Magonjwa
Maambukizi ya Dengue wakati wa ujauzito huweza kudhuru afya ya watoto wachanga
Maambukizi ya Dengue wakati wa ujauzito huweza kudhuru afya ya watoto wachanga:
Utafiti unaonyesha kwamba hata maambukizi madogo ya Dengue yanahusishwa na tatizo la kuzaa watoto wenye uzito mdogo na hatari ya kulazwa hospitalini.
Takwimu zinaonyesha Watoto ambao mama zao walikuwa na homa ya dengue wakati wa ujauzito wako katika hatari kubwa ya kuzaliwa na uzito mdogo na kuhitaji matibabu/huduma ya hospitali katika miaka yao mitatu ya kwanza ya maisha,
Watafiti wametaka dengue kuongezwa katika orodha ya magonjwa yanayowasumbua wajawazito, ambayo wanawake wanashauriwa kuchukua hatua za kuepuka kwa sababu ya hatari kwa watoto wao ambao hawajazaliwa.
Ugonjwa wa dengue wakati wa ujauzito ulisababisha ongezeko la asilimia 27% la hatari ya kulazwa hospitalini katika miaka mitatu ya kwanza ya maisha, na kuongeza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu(medical expenditures).
Dengue ni maambukizi ya virusi yanayosambazwa kwa kung’atwa na aina kadhaa za mbu aina ya Aedes, ambapo inatishia afya ya takriban nusu ya idadi ya watu duniani.
Ingawa visa vingi havina dalili yoyote, virusi hivyo vinaweza kusababisha ugonjwa wa homa kali, na mara kwa mara kifo, lakini bado kumekuwa na ushahidi mdogo wa kuhusisha matokeo mabaya zaidi kwa Watoto wanaozaliwa hadi sasa.
Watafiti katika Vyuo Vikuu vya Surrey na Birmingham nchini Uingereza walichambua rekodi za afya kwa wanawake na watoto wanaoishi katika jimbo lenye wakazi wengi kusini-mashariki mwa Brazili la Minas Gerais kati ya Mwaka 2011 na 2017, wakiunganisha takwimu za kuzaliwa, vifo, kulazwa hospitalini na maambukizi ya dengue kwa muda.
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la American Economic Journal: Applied Economics, uligundua kuwa maambukizi ya dengue ya wastani wakati wa ujauzito yalihusishwa na kuzaliwa kwa watoto wachanga wenye Uzito mdogo.
Athari hiyo ilijitokeza haswa kwa watoto wachanga walio katika kiwango cha chini mwisho kwenye kipimo yaani “lower end of the birth weight scale”, na ongezeko la asilimia 15%, 67%, na 133% katika matukio ya kuzaliwa kwa uzito wa chini(low birth weight) na Uzito wa chini sana(extremely low-birth weight). Hii inasikitisha kwa sababu tafiti za awali zimehusisha tatizo la Uzito mdogo kwa watoto wanaozaliwa na hali duni ya afya kwa muda mrefu,hali ya kijamii na hali duni ya kiuchumi.
Watafiti pia waligundua kuwa dengue wakati wa ujauzito ilisababisha ongezeko la asilimia 27% la hatari ya kulazwa hospitalini wakati wa miaka mitatu ya kwanza ya maisha, na iliongeza kwa kiasi kikubwa gharama za matibabu(medical expenditures).
Mwandishi mwenza wa utafiti huo Dk Martin Foureaux Koppensteiner katika Chuo Kikuu cha Surrey alisema: “Sasa kuna ushahidi wa kutosha juu ya madhara ya maambukizi ya dengue kwenye uzazi hasa wakati wa mtoto kuzaliwa. Hii Inasisitiza umuhimu wa kuongeza ufahamu, kuzuia, na kuchukua hatua zinazolengwa ili kupunguza athari za ugonjwa huu ulioenea kwa afya ya mama na mtoto.”
Alipendekeza kuwa homa ya dengue inapaswa kuongezwa kwenye orodha inayoitwa TORCH,
TORCH: ni Orodha ya maambukizi au magonjwa yanayohitaji kudhibitiwa na kuepukwa wakati wa ujauzito – Hii ni pamoja na maambukizi kama vile;
- toxoplasmosis,
- rubela,
- VVU,
- kaswende,
- tetekuwanga,
- Zika,
- Pamoja na virusi vya herpes simplex.
” Kuweka homa ya dengue katika orodha hii,itahakikisha kwamba wajawazito wanafahamu hatari zinazotokana na maambukizi haya wakati wa ujauzito na wanaweza kuchukua tahadhari kama vile ya kutumia dawa za kuua wadudu,kujikinga n.k” alisema Dk Martin Foureaux Koppensteiner.