WHO
WHO yazindua mwongozo mpya wa kupunguza vifo vya kuzama majini duniani
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vifo vya Kuzama Majini yanayofanyika kila mwaka tarehe 25 Julai, Shirika la Afya Duniani (WHO) limezindua kifurushi kipya cha kitaalamu kinachoitwa PROTECT, chenye lengo la kusaidia serikali na jamii kutekeleza hatua saba zilizothibitishwa kisayansi za kupunguza vifo vinavyotokana na kuzama majini.
Kwa mujibu wa WHO, takribani watu 300,000 hufariki dunia kila mwaka kutokana na kuzama majini. Tatizo hili pia ni miongoni mwa sababu 10 kuu za vifo kwa watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 14. Vifo vingi hutokea kwenye mito, maziwa, visima, matenki ya kuhifadhi maji nyumbani na mabwawa ya kuogelea.
WHO inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya vifo hivi hutokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ambako hatua za usalama na huduma za uokoaji bado hazijaimarishwa vya kutosha.
Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari
WHO imeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya watu kuzama kutokana na kuongezeka kwa matukio ya mafuriko, dhoruba na vipindi vya joto kali.
Tafiti zinaonyesha kuwa joto kali lina uhusiano mkubwa na ongezeko la vifo vya kuzama. Kwa mfano, nchini Uingereza, utafiti umebaini kuwa vifo vya kuzama huongezeka kwa asilimia 7.2 kwa kila nyuzi joto 1°C zinazoongezeka, huku hatari ikiwa karibu mara tano zaidi siku ambazo joto linazidi 25°C ikilinganishwa na siku zenye joto chini ya 10°C.
Hatua saba za PROTECT
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema kila kifo cha kuzama ni janga ambalo mara nyingi linaweza kuzuilika.
Kifurushi cha PROTECT kinapendekeza hatua saba muhimu:
- Kuboresha miundombinu ili watu wawe salama wanapotumia maeneo ya maji.
- Kuimarisha uwezo wa uokoaji na huduma za kufufua maisha kwa waokoaji na wananchi.
- Kuboresha usalama kwa watu wanaofanya kazi karibu na maji.
- Kuweka viwango madhubuti vya usalama katika usafiri wa majini.
- Kufundisha watoto na jamii ujuzi wa kuogelea na usalama wa majini.
- Kuimarisha mifumo ya uangalizi na ulinzi wa watoto.
- Kujiandaa kukabiliana na mafuriko na majanga mengine yanayohusiana na maji.
Ghana yazindua rasmi mwongozo huo
WHO imezindua rasmi kifurushi cha PROTECT nchini Ghana, ikitambua juhudi za nchi hiyo katika kuimarisha usalama wa majini.
Takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 1,100 hufariki kwa kuzama kila mwaka nchini Ghana, sawa na wastani wa vifo vitatu kila siku, huku watoto na vijana wakiwa katika hatari kubwa zaidi.
Wito wa ushirikiano
Kaulimbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Vifo vya Kuzama Majini ni “Unite to turn the tide” (Tuungane kubadili mwelekeo), ikisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta mbalimbali na jamii katika kuzuia vifo vinavyotokana na kuzama majini.
WHO imeeleza kuwa utekelezaji wa hatua hizi unaweza kuokoa maelfu ya maisha kila mwaka, hasa katika nchi zinazoendelea ambako athari za kuzama majini bado ni kubwa.
Chanzo
- World Health Organization (WHO): Ahead of World Drowning Prevention Day, WHO launches PROTECT technical package to reduce drowning deaths.
- Global Strategy for Drowning Prevention (WHO).
