magonjwa
Sababu ya mikono kufa ganzi
Sababu 12 Za Mikono Kufa Ganzi: DALILI HII INASABABISHWA NA NINI?
Mikono kufa ganzi ni hali ambayo mtu hupoteza hisia za kawaida katika mikono au vidole. Mtu anaweza kuhisi kama anachomwa chomwa na sindano ndogo, kutambaa kwa wadudu, kuwaka moto, au kushindwa kuhisi anapogusa kitu.
Kitaalamu, hali hii huitwa Hand Numbness au Paresthesia kutegemea aina ya hisia zinazojitokeza.
Mikono kufa ganzi hutokea pale ambapo mishipa ya fahamu (Nerves) inapopata msukumo, kubanwa, kujeruhiwa au kuharibika kiasi cha kushindwa kusafirisha taarifa za hisia kwenda kwenye ubongo vizuri.
Zifuatazo ni sababu kuu zinazoweza kusababisha hali hii.
1. Kubanwa kwa mishipa ya fahamu kwenye kifundo cha mkono (Carpal Tunnel Syndrome)
Carpal Tunnel Syndrome ni mojawapo ya sababu zinazoweza kusababisha mikono kufa ganzi.
Hali hii hutokea pale mshipa wa fahamu unaoitwa Median Nerve unapobanwa kwenye kifundo cha mkono.
Chat Nasi Whatsapp
"Ungana na Wasomaji zaidi ya 12,000 wanaopata huduma ndani ya afyaclass, Kama unachangamoto yoyote ya kiafya; Kwa Ushauri&Tiba tuwasiliane hapa kupitia WhatsApp, Kama huna Whatsapp tuma SMS au Piga +255758286584."
Chat WhatSapp HapaMshipa huu unapobanwa, mtu anaweza kupata:
- Ganzi kwenye kidole gumba.
- Ganzi kwenye kidole cha shahada.
- Ganzi kwenye kidole cha kati.
- Maumivu kwenye kifundo cha mkono.
- Mikono kufa ganzi zaidi wakati wa usiku.
Hali hii inaweza kuwapata watu wanaofanya kazi zinazohusisha matumizi ya mara kwa mara ya mikono na vifundo vya mikono. Pia inaweza kujitokeza wakati wa ujauzito kutokana na kuongezeka kwa maji mwilini na uvimbe unaoweza kuongeza shinikizo kwenye mshipa wa fahamu.
2. Ugonjwa wa Kisukari (Diabetes Mellitus)
Kisukari ni sababu nyingine inayoweza kusababisha mikono na miguu kufa ganzi.
Mtu anapokuwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa muda mrefu, hali hii inaweza kuharibu mishipa ya fahamu inayosafirisha taarifa za hisia kutoka sehemu mbalimbali za mwili kwenda kwenye ubongo.
Uharibifu huu huitwa Diabetic Peripheral Neuropathy.
Dalili zake ni pamoja na:
- Mikono na miguu kufa ganzi.
- Kuhisi kama unachomwa na sindano.
- Maumivu au hisia kama ya kuwaka moto.
- Kupungua kwa uwezo wa kuhisi mguso.n.k
Mara nyingi, hali hii inayosababishwa na Ugonjwa wa kisukari huanza kuathiri miguu kabla ya mikono.
3. Upungufu wa Vitamin B12
Vitamin B12 ni muhimu katika utengenezaji na utunzaji wa mfumo wa mishipa ya fahamu.
Upungufu wa vitamin hii unaweza kusababisha uharibifu wa mishipa ya fahamu na kuleta hali inayojulikana kama Peripheral Neuropathy.
Mtu mwenye upungufu wa Vitamin B12 anaweza kupata shida ya:
- Mikono na miguu kufa ganzi.
- Kuhisi kuchomachoma kwenye vidole.
- Misuli kuwa dhaifu.
- Kupoteza usawa wakati wa kutembea.
- Uchovu kutokana na upungufu wa damu unaoweza kuambatana na hali hiyo.
4. Matatizo ya pingili za shingo (Cervical Spondylosis)
Pingili za shingo zina jukumu muhimu katika kulinda uti wa mgongo na mishipa ya fahamu inayokwenda kwenye mikono.
Mabadiliko yanayotokea kwenye pingili za shingo kadiri umri unavyoongezeka yanaweza kusababisha mishipa ya fahamu kubanwa.
Hali hii inaweza kusababisha:
- Ganzi kwenye mikono au vidole.
- Maumivu ya shingo.
- Maumivu yanayosambaa kutoka shingoni kwenda begani na mkononi.
- Udhaifu wa misuli ya mikono.
