye figo.
Chat Nasi Whatsapp
"Ungana na Wasomaji zaidi ya 12,000 wanaopata huduma ndani ya afyaclass, Kama unachangamoto yoyote ya kiafya; Kwa Ushauri&Tiba tuwasiliane hapa kupitia WhatsApp, Kama huna Whatsapp tuma SMS au Piga +255758286584."
Chat WhatSapp HapaKwa kawaida, maambukizi yanaweza kuanzia kwenye mrija wa mkojo(Urethra) au kibofu cha Mkojo(Urinary Bladder) na kupanda kupitia njia ya mkojo(Ureter) hadi kwenye figo.
Dalili za maambukizi ya figo
Mwanaume anaweza kupata dalili zifuatazo:
- Maumivu ya mgongo Kwa Sehemu ya chini au ubavuni, hasa sehemu iliyo karibu na mbavu.
- Homa na hali ya kutetemeka kwa baridi.
- Kichefuchefu au kutapika.
- Maumivu au kuhisi hali ya kuungua wakati wa kukojoa.
- Kukojoa mara nyingi kuliko kawaida.
- Kujisikia Uchovu sana na mwili kuwa dhaifu.
Madhara yake ni yapi?
Maambukizi ya figo yakichelewa kutibiwa yanaweza kuharibu tishu za figo na, katika hali mbaya zaidi, kusababisha kupungua kwa uwezo wa figo kufanya kazi.
Muhimu: Mwanaume mwenye dalili za UTI zinazoambatana na homa au maumivu ya ubavu anapaswa kupata uchunguzi wa haraka hospitalini au kwa Ushauri zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584.
2. Kuvimba kwa tezi dume (Prostatitis)
Tezi dume ni kiungo cha mfumo wa uzazi wa mwanaume kilichopo chini ya kibofu cha mkojo. Tezi hii huzunguka sehemu ya mwanzo ya mrija wa mkojo.
Maambukizi ya bakteria kwenye mfumo wa mkojo yanaweza kuhusishwa na kuvimba kwa tezi dume, hali inayojulikana kama prostatitis.
Dalili za prostatitis
Mwanaume anaweza kupata:
- Maumivu wakati wa kukojoa.
- Kukojoa mara kwa mara au kuhisi haja ya kukojoa kwa haraka.
- Ugumu wa kuanza kukojoa.
- Maumivu sehemu ya chini ya tumbo.
- Maumivu kwenye eneo la kati ya korodani na njia ya haja kubwa.
- Maumivu kwenye uume au korodani.
- Maumivu wakati wa kumwaga shahawa.
- Homa na kutetemeka, hasa maambukizi yanapokuwa makali.
Madhara yake ni yapi?
Ikiwa hali ya kuvimba kwa tezi dume(prostatitis) kutokana na maambukizi ya bakteria haitatibiwa vizuri, inaweza kusababisha:
- Kushindwa kutoa mkojo kabisa.
- Kujikusanya kwa usaha ndani ya tezi dume, hali inayoitwa prostatic abscess.
- Maumivu yanayoendelea au kurudia rudia.
- Matatizo ya Kiutendaji kwenye tendo la ndoa kwa baadhi ya wagonjwa.
- Na katika hali mbaya zaidi Maambukizi haya yanaweza kusambaa kwenye damu.
Si kila mwanaume mwenye UTI atapata prostatitis, lakini dalili zinazofanana na hizo zinahitaji uchunguzi wa kitabibu.
3. Kushindwa kukojoa (Urinary Retention)
UTI inaweza kuambatana na hali ya uvimbe au maumivu yanayofanya kukojoa kuwa kugumu. Tatizo hili linaweza kuwa kubwa zaidi ikiwa mwanaume ana tatizo la tezi dume iliyoongezeka ukubwa au kuziba kwa njia ya mkojo.
Kushindwa kutoa mkojo kabisa kunaitwa acute urinary retention na ni hali inayohitaji matibabu ya dharura.
Dalili za tatizo hili
- Kuhisi kibofu kimejaa lakini mkojo hautoki.
- Kupata maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo.
- Kukojoa matone matone.
- Kutumia nguvu nyingi kujaribu kutoa mkojo.
- Kuhisi kwamba kibofu hakijaisha mkojo baada ya kukojoa.
Kwa nini ni hatari?
Mkojo unaposhindwa kutoka, unaweza kujikusanya kwenye kibofu na kusababisha maumivu makali pamoja na kutengeneza mazingira ya bacteria kuzaliana zaidi. Tatizo likidumu au kuhusishwa na kuziba kwa njia ya mkojo, au maambukizi ya bacteria kupanda kutoka sehemu za chini za mfumo wa mkojo kwenda juu linaweza kuathiri mpaka figo.
Ikiwa mwanaume hawezi kukojoa kabisa, anapaswa kwenda hospitalini mara moja. Asisubiri UTI ipone yenyewe. Au kwa Ushauri zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584.
4. Maambukizi kusambaa kwenye damu (Sepsis)
Sepsis tunazungumzia maambukizi ya bacteria kusambaa kwenye damu, hii ni hali ya hatari inayotokea pale mwili unapopata mwitikio mkali na usiodhibitiwa dhidi ya maambukizi, na kusababisha viungo vya mwili kuanza kuathirika.
Katika hali mbaya, bakteria wanaosababisha maambukizi ya figo au sehemu nyingine za mfumo wa mkojo wanaweza kusababisha sepsis.
Dalili za sepsis
- Homa kali au joto la mwili kushuka sana.
- Kutetemeka kwa baridi.
- Mapigo ya moyo kwenda kasi.
- Kupumua haraka au kwa shida.
- Hali ya Kuchanganyikiwa au kupoteza fahamu.
- Kizunguzungu kikali au udhaifu mkubwa wa mwili.
- Kupungua kwa kiasi cha mkojo n.k.
Madhara yake
Sepsis inaweza kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa viungo muhimu kama figo na mapafu. Bila matibabu ya haraka, inaweza kuhatarisha maisha.
Si kila UTI husababisha sepsis. Hata hivyo, ni muhimu kutambua dalili hizi mapema na kutafuta huduma ya dharura.
5. Uharibifu wa figo na kupungua kwa uwezo wake wa kufanya kazi
UTI ya kawaida kwenye kibofu haisababishi moja kwa moja figo kushindwa kufanya kazi. Hatari huongezeka pale maambukizi yanapofika kwenye figo, yanaporudia mara kwa mara au yanapochelewa kutibiwa.
Uharibifu unaweza kutokeaje?
Maambukizi makali ya bacteria kwenye figo yanaweza kuharibu baadhi ya tishu zake. Katika hali fulani, uharibifu huo unaweza kusababisha makovu kwenye figo na kupunguza uwezo wake wa kuchuja uchafu kutoka kwenye damu.
Madhara yanayoweza kutokea
- Kupungua kwa uwezo wa figo kufanya kazi.
- Ugonjwa sugu wa figo katika baadhi ya wagonjwa.
- Kuongezeka kwa shinikizo la damu katika hali fulani.
- Kushindwa kwa figo katika hali kali.
Hata hivyo, watu wengi wanaopata maambukizi ya figo na kutibiwa mapema hupona bila kupata uharibifu wa kudumu.
Hatari huwa kubwa zaidi kwa watu wenye kisukari, matatizo ya awali ya figo, kinga dhaifu au maambukizi yanayojirudia.
6. Matatizo ya kiutendaji wakati wa tendo la ndoa
UTI inaweza kuathiri uwezo wa tendo la ndoa kwa sababu ya maumivu, usumbufu wakati wa kukojoa na hofu inayotokana na ugonjwa.
Ikiwa maambukizi yamehusisha tezi dume, mwanaume anaweza pia kupata maumivu wakati wa kumwaga shahawa.
Matatizo yanayoweza kujitokeza
- Maumivu wakati wa kumwaga shahawa.
- Kupungua kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa kutokana na maumivu au kutokuwa vizuri.
- Usumbufu wakati wa tendo la ndoa.
- Matatizo ya Kiutendaji wakati wa tendo kwa baadhi ya wanaume wenye hasa wenye shida ya kuvimba kwa tezi dume kwa Sababu ya maambukizi ya bacteria(prostatitis).
Je, UTI husababisha mwanaume kushindwa kusimamisha uume moja kwa moja?
Hapana. UTI haisababishi moja kwa moja tatizo la Kushindwa kusimamisha uume kwa kila mwanaume. Hata hivyo, maumivu yanayoendelea, prostatitis sugu na matatizo mengine yanayohusiana na afya ya mfumo wa uzazi yanaweza kuathiri utendaji wa tendo la ndoa kwa baadhi ya wagonjwa.
Ikiwa tatizo la kusimamisha uume linaendelea hata baada ya maambukizi kutibiwa, ni muhimu kupata uchunguzi wa daktari.