Wakati mwingine, tatizo linaweza kusababishwa na diski ya pingili za shingo kutoka nje ya nafasi yake na kubana mshipa wa fahamu.
5. Kulalia mkono au kuuweka kwenye mkao usiofaa
Je, umewahi kuamka asubuhi na kukuta mkono umekufa ganzi?
Hali hii inaweza kusababishwa na kulalia mkono au kuuweka katika mkao unaobana mishipa ya fahamu kwa muda mrefu.
Shinikizo hilo linaweza kuathiri mawasiliano ya mishipa ya fahamu kwa muda mfupi na kusababisha:
- Ganzi.
- Hali ya Kuchomachoma.
- Kupungua kwa hisia.
Mara nyingi hali hii huisha baada ya kuondoa shinikizo na kubadilisha mkao wa mkono.
Hata hivyo, ikiwa ganzi inajirudia mara kwa mara au inadumu kwa muda mrefu, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi.
6. Kubanwa kwa mshipa wa fahamu kwenye kiwiko (Cubital Tunnel Syndrome)
Hali hii hutokea pale mshipa wa fahamu unaoitwa Ulnar Nerve unapobanwa kwenye eneo la kiwiko.
Mshipa huu unapobanwa unaweza kusababisha:
- Ganzi kwenye kidole kidogo.
- Ganzi kwenye kidole cha nne (Ring Finger).
- Maumivu kwenye kiwiko.
- Udhaifu wa kushika vitu.
Watu wanaokaa muda mrefu wakiwa wameegemeza viwiko kwenye meza au wanaokunja viwiko kwa muda mrefu wanaweza kuwa katika hatari zaidi.
7. Upungufu wa damu au matatizo ya mzunguko wa damu
Mzunguko wa damu una umuhimu mkubwa katika kupeleka oksijeni na virutubisho kwenye tishu mbalimbali za mwili, ikiwemo mishipa ya fahamu.
Matatizo ya mishipa ya damu yanayopunguza usambazaji wa damu yanaweza kuathiri utendaji wa mishipa ya fahamu na kusababisha ganzi.
Pia, hali inayoitwa Raynaud’s Disease husababisha mishipa midogo ya damu kwenye vidole kubana, hasa mtu anapopata baridi au msongo wa mawazo.
Dalili zake zinaweza kuwa:
- Vidole kuwa vyeupe.
- Vidole kuwa vya bluu.
- Vidole kuwa na ganzi.
- Maumivu au kuchomachoma wakati damu inaporejea.
Ni muhimu kutofautisha upungufu wa damu (Anemia) na matatizo ya mzunguko wa damu, kwa sababu si kila mtu mwenye anemia hupata ganzi ya mikono.
8. Matatizo ya tezi ya thyroid (Hypothyroidism)
Tezi ya thyroid inapozalisha homoni chache kuliko mahitaji ya mwili, hali hiyo huitwa Hypothyroidism.
Hali hii inaweza kuhusishwa na kuvimba kwa tishu zinazozunguka mishipa ya fahamu au kuongeza uwezekano wa kupata Carpal Tunnel Syndrome.
Mgonjwa anaweza kupata:
- Mikono kufa ganzi.
- Uchovu wa mara kwa mara.
- Kuongezeka uzito.
- Kuhisi baridi kupita kiasi.
- Ngozi kukauka.
9. Matumizi ya pombe kupita kiasi
Matumizi ya pombe kwa muda mrefu yanaweza kuharibu mishipa ya fahamu.
Hali hii huitwa Alcoholic Neuropathy.
Madhara yake yanaweza kujumuisha:
- Ganzi kwenye mikono na miguu.
- Maumivu ya kuchoma moto.
- Udhaifu wa misuli.
- Kupungua kwa uwezo wa kuhisi mguso.
Pia, matumizi makubwa ya pombe yanaweza kuambatana na upungufu wa virutubisho muhimu kwa afya ya mishipa ya fahamu.
10. Matumizi ya baadhi ya dawa
Baadhi ya dawa zinaweza kuathiri mishipa ya fahamu na kusababisha ganzi kama madhara yake.
Mifano ni:
- Baadhi ya dawa za saratani (Chemotherapy).
- Baadhi ya dawa zinazotumika kutibu maambukizi ya HIV.
- Baadhi ya antibiotiki zinapotumika kwa muda mrefu.
Mtu anayepata dalili hizi baada ya kuanza dawa mpya anashauriwa kuzungumza na mtaalamu wa afya. Asiache dawa alizoandikiwa bila ushauri.
11. Magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu (Multiple Sclerosis)
Multiple Sclerosis ni ugonjwa unaoathiri mfumo mkuu wa fahamu, yaani ubongo na uti wa mgongo.