7. Maumivu ya muda mrefu na UTI inayojirudia
Baadhi ya wanaume hupata UTI mara kwa mara au dalili zinazoendelea hata baada ya kutumia dawa.
Hali hii inaweza kusababishwa na mambo mbalimbali, kama vile:
- Maambukizi ambayo hayakutibiwa kwa dawa inayofaa.
- Kutomaliza dozi ya dawa kama ilivyoelekezwa.
- Tezi dume iliyoongezeka ukubwa na kuzuia mkojo kutoka vizuri.
- Mawe kwenye mfumo wa mkojo.
- Tatizo la kimuundo katika mfumo wa mkojo.
- Hali ya kuvimba tezi dume(Prostatitis) kutokana na maambukizi ya bakteria inayojirudia mara kwa mara.
UTI inayojirudia haipaswi kuchukuliwa kuwa ni hali ya kawaida. Mwanaume anapopata maambukizi yanayorudia, anahitaji kuchunguzwa ili kubaini chanzo chake badala ya kuendelea kutumia antibiotiki bila vipimo vinavyofaa.
8. Kujikusanya kwa usaha kwenye tezi dume au figo
Katika hali isiyo ya kawaida, maambukizi ya bakteria yanaweza kusababisha usaha kujikusanya ndani ya tishu za tezi dume au figo.
Tatizo hili linaweza kutokea hasa pale maambukizi yanapokuwa makali au yasipotibiwa ipasavyo.
Dalili zinazoweza kuashiria tatizo kubwa
- Homa inayoendelea.
- Maumivu makali kwenye nyonga, sehemu ya chini ya tumbo au ubavuni.
- Kushindwa kukojoa.
- Hali ya mwili kuendelea kuwa mbaya licha ya kuanza matibabu.
Hali hii inaweza kuhitaji matibabu maalumu hospitalini, yakiwemo antibiotiki na wakati mwingine utaratibu wa kutoa usaha.
Si kila UTI husababisha hali hii ya Usaha. Hili ni tatizo lisilotokea mara nyingi, lakini linahitaji kutambuliwa na kutibiwa mapema.
Je, UTI kwa mwanaume inaweza kusababisha utasa?
Hili ni swali muhimu kwa wanaume wengi.
UTI ya kawaida haimaanishi moja kwa moja kwamba mwanaume atakuwa tasa.
Hata hivyo, maambukizi yanapohusisha viungo vya uzazi, kama tezi dume au korodani na mirija inayohusiana na korodani, yanaweza kuathiri afya ya uzazi kutegemea kiungo kilichoathirika na ukali wa maambukizi.
Pia, baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kusababisha dalili zinazofanana na UTI. Kwa hiyo, mwanaume mwenye maumivu ya korodani, usaha kutoka kwenye uume au dalili baada ya kufanya ngono bila kinga anapaswa kuchunguzwa ili kubaini chanzo halisi.
Ni muhimu kutofautisha UTI na magonjwa ya zinaa kwa sababu chanzo na matibabu yake yanaweza kutofautiana.
Sababu zinazoweza kuongeza hatari ya UTI kwa mwanaume
Ingawa UTI hutokea mara nyingi zaidi kwa wanawake, wanaume wanaweza kuipata kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo:
- Tezi dume kuongezeka ukubwa: Hii inaweza kuzuia mkojo kutoka vizuri na kufanya kibofu kisimalize kutoa mkojo wote. Hali hii huongeza hatari ya bacteria kuzaliana zaidi
- Mawe kwenye mfumo wa mkojo: Yanaweza kuzuia mtiririko wa mkojo na kuongeza hatari ya maambukizi.
- Kutumia mpira wa kupitisha mkojo (catheter): Unaweza kurahisisha bakteria kuingia kwenye mfumo wa mkojo.
- Kisukari: Kinaweza kuongeza hatari ya maambukizi, hasa kisipodhibitiwa vizuri.
- Matatizo ya kimuundo ya mfumo wa mkojo: Yanaweza kuzuia mkojo kupita au kutoka vizuri,Kisha kuongeza hatari ya maambukizi ya bacteria hawa.
- Magonjwa ya zinaa: Baadhi yake yanaweza kusababisha maumivu wakati wa kukojoa na uchafu kutoka kwenye mrija wa mkojo, hivyo kuhitaji uchunguzi tofauti.
Ni muhimu kutambua kwamba si kila maumivu wakati wa kukojoa ni UTI. Vipimo vinaweza kuhitajika ili kubaini chanzo sahihi.
Jinsi ya kujikinga na madhara ya UTI kwa mwanaume
Ili kupunguza hatari ya matatizo yanayoweza kutokana na UTI:
- Nenda hospitalini mapema: Ukipata dalili za UTI, pata uchunguzi badala ya kusubiri maambukizi yapone yenyewe. Au kwa Ushauri zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584.
- Fanya kipimo cha mkojo: Daktari anaweza kuagiza kipimo cha mkojo Urinalysis(Urine test) na, inapohitajika unaweza kufanya urine culture.
- Tumia dawa ulizoandikiwa kwa usahihi: Ikiwa umepewa antibiotiki, fuata maelekezo ya mtaalamu wa afya.
- Usitumie antibiotiki kiholela: Dawa isiyofaa inaweza kushindwa kutibu maambukizi na kuchangia usugu wa bakteria dhidi ya dawa.
- Kunywa maji ya kutosha: Husaidia kuzuia upungufu wa maji mwilini na kufanya mkojo utoke mara kwa mara, isipokuwa umeelekezwa na daktari kupunguza maji.
- Chunguza UTI inayojirudia: Daktari anaweza kuchunguza kama kuna tatizo la tezi dume, mawe au kuziba kwa njia ya mkojo.
- Zingatia afya ya kingono: Tumia kondomu kwa usahihi na pata vipimo vya magonjwa ya zinaa ikiwa kuna uwezekano wa maambukizi.
Kwa wanaume, UTI inayoshukiwa inahitaji tathmini ya mtaalamu wa afya kwa sababu wakati mwingine huhusishwa na tatizo jingine la mfumo wa mkojo.
Wakati gani mwanaume mwenye UTI anapaswa kwenda hospitalini haraka?
Tafuta huduma ya afya haraka au kwa Ushauri zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584, ikiwa una dalili zifuatazo:
- Homa au kutetemeka kwa baridi.
- Maumivu ya mgongo au ubavuni.
- Damu kwenye mkojo.
- Kutapika au kushindwa kunywa maji.
- Maumivu makali ya sehemu ya chini ya tumbo.
- Dalili zinazozidi kuwa mbaya au kutopungua baada ya kuanza matibabu.
Nenda hospitalini mara moja ikiwa huwezi kukojoa kabisa, unachanganyikiwa, unapata shida ya kupumua au una dalili za hali mbaya ya mwili. Hizi zinaweza kuashiria tatizo linalohitaji matibabu ya dharura.
Reviews;
UTI kwa mwanaume ni tatizo linaloweza kutibika, lakini kuchelewa kupata matibabu au kutumia dawa bila uchunguzi kunaweza kuongeza hatari ya matatizo kama maambukizi ya figo, kuvimba kwa tezi dume, kushindwa kukojoa na, katika hali kali kupata sepsis.
Si kila mwanaume mwenye UTI atapata madhara haya. Hatari hutegemea sehemu iliyoathirika, chanzo cha maambukizi, hali ya afya ya mgonjwa na jinsi anavyopata matibabu.
Ushauri muhimu: Mwanaume mwenye dalili za UTI anapaswa kupata uchunguzi wa kitabibu mapema ili kubaini chanzo cha maambukizi na kupata matibabu yanayofaa.
kwa Ushauri zaidi na Tiba tuwasiliane +255758286584.
References;
- Centers for Disease Control and Prevention (CDC). Clinical Overview of Urinary Tract Infections.
- National Health Service (NHS). Urinary Tract Infections (UTIs).
- National Health Service (NHS). Prostatitis.
- National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK). Prostatitis: Inflammation of the Prostate.
- National Institute of Diabetes and Digestive and Kidney Diseases (NIDDK). Definition & Facts of Kidney Infection (Pyelonephritis).
- National Institute for Health and Care Excellence (NICE). Urinary Tract Infection (Lower): Antimicrobial Prescribing — Summary of the Evidence.
Ushauri,Elimu,Tiba
Medical Consultation: Karibu afyaclass Kwa Ushauri na Tiba, Kama una Tatizo lolote la kiafya, tafadhali Wasiliana na Daktari moja kwa moja hapa || Call au Sms(+255758286584) au Whatsapp.
Je, unahitaji ushauri binafsi au matibabu ya tatizo lolote?
💬 Wasiliana na Daktari Hapa(Whatsapp)