Katika ugonjwa huu, kinga ya mwili hushambulia utando unaolinda nyuzi za mishipa ya fahamu unaoitwa Myelin Sheath.
Matokeo yake ni kuvurugika kwa mawasiliano kati ya ubongo na sehemu mbalimbali za mwili.
Dalili zinaweza kujumuisha:
- Mikono au miguu kufa ganzi.
- Udhaifu wa misuli.
- Matatizo ya kuona.
- Kupoteza uratibu wa mwili.
- Matatizo ya kutembea.
12. Kiharusi (Stroke)
Kiharusi hutokea pale ambapo usambazaji wa damu kwenye sehemu ya ubongo unakatika au mshipa wa damu kwenye ubongo unapopasuka.
Hali hii inaweza kuathiri sehemu ya ubongo inayodhibiti hisia na mienendo ya mikono.
Mtu anaweza kupata ganzi ya ghafla upande mmoja wa mwili, ikiwemo mkono mmoja.
Dalili za hatari ni:
- Mkono mmoja kuwa dhaifu au kufa ganzi ghafla.
- Uso kupinda upande mmoja.
- Kushindwa kuzungumza vizuri.
- Kupoteza uwezo wa kuona vizuri ghafla.
- Kupoteza usawa au kupata kizunguzungu kikali.
Hizi ni dalili zinazohitaji huduma ya dharura hospitalini. Usisubiri kuona kama zitapona zenyewe.
VIPI MTU ANAYEPATA GANZI YA MIKONO ANAPASWA KUCHUNGUZWA?
Matibabu ya mikono kufa ganzi hutegemea chanzo cha tatizo. Mgonjwa anaweza kuhitaji uchunguzi mbalimbali kulingana na historia na dalili zake.
Vipimo vinavyoweza kuhitajika ni:
- Blood Glucose / HbA1c – kuchunguza kisukari.
- Vitamin B12 – kuchunguza upungufu wa Vitamin B12.
- Thyroid Function Tests – kuchunguza matatizo ya tezi ya thyroid.
- Full Blood Count (FBC) – kuchunguza hali ya damu.
- Nerve Conduction Study – kuchunguza utendaji wa mishipa ya fahamu.
- MRI au X-ray ya shingo – inapokuwa kuna dalili zinazoashiria tatizo la pingili za shingo.
Si kila mgonjwa anahitaji vipimo vyote; daktari ataamua kulingana na hali ya mgonjwa.
Bonus point;
Mikono kufa ganzi si ugonjwa mmoja, bali ni dalili inayoweza kusababishwa na matatizo mbalimbali, kuanzia kubanwa kwa mishipa ya fahamu, kisukari, upungufu wa Vitamin B12, matatizo ya shingo mpaka magonjwa yanayoathiri mfumo wa fahamu.
Muhimu: Ikiwa mikono inakufa ganzi mara kwa mara, ganzi inadumu kwa muda mrefu au inaambatana na udhaifu wa misuli, ni muhimu kwenda hospitalini kwa uchunguzi ili kubaini chanzo halisi.
Ganzi inayoanza ghafla pamoja na dalili za kiharusi inahitaji huduma ya dharura.
Kwa Ushauri Zaidi,Elimu na Tiba tuwasiliane +255758286584.
REFERENCES;
- Mayo Clinic Staff. (2025, July 31). Numbness in hands: Causes and definition. Mayo Clinic.
- National Institute of Arthritis and Musculoskeletal and Skin Diseases (NIAMS). (n.d.). Carpal tunnel syndrome. National Institutes of Health.
- MedlinePlus. (n.d.). Numbness and tingling. U.S. National Library of Medicine.
- NHS. (n.d.). Peripheral neuropathy. National Health Service.
- NHS. (n.d.). Causes of peripheral neuropathy. National Health Service.
- NHS. (n.d.). Pins and needles. National Health Service.
- Mayo Clinic Staff. (n.d.). Peripheral neuropathy: Symptoms and causes. Mayo Clinic.
- Mayo Clinic Staff. (2025, October 31). Numbness: Causes and definition. Mayo Clinic.
Ushauri,Elimu,Tiba
Medical Consultation: Karibu afyaclass Kwa Ushauri na Tiba, Kama una Tatizo lolote la kiafya, tafadhali Wasiliana na Daktari moja kwa moja hapa || Call au Sms(+255758286584) au Whatsapp.
Je, unahitaji ushauri binafsi au matibabu ya tatizo lolote?
💬 Wasiliana na Daktari Hapa(Whatsapp)

